Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira MORUWASA,kujenga uzio katika bwawa la Mindu lililopo Manispaa ya Morogoro, ili kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika kando mwa bwawa hilo ikiwemo kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha pamoja na wadau wa maji cha kujadili mikakati mbalimbali itakayosaidia kuondoa tatizo la maji mkoani humo.

“Kuzunguka bwawa la Mindu hakuna mtu yoyote atakayeruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu, tunaweka uzio “amesema.

Amesema bwawa hilo linategemewa kwaajili ya maji kwa matumizi ya binadamu kwa miaka 50,000 ijayo, hivyo upo umuhimu mkubwa wa kulihifadhi na kulitunza.

Pia amesema wataweka mabango makubwa nyenye zuio la mtu yoyote kuingia katika bwawa hilo, sambamba na kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti zaidi katika bwawa hilo

Chifu wa kabila la Waluguru Kingalu Mwana Banzi wa 15 akizingumza na waandishi wa habari, alisema hali ya vyanzo vya maji siyo nzuri kwa sasa na kuiomba serikali na wadau mbalimbali kuungana na machifu kwaajili ya kunusuru hali hiyo.

“Sisi machifu tunauwezo wa kuombea mvua ikanyesha na pia tunaweza kuzuia majanga mbalimbali kwa kutumia mila na desturi zetu”amesema.

Amesema tangu enzi za baba wa Taifa mila na desturi zilitumika katika kuombea mvua na majanga mengine, hivyo sio jambo geni kwa Watanzania hivyo ni muhimu likaendelea kupewa nafasi.

Pia aliomba Rais Samia Hassan Suluhu kutumia rungu lake kuzuia mashine za kukata miti maarufu kama chenso ambazo zimekuwa kisababishi kikubwa cha ukataji miti hovyo na hivyo kuharibu mazingira na kusababisha kukosekana kwa mvua.

“Chenso ni tatizo kubwa,namuomba Rais Samia atoe zuio ili zisitumike kupunguza huu uharibifu wa mazingira,” amesema.

Pia ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya bidhaa za chuma ili watengenezaji wa bidhaa za miti wawe na mbadala huo