Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali ipo tayari kupeleka mabadiliko ya sheria ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho kukubaliana baadhi ya mapendekezo hayo.

Akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma leo Novemba 9, 2022,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye,amesema kuwa Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari.

“Serikali ina nia ya njema kwani haikupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni kwa kuwa kulikuwa kuna maeneo ambayo wadau wa habari na Serikali hawakukubaliana.

“Sisi kama Serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya Serikali mpaka sasa bado ni njema. Lakini Serikali ilishindwa kupeleka mapendekezo katika Bunge la Novemba kwa kuwa kulikuwa bado taratibu zingine hazikukamilika ” amesema.

Amesema kuwa katika kikao cha mwisho ndicho kitakachotoa mwelekeo wa kupelekea mapendekezo hayo bungeni hivyo Serikali haipo kimya bali ipo katika mchakato wa kufanikisha mabadiliko hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben,amesema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

“Tutoe mawazo yetu ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliana ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka.
Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ amesema.

Naye Deodatus Balile,Mwenyekiti wa TEF,amewaomba wadau wa habari kushiriki vema katika kikao cha mwisho cha Serikali na wadau wa habari kwa kuwa ni muhimu kitakachofanyika Novemba 22, 2022, jijini Dar es Salaam.

“Ni vyema sasa kama kuna mtu anawazo, alilete kupitia umoja wa haki ya kupata habari ili kwenye kikao hicho tuwe na lugha moja,’’ amesema Balile.

Hata hivyo James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), amesema anaamini kuwa katika kikao cha pili,hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.

“Baada ya kikao cha pili kama ambavyo imeelezwa na serikali, tunaamini mabadiliko yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi, serikali na tasnia kwa ujumla,” amesema.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape amesema serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali.Kwenye kikao hicho Nape amesema, uhuru uliopo sasa unapaswa kutumika vizuri.

‘‘Sisi kama tupo happy (tuna furaha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ amesema.

Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

By Jamhuri