Bil.4.6/- kuibadilisha ranchi ya Kongwa

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 4.6 kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa katika ranchi ya Kongwa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mbegu bora za ng’ombe, uchimbaji wa visima na ununuzi wa matrekta.

Hayo yameainishwa na Elisa Binamungu Meneja wa Ranchi ya Kongwa wakati akisoma taarifa ya utendaji wa shamba la mifugo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua shamba la mifugo la NARCO – Kongwa ili kujionea maendeleo ya shamba na shughuli za ufugaji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Daniel Elias Mushi (kulia) na Meneja wa Ranchi ya Kongwa Bw. Elisa Binamungu wakikagua na maeneo ya Ranchi hiyo, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kufanya ziara ya kikazi katika ranchi hiyo hivi karibuni.

Bw.Binamungu alisema Serikali imeongeza uzalishaji wa nyama ya ng’ombe, ambapo ranchi ina ukubwa wa hekta 38,000 zenye uwezo wa kuweka uniti za mifugo 25,000.

“Eneo hili limegawanywa katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ina jumla ya uniti za mifugo 12,427 na sehemu ya pili ina uniti za mifugo 16,897” Amesema Binamungu.

Akizungumza na wafanyakazi na wananchi wanaozunguka eneo la ranchi hiyo Senyamule alisema tunapoongelea mifugo tunaongelea uchumi wetu na kusisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa wingi wa mifugo ikitanguliwa na Ethiopia.

“Sisi tuna mifugo mingi sana ila mazao haya ya mifugo na nyama hayauziki nje kwa kiasi kikubwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuweka msukumo Madhubuti katika eneo hili kwa kuwa lipo kundi kubwa linalotegemea mifugo” alisema Senyamuli.

Alisema,eneo la Kongwa lipo kimkakati hivyo menejimenti ya shamba hilo itumie fursa hiyo kuuza bidhaa zake na kujitangaza ipasavyo ili waweze kunufaika na uwepo wa barabara kuu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na Menejimenti, wafanyakazi na wananchi wanaozunguka eneo la ranchi ya Kongwa na kusisitiza kufanya kazi kwa weledi, kujitangaza na kuwa na ubunifu zaidi ili uwepo wa ranchi hiyo pembezoni mwa barabara kuu uweze kuwa na manufaa.

“Serikali imetoa fedha nyingi ili kurejesha shamba hili katika hali yake ya ubora wajuu zaidi, tumieni fursa hii pia kutangaza shamba hili, wengi hawalifahamu. Nitoe rai kwenu kuendelea pia kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka ili wawe walinzi namba moja wa shamba hili” Senyamule amesisitiza.

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa White Zuberi amesema kuwa ranchi ya Kongwa ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa Taifa na wana Kongwa kwa ujumla.

Ranchi ya Kongwa ni miongoni mwa Ranchi kongwe za Taifa na ipo katika Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Kongwa na kata ya Mtanana. Ranchi hii ndio ya kwanza kuanzishwa na ilianza wakati wa mkoloni.

Sehemu ya Ng’ombe ambao wanapatikana kwenye Ranchi ya NARCO iliyopo katika wilaya ya Kongwa