Na Albano Midelo, JamhuriMedia,Songea

Jumla ya shilingi bilioni 764 zinatarajia kutumika katika kutekeleza ujenzi wa barabara itakayounganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlilayoyo wilayani Namtumbo amesema ujenzi wa barabara hiyo unaanzia Kijiji cha Lumecha,Kitanda na Londo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma na Kwenda Kilosa kwa Mpepo,Malinyi,Ntivira, Lupilo, Ifakara hadi Mikumi mkoani Morogoro.

Amesema Mkandarasi wa barabara hiyo alishapatikana na fedha zitakazotumika kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo zinafahamika na kwamba mkataba umeshasainiwa na ujenzi unaanza wakati wowote.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas

Akizungumzia barabara ya Mtwara pachani wilayani Namtumbo yenye urefu wa kilometa 300 inayopita vijiji vya Ligera, Lingusenguse,Lusewa hadi Tunduru ,Naibu Waziri amesema usanifu umekamilika na kwamba maeneo yote korofi yatawekewa lami nyepesi na zege kuwezesha magari kupita mwaka mzima.

Hata hivyo amesema serikali ina mpango wa kufanya usanifu wa kina ili barabara hiyo iweze kujengwa katika kiwango cha lami ambapo amesisitiza kuwa barabara hizo zipo kwenye Ilani ya CCM ya 2020 hadi 2025 hivyo Ilani inaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo wilaya zake zote zimeunganishwa kwa lami na hivi sasa kazi ya kuunganisha kwa lami ndani ya wilaya inaendelea kutekelezwa na serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Kigoma Malima

By Jamhuri