Binti aboresha kitimwendo kuwasaidia walemavu

*Sasa kitawawezesha kufanya kazi za mikono, mazoezi kwa urahisi

*Agizo la Serikali kwa TIRDO, SIDO kushirikiana naye lapuuzwa

Dar es Salaam

Na Alex Kazenga 

Binti wa Kitanzania, Joan Mohamed (24), ameibuka na ubunifu wa aina yake utakaokifanya kitimwendo (wheelchair) kuwa na msaada zaidi kwa walemavu.

Kwa kawaida kitimwendo kimekuwa kikitumiwa na walemavu wengi kwa kuwawezesha kusukumwa kutoka sehemu moja hadi nyingine na si zaidi ya hapo.

Lakini sasa, Joan, binti kutoka Morogoro na mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Mitambo (Mechanical Engineering) katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ameongeza matumizi ya kifaa hiki maalumu kwa ubunifu wa kisasa na wa kisayansi.

Novemba mwaka jana, mwandishi wa makala hii alitembelea Maonyesho ya Teknolojia yanayofanyika kila mwaka chuoni hapo yakiwashirikisha wahitimu wa DIT ili kuonyesha ubunifu wao, na kuvutiwa na ubunifu wa Joan, aliyehitimu mwaka huo huo, kwa kuwa kwa namna moja au nyingine unayagusa maisha na hisia za walemavu wengi ndani na nje ya nchi; hasa wenye matatizo ya miguu.

Ubunifu wa Joan unakifanya kitimwendo kuwawezesha walemavu kujiinua na kusimama bila kuhitaji msaada wa mtu mwingine.

“Watu wenye ulemavu, hasa waliopooza miguu, hupitia nyakati ngumu katika maisha yao. Unakuta hawawezi kujifanyia mazoezi wala kujihudumia hata kwa kuchukua kitu kidogo tu, eti kwa kuwa ni lazima wasimame ndipo wakichukue! Hii inasikitisha sana,” anasema Joan.

Kwa kutumia kitimwendo kilichoboreshwa, tatizo hilo linaondoka, kwa kuwa mlemavu anaweza kujinyanyua (kusimama) na kuchukua kitu ambacho awali asingeweze hadi atakaposaidiwa.

Joan anasema ubunifu aliouongeza kwenye kitimwendo utawasaidia kujiendesha na kufanya mazoezi ya kusimama na kukaa bila kuhitaji msaada wa mtu mwingine.

Mbali na mazoezi, Joan anabainisha kuwa kitimwendo hicho chenye uwezo wa kujikunja na kukunjua kitawawezesha kufanya kazi za aina mbalimbali, iwe za mikono au hata za kitaaluma kama kufundisha kwa wenye taaluma ya ualimu.

Ni kawaida kwamba hakuna kinachotokea duniani bila kuwa na chanzo wala sababu, na ndivyo ilivyo kwa Joan, anayebainisha hilo kwa kuweka wazi kuwa tatizo la miguu linalomkabili bibi yake; Gladys Semwenda, mwenye umri wa miaka 74, ndicho kichocheo kilichosababisha kufikia hatua au uamuzi wake wa kuboresha kitimwendo.

Wakati Joan na familia yake wakiishi Morogoro, bibi Gladys yupo mkoani Arusha.

Katika uboreshaji alioufanya Joan anasema kwenye kitimwendo kilichokuwapo kwenye maonyesho DIT, ameweka kifaa kinachoitwa ‘pneumatic shock up, akisema kifaa hiki hufanya kazi kama pampu ya baiskeli au ‘buti‘ ya gari.

“Ndani ya kifaa hicho kuna gesi aina ya ‘hydrogen’ ambayo hubanwa ili kukiwezesha kitimwendo kufunga na kufunguka kinapokuwa kimewekewa mzigo juu yake,” anasema.

Ili shock up ambayo Joan ameifunga kwa chini katika kitimwendo cha kawaida iweze kufanya kazi ya kufunga na kufunguka, imeunganishwa na waya kama ulivyo mfumo wa breki za baiskeli.

Mfumo huo hufanya kazi bila kuathiri mfumo wa awali wa kitimwendo husika, ambapo Joan anasema ili ufanye kazi, mtumiaji anatakiwa kuminya breki kuruhusu gesi ifunguke na mtu aliyekaa kwenye kiti kuinuliwa juu.

“Hata akitaka kukaa, mtumiaji wa kitimwendo hicho ataminya breki hizo kuruhusu gesi kufungwa na kiti kuanza kujikunja ili aweze kukaa bila shida yoyote,” anasema.

Ili kuzuia mtumiaji wa kitimwendo asianguke, Joan ameweka mikanda miwili sehemu ya miguuni na kiunoni ambayo humshikilia na kumuweka sawasawa anapoinuka na kusimama bila shida.

“Mlemavu anayehitaji kufanya kazi akiwa amesimama, mathalani kupika kwa kutumia jiko la gesi au la umeme; au kusimama ubaoni (darasani) kwa ajili ya kufundisha, basi akiwa na kitimwendo cha aina hii atatekeleza majukumu hayo kwa ufanisi.

“Kwa waliopooza miguu na wanaohitaji kufanya mazoezi kunyoosha misuli, basi nao kwa kutumia kiti hiki watakuwa na uwezo wa kujifanyia mazoezi bila kutegemea msaada wa mtu mwingine,” anasema Joan.

Kwa upande mwingine, Joan anasema mbali na kuyawazia matatizo (ya miguu) yanayomkabili bibi Gladys, safari aliyowahi kuifanya nchini China ilichochea na kurahisisha uboreshaji alioufanya kwenye kitimwendo na kuimarisha ndoto aliyokuwa nayo tangu awali.

“Nimewahi kwenda China kwa ajili ya matembezi na biashara. Nikiwa kule niliona walemavu wa miguu wakitumia vitimwendo vyao huku wakiwa wamesimama! Hii ilinishitua kidogo. Nikaona kumbe hata kwetu inawezekana. Lakini kwa kweli vile vitimwendo wanavyotumia walemavu wa China vimeboreshwa zaidi, kwa kuwa vinatumia hadi umeme.

“Nilitamani kununua kimoja nimletee bibi yangu, lakini nilipoambiwa gharama za kukifikisha nchini, nilichoka kabisa,” anasema Joan.

Ili kitimwendo kilichoboreshwa kutoka China kinunuliwe na kusafirishwa hadi Tanzania, mhusika atalazimika kuingia mfukoni na kutoa zaidi ya Sh milioni 5.

Ni kutokana na ukubwa huo wa gharama ndipo Joan akapata wazo la kuboresha vitimwendo vilivyopo nchini ambavyo havina mfumo kama ule alioushuhudia China na kuamini ungekuwa msaada mkubwa kwa bibi Gladys.

Wakati wa maonyesho ambayo mwandishi huyo ameyashuhudia pale DIT, kwa mara ya kwanza Joan akakiweka hadharani kitimwendo kilichoboreshwa na kuwavutia watazamaji wengi.

Mmoja wa wadau wa sayansi na teknolojia waliovutiwa na ubunifu huo ni aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa kipindi hicho, Profesa Kitila Mkumbo.

Mara moja Profesa Mkumbo ambaye uwaziri wake umetenguliwa Januari mwaka huu na kubaki kuwa  Mbunge wa Ubungo, wakati akiwa kwenye maonyesho hayo aliagiza Joan aunganishwe na kushirikiana na taasisi za serikali zinazoshughulikia masuala ya ubunifu na zile zinazohudumia walemavu nchini.

Pamoja na pongezi kwa Joan, Prof. Mkumbo aliahidi kuanzia mwaka huu serikali itakuwa ikitoa tuzo maalumu kwa mbunifu wa kifaa, mfumo au nyenzo itakayotoa msaada wa moja kwa moja kwa jamii na kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili watu.

“Kuhitimu masomo ya daraja fulani la elimu kwa mwanafunzi yeyote yule ni jambo moja, ila kutumia elimu aliyoipata kutatua changamoto za kijamii ni jambo jingine, tena la muhimu,” anasema Prof. Mkumbo. 

Anasema nyenzo iliyobuniwa na Joan inaweza kuonekana ndogo lakini inajibu changamoto nyingi ambazo walemavu wa miguu hupitia.

“Kuna watu wengi wanahitaji kupata vitimwendo, sasa tukiona ubunifu kama huu lazima tufikirie namna ya kumuunganisha mhusika na watu waliobobea na wanaohusika katika suala hilo ili washirikiane kufanya uzalishaji mkubwa zaidi,” anasema na kubainisha kuwa ubunifu huo pia unatatua changamoto ya tatizo la ajira kwa vijana huku akisema Joan ana nafasi ya kujiingizia kipato pasipo kutegemea kuajiriwa na serikali au taasisi binafsi.

Miongoni mwa taasisi ambazo zilipaswa kumtazama Joan kwa umakini katika kutekeleza agizo la Prof. Mkumbo ni Tanzania Industrial Research and Development Organisation (TIRDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Hata hivyo, tangu Joan amepewa ahadi hiyo mwaka jana, imetimia miezi sita sasa bila kutekelezwa wala kupewa matumaini ya kusaidiwa, hali inayomlazimu sasa afikirie kutafuta wafadhili ambao watamsaidia kutimiza ndoto yake.

“Nimekata tamaa ya kuwafuatilia watu nilioambiwa kwamba watanisaidia kuniunganisha na taasisi za serikali, sasa hivi nimekiboresha kitimwendo kwa kukiongezea mfumo wa umeme.

“Mwanzoni hakikuwa na mfumo unaokiwezesha kujiendesha chenyewe. Ilikuwa mtumiaji akitaka kwenda mahali lazima asukumwe, sasa hivi nimekiongezea mfumo huo ambao atakuwa anauwasha halafu chenyewe kinaanza kutembea bila kusukumwa,” anasema.

Katika hatua ya kutaka wazo lake lionekane kwa watu wengi na aweze kupata wafadhili, Joan anadai kuwa kuna mashindano ya ubunifu yanayotarajiwa kufanyika nchini mwezi ujao, amepeleka jina lake ili ashiriki na watu wakione kitimwendo alichokiboresha.

Akizungumzia gharama za uhandisi alizotumia kuboresha kitimwendo, Joan anasema wakati wa maonyesho yaliyofanyika mwaka jana DIT alikuwa amekwisha kutumia takriban Sh 700,000 hadi kukikamilisha, na kwa kipindi hicho aliamini kuwa iwapo kingepitishwa na mamlaka za serikali, gharama hizo zingepungua hadi Sh 500,000.

“Mwanzoni niliwaza kukiuza kwa Sh 1,000,000 lakini bei hii itaongezeka kutokana na mfumo wa umeme ambao nimeongeza, gharama inaweza kupungua endapo nitapata wafadhili ili tuzalishe vitimwendo vingi,” anasema.

Katika hatua nyingine, kitimwendo kilichoboreshwa kimefungiwa kengele ya baiskeli, tofauti na vingine vinavyotumika kwa miaka mingi mitaani na hata majumbani.

Kwa nini kiwekewe kengele?

Joan anasema: “Inasikitisha kwamba watu wengi hawawajali watumiaji wa vitimwendo, hasa wanapokuwa barabarani. Wengine hata kuwapisha inakuwa vigumu, lakini kuwapo kwa kengele kutawatahadharisha wengine kuwa kuna mtu anakuja na kitimwendo.

“Hata wakiwa nyumbani wanaweza kutumia kengele kwa ajili ya kuomba msaada kwa mtu au watu waliopo nje ya nyumba. Ndiyo maana nikaona ni vema kuweka nyenzo hii itakayosaidia wengine kufahamu uwepo wa mlemavu husika katika eneo fulani,” anasema.