UJUMBE WA KWARESMA – (5) Papa Francis na ‘uongofu wa mazingira’

Jumapili ya wiki hii ni Sikukuu ya Kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo; yaani Pasaka. Kwa maana hiyo leo tunawaletea sehemu ya mwisho ya mfululizo wa Ujumbe wa Kwaresma kwa mwaka 2022 kama ulivyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC).

SURA YA TATU

Upatanisho katika maisha ya kila siku 

Wapendwa Taifa la Mungu na wote wenye mapenzi mema, dhana ya upatanisho haina budi kumgusa kila mmoja katika jamii zetu. 

Upatanisho hurejesha uhusiano uliovunjika. Ni hatua ya kupokeana tena baada ya kuhitilafiana kiasi cha kutoaminiana. Upatanisho ni hatua na kilele cha kushiriki meza moja pale mtu mmoja mmoja au jamii ya watu wanapokubaliana kuzika tofauti zao. 

Hatua hii ya upatanisho ni ngumu sana kwa vile inamtaka kila mmoja kusamehe na kutembea katika njia ya amani na utulivu. 

Kijamii 

Kama tulivyodokeza hapo awali, upatanisho unapaswa kugusa jamii zetu katika ujumla wake wote. Katika dunia ya leo ambayo watu tuna mwelekeo wa kuweka matamanio na malengo yetu binafsi mbele zaidi ya malengo ya jumuiya, kushuhudia misigano ya kijamii ni jambo la kawaida kabisa.  

Kwa mfano, tumeshuhudia mifarakano kati ya mtu na mtu, familia na familia (wazazi kati yao wenyewe, wazazi na watoto na watoto kati yao: mfano migogoro ya ndoa isiyokwisha); jamii na jamii fulani (rejea migogoro isiyokwisha kati ya wafugaji na  wakulima) na hata kundi fulani na kundi fulani; na wakati mwingine kati ya taifa na taifa. 

Matokeo ya mifarakano hiyo ni uadui kiasi cha kupoteza maelewano na kufikia kutozungumza kati ya mtu na mtu.  

Katika mazingira hayo unahitajika upatanisho ili kuzileta familia na jamii zetu pamoja na hivyo kuzirudisha katika amani na utulivu. 

Lengo na madhumuni ya upatanisho huu ni kuzirudisha katika urafiki na maelewano yaliyovunjika. Ni katika mtazamo huo tunaweza kuungana na Mt. Paulo akisema: “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya,  amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama.” (Kol 1:21-22).  

Upatanisho unahitajika katika jamii zetu ili kuwarudisha watu pamoja na kuwaponya kutoka katika majeraha ya uadui na mifarakano. Hiki ndicho kinachotusukuma kuwaandikia ujumbe huu wa Kwaresma: “Tunawasihi mpatanishwe na Mungu.” 

Maandiko Matakatifu yanatualika yakisema: “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali pia kwa dhambi za ulimwengu wote.” (1 Yoh 2:1-2).  

Upatanisho huunganisha watu, maana Kristo  mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na  watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. “Kwa maana  yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili  kuwa mmoja, akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.  Naye akiisha kuuondoa uadui kwa mwili wake akafanya  Amani.” (Efe 2:14-15).  

Wakati huu wa Kwaresma, tunazialika jamii zetu zilizotengana na kufarakana kutumia ishara na  alama za upatanisho zinazokubalika Kikristo ili zikutane na  kurejesha upya uhusiano mwema. 

Bahati nzuri ni kwamba sisi Waafrika tu matajiri wa ishara na alama hizo. Kwetu Tanzania makabila mbalimbali yana ishara na alama za upatanisho. Kwa mfano, yapo makabila ambayo hutumia chakula cha pamoja kama ishara ya kupatana. 

Kisiasa 

Kisiasa Upatanisho husaidia watu kuwa huru, kuwajibika, kwa kutetea haki zao na za wengine; kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa umoja, juhudi na maarifa; na kujenga demokrasia kwa kushiriki katika chaguzi zilizo huru na za haki. 

Mchakato wa upatanisho husaidia watu kuishi kwa umoja na amani. Lakini uovu hauwezi kwisha, maadamu tunaishi katika ulimwengu huu uliogubikwa mifarakano; na upatanisho wa kweli ni tumaini la binadamu yeyote anayemwogopa Mungu. 

Dunia inahitaji kwanza kupatanishwa na Mungu na kisha upatanisho ndani ya jamii.  Pasiwepo watu ambao maisha yaoyote ni ya manung’uniko sababu tu njia za upatanisho zimefungwa na upande wa pili.  

Sote tunaalikwa ndani ya jamii ya Kitanzania kulitazama na kulifanyia kazi hilo katika ukweli na uadilifu. 

Tukirejea barua ya SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar) ya mwaka 2013, tunaona kwamba, licha ya kwamba Kanisa halifungamani na chama chochote cha kisiasa, lina wajibu wa kuonyesha na kuhakikisha kwamba tunu msingi zitakazosaidia mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, uhuru, utu na heshima kwa  binadamu zinadumishwa. 

Tunu hizi ni muhimu katika kuunda na kukuza jamii yenye amani na utulivu; jamii yenye kuishi kwa maelewano.  

Kisiasa, ‘upatanisho’ wa kweli hupatikana katika kuitafuta, kuiishi na kuilinda demokrasia na amani dumifu. Ili kufikia demokrasia ya kweli kama njia ya kuelekea mapatano ya kweli, bado yanahitajika majadiliano kati ya wadau mbalimbali wa kisiasa na hasa katika vikao muhimu vya kutoa uamuzi. 

Hivyo basi, viongozi wetu hawana budi kubadilika kuona kwamba demokrasia na utawala bora vinashika hatamu kwa ajili ya manufaa ya wengi.  

“Tunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Mungu” ni ujumbe ambao unatuasa sisi sote tujipatanishe kati yetu na hasa pale ambapo maisha yetu ya kisiasa yamekwenda kombo. 

Vyama vyetu vya siasa vinapaswa kuwa ni majukwaa ya majadiliano yanayojengeka katika msingi wa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti, ili kujenga na kuimarisha amani na utulivu katika jamii kwa sababu: “Upatanisho ni jambo linalotangulia siasa, na kwa sababu hii wenyewe (upatanisho) ni muhimu sana kwa kazi  ya siasa yenyewe. 

“Bila nguvu ya upatanisho kuumbwa ndani ya mioyo ya watu, majukumu ya kisiasa kwa ajili ya amani  yanakosa msingi wake wa ndani.” (AM, 19). 

Wakati huu wa Kwaresma, kila mmoja katika Taifa  la Mungu anahimizwa kutekeleza wajibu wake, kwa njia ya  toba, kujenga na kudumisha moyo wa mapatano na uelewano katika jamii. 

Mazingira yetu

Mazingira ni “Uhusiano uliopo kati ya maumbile na jamii inayoishi humo.” (Laudato Si, 139). Mungu alitupatia ulimwengu na vyote vilivyomo ili tuvitunze na tuvitumie kadiri ya mpango wake. 

Uharibifu wa mazingira ni uharibifu wa mpango wa uumbaji wa Mungu. Tunapotunza mazingira, tunajitunza sisi wenyewe. “Upatanisho” na mazingira ni kurekebisha tabia ambazo zimesababisha uharibifu huo wa mazingira. (taz. Rum 8:20-21). 

Kwa kutambua umuhimu wa ‘upatanisho’ huu wa kiikolojia, Baba Mtakatifu Fransisko anaona pia nafasi ya “Mazungumzo mapya kuhusu mustakabali wa sayari. Tunahitaji mazungumzo ambayo yanajumuisha kila mtu, kwa changamoto ya mazingira tunayopitia… Tunahitaji mshikamano mpya na wa wote. 

“Sote tunaweza kushirikiana kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya utunzaji wa uumbaji, kila mmoja kulingana na utamaduni wake, uzoefu, ushiriki na vipaji.” (Laudato Si, 14).  

Kuupatanisha ulimwengu na Mungu mwenyewe ndiyo kusema kwamba, uumbaji wote unakuwa ufalme wa Mungu ambao hutambuliwa kimsingi na ufufuo wa Kristo na ambao utakuja katika utimilifu na utukufu wake na kuja kwa Kristo kwa mara ya pili. 

Baba Mtakatifu Fransisko anafundisha kwa kusema kwamba, ikiwa hatubadiliki kimitazamo na maisha yetu, suluhisho la shida yetu ya kiikolojia ya ulimwengu haitafika kabisa. 

Baba Mtakatifu Fransisko anatualika kufanya kile anachokiita ‘Uongofu wa Mazingira’; toba ya mazingira; upatanisho wa mazingira. 

Baba Mtakatifu Fransisko anatualika akisema kwamba, uongofu/upatanisho huu wa mazingira unatutaka tutambue wajibu tulio nao kwetu wenyewe, kwa jirani na kwa Muumba. 

Akielezea juu ya uhusiano wa mazingira na hali yetu ya ndani, Baba Mtakatifu Fransisko anaona kuwa: “Majangwa ya nje ulimwenguni yanaongezeka, kwa sababu majangwa ya ndani yamekuwa makubwa sana. Kwa sababu hii, mgogoro wa kiikolojia pia ni wito wa uongofu wa kina/mkubwa wa mambo ya ndani.” (Laudato Si, 217).  

Baba Mtakatifu Fransisko anatukumbusha kwamba  jambo hilo litawezekana iwapo tu tutaanza kwa kujitafiti dhamiri zetu na kurudi kwenye utambuzi wa uhusiano uliopo kati yetu na viumbe vingine. 

Kisha kujitafiti, tuungame na tuache tabia mbaya ya kutaka kutumia zaidi ya kile kilicho cha lazima na tunachokihitaji. 

Tunahitaji wongofu ambao utatufanya “Tuchunguze maisha yetu na kutambua njia ambazo tumeharibu uumbaji wa Mungu kupitia matendo yetu na kushindwa kwetu kutenda/kuchukua hatua. Tunahitaji uongofu, au mabadiliko ya moyo.” (Laudato Si, 218).  

Katika kuhimiza umuhimu wa mabadiliko ya moyo kama  njia ya upatanisho wa kiikolojia, Baba Mtakatifu Fransisko anaona pia nafasi ya elimu kwa jamii kwani Upatanisho na mazingira yetu hauna budi kuendana na elimu juu uharibifu  wa mazingira. 

“Elimu ya ikolojia inaweza kufanyika katika  mazingira mbalimbali: shuleni, kwenye familia, kwenye vyombo vya habari, kwenye katekesi na kwingineko. Elimu bora hupanda mbegu tangu tukiwa wadogo, na hizo huendelea kuzaa matunda maishani.” (Laudato Si, 213).

Ni sisi maaskofu wa Kanisa Katoliki wa Tanzania…