Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro (ACP) Samwel Kijanga, amehudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Chamwino, Wilaya ya Morogoro kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo viongozi wa dini, Diwani wa Kata ya Chamwino Mheshimiwa Faraji Suleiman, pamoja na wananchi wa kata hiyo.
Lengo kuu la mkutano huo ni kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo na kutoa elimu ya Polisi Jamii.Ambapo ACP Kijanga amesema kuwa, jukumu la Polisi Jamii ni kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kuzuia na kutanzua uhalifu katika maeneo yao.
Aidha, ACP Kijanga ameeleza namna ya kupata haki kupitia mfumo wa Haki Jinai, na kuwasisitiza wananchi kufuatilia kesi zao na kwenda kutoa ushahidi Mahakamani. Pia njia sahihi za kuzuia uhalifu ni pamoja na kuandaa daftari la wakazi, kutoa taarifa kwa wakati, na kuendeleza vikundi vya ulinzi shirikishi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chamwino, Mheshimiwa Faraji Suleiman, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kushiriki mkutano huo na kwa juhudi zake katika kutatua changamoto za wananchi.










