…………………………………………………………………………………………………..

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA), imepongeza maendeleo ya utekelezaji ujenzi mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa maji wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha jumla ya megawati 2,115 uliofikia asilimia 81.82 hadi kufikia Januari 31,2023.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi DAWASA, Jenerali Davis Mwamunyange wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa Julius Nyerere ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua zoezi la ujazaji maji bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.

“Mheshimiwa Rais alituagiza sisi DAWASA tunufaike kupitia maji ya mto Rufiji kwa kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani baada ya kuwa yamezalisha umeme” amesema Jenerali Mwamunyange.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amepongeza kazi nzuri iliyofanyika kwenye mradi huo na amefurahi ushirikiano mkubwa uliopo kati yao (DAWASA) na TANESCO.

Awali Mhandisi Mkazi Lutengano Mwandambo alieleza kuwa zoezi la ujazaji maji linaendelea vizuri na limefikia mita za ujazo 131.02 kutoka usawa wa bahari.

By Jamhuri