Rais mteule wa Nigeria Bola Tinubu ameapishwa leo kuwa kiongozi wa taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika linalokabiliwa na changamoto nyingi.

Anaingia rasmi madarakani huku raia wakiwa na matumaini mapya ya maisha bora na masuala mengine ambayo serikali yake inatarajiwa kuyaboresha.

Bola Tinubu, gavana wa zamani wa jiji la Lagos ambalo ni kitovu cha uchumi Nigeria amechukua nafasi ya  alliyekuwa Rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari. Ataiongoza nchi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa taifa la tatu kwa wingi wa watu itakapofika mwaka 2050. Tinubu mwenye miaka 71, ameahidi kuendeleza juhudi za Buhari za kuendeleza demokrasia katika nchi inayokabiliwa na mizozo mingi ya kiusalama, umasikini na njaa masuala ambayo yamekuwa yakiwakasirisha raia.

Tinubu alitangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa Februari 25 aliposhinda kwa kura milioni 8.8 na idadi ya kura zinazotakiwa kwenye theluthi mbili ya majimbo yote ya Nigeria.

Licha ya kuchaguliwa kwake kuendelea kupingwa mahakamani na vyama vya upinzani na miongoni mwa vijana walio wengi,  Licha ya kuchaguliwa kwake kuendelea kupingwa mahakamani na vyama vya upinzani na miongoni mwa vijana walio wengi, Tinubu ameahidi kuwaunganisha Wanigeria. Ilani yake ya “matumaini mapya” inatoa vipaumbele katika kutengeneza nafasi za kazi za kutosha na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwekezaji kwenye kilimo na miundo mbinu ya umma.

Vipaumbele vingine vinahusisha kutoa nafasi za kiuchumi kwa watu masikini pamoja na kuwa na kuwa na mfumo bora wa usalama wa taifa ili kukabiliana na changamoto zote za kiusalama. 

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema ahadi na matumaini yaliyotolewa na Tinubu yanakumbusha kile alichoahidi Buhari alipochaguliwa kuwa rais mwaka 2015. Vipaumbele vyake navyo vilijikita katika kupambana na vitisho vya usalama na kuukuza uchumi lakini  aliishia kushindwa kufikia matarajio ya walio wengi.

Kati ya waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Bola Tinubu ni mwakilishi maalumu wa Rais wa China Xi Jing Ping, ikiwa ni kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China

By Jamhuri