Bomoabomoa na kibwagizo cha ‘Hapa kazi tu’

bomoa-559x520Wakati majonzi, vilio na watu kupoteza fahamu kutokana na kubomolewa nyumba zao zilizojengwa bila kufuata utaratibu kwenye maeneo ya wazi na hifadhi ya barabara katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam huku kibwagizo cha ‘Hapa Kazi Tu,’ kikinogesha kazi hiyo, wananchi wameendelea kuhoji maana ya kibwagizo hicho.

Wiki iliyopita, nyumba zaidi ya 25 zimebomolewa yakiwamo makanisa mawili ya Anglikana na Tanzania Assemblies of God na nyumba ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania iliyoko katika eneo la Mivumoni, Kata ya Wazo.

Ubomoaji huo unasimamiwa na Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliokuwa na silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi.

Huku vilio vikiendelea kutawala, mke mwanajeshi huyo alizimia baada ya kupata mshtuko na kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu. Mwingine aliyezimia ni mmiliki mmoja wa nyumba iliyobomolewa katika eneo hilo hilo, aliyekuwa akichukua picha wakati nyumba yake ikivunjwa na ghafla alipata mshtuko.

Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya, ameeleza kwamba kazi hiyo ya ubomoaji nyumba hizo ilianza 12 asubuhi na kwamba katika eneo la Mbezi Beach baadhi ya watu wa Serikali walivamia eneo hilo na kujenga ofisi ya Serikali ya Mtaa huku wakijua kitendo hicho ni kinyume na utaratibu.

Kwenye utawala wa Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, maeneo mengi ya wazi yalikuwa yamevamiwa na kujengwa majengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya mafuta. Lakini waliotoa vibali vya ujenzi ni maofisa wa Ardhi wa majiji, manispaa na wilaya. Hakuna yeyote katika maofisa hao aliyepelewa mahakamani kwa kukiuka taratibu za kazi.

Bila aibu, hawa nao wanaibuka na kibwagizo cha Rais Magufuli ‘Hapa kazi tu’. Wako wapi maofisa Ardhi waliouza bustani ya Samora na kusisitiza kwamba inajengwa kisasa na kuweka bustani yenye mvuto zaidi, lakini mbinu yao kubwa ilikuwa kupora eneo hilo na kuweka biashara zao za migahawa? 

Wako wapi maofisa wa Manispaa ya Kinondoni waliouza barabara eneo la Mikocheni na kuruhusu shule kujengwa? Hawa nao bila haya wanasema ‘Hapa kazi tu.’ Kazi wanazozisifu ni zipi?

Vibaka wanapoiba mali za Watanzania wenzao, majambazi, miamba ya rushwa, uonevu na ubabe mwingine wa namna mbalimbali nao na ‘hapa kazi tu’, wapokeaji wa kaulimbiu wanakuwa na malengo tofauti kabisa.

Mwaka 1995 alipoingia madarakani Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, naye akaibuka na kaulimbiu ya ‘mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe’ na ‘kila mtu atakula kwa urefu wa kamba yake’ ambazo zilitumiwa na wahalifu kutekeleza uhalifu wao huku wakinukuu maneno hayo.

Wananchi walipata shida kwa kaulimbiu hizo ambazo zinatazamwa na Watanzania kwa nia na mawazo tofauti kabisa na waasisi wa kauli hizo.

Wao wanamaanisha wananchi waongeze bidii ya kuwajibika kwa lengo la kukuza maendeleo ya Taifa, lakini wanaotazama kwa namna tofauti wanaipeleka katika nia na matendo maovu. Kaulimbiu ya ‘Hapa kazi tu’ itumike kwa kuhamasishana kufanya kazi kwa bidii badala ya kuendekeza uvivu na vitendo vya kihalifu.

Hivi karibuni, wabunge wa vyama vya Upinzani chini ya mwavuli wa Ukawa walitimuliwa bungeni na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya kufanya fujo walipokuwa wanapinga Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuingia bungeni kama Rais wakati muda wake wa kuwa madarakani umekwisha.

Wabunge wa Upinzani waliwasilisha ujumbe wao huo wa kila mpenda haki duniani kwamba Dk. Shein hakuwa na uhalali kisheria wa kuhudhuria uzinduzi wa Bunge la 11 kwa kofia ya rais, huku akiongeza hasira zilizotokana na uporaji wa haki za Wazanzibari katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Ndugai aliwaamuru watoke nje ya Ukumbi wa Bunge uliokuwa na askari wa uraiani walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo kinyume na taratibu za mabunge duniani. Ubabe huo nao uliambatana na kibwagizo cha ‘Hapa kazi tu’, ambacho kinatafsiri nyingi ambazo zinatofautiana vichwani mwa Watanzania.

Nachelea kusema kuwa kwenye Bunge la 11 bila shaka hoja nzito zenye kugusa maslahi ya Taifa zitapitishwa ama kukwamishwa kibabe, na pengine kwa mabomu ya machozi kama baadhi ya wabunge walivyoingia madarakani kwa kusaidiwa na ubabe wa polisi.