Seif_hamad(17)Ili kudhihirisha kuwa Zanzibar kuna tofauti za kiitikadi za kihistoria na hasa kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba hapa kuna mifano ya matokeo ya chaguzo zilizofanyika Zanzibar tangu 1957 mpaka 2010.

Katika uchaguzi wa kwanza 1957 ASP walipata viti 5 kati ya viti 6 na Muslim Association kiti kimoja (Stone Town). Uchaguzi wa kwanza wa Januari 1961 ASP viti 10, ZNP viti 9, ZPPP viti 9, marudio ya uchaguzi wa Juni, 1961 ASP viti 10, ZNP (HIZBU) viti 10 na ZPPP viti 3. Uchaguzi wa 1963 ASP 13, ZPPP VITI 6 na HIZBU 6. 

Ndipo yakatokea yale MAPINDUZI matukufu ya Januari 12, 1964 kumaliza dosari za matabaka. Hayati Mzee Abeid Karume aliwahi kutamka kwamba kule Visiwani hakutakuwa na uchaguzi ng’o!

Likatolewa tamko yaani “Decree” kuondoa mambo ya uchaguzi visiwani. Hili liliwastusha sana mabepari na watawala kule visiwani (waarabu) wakaamua kutimkia nje ya nchi na kurudi kwenye nchi za asili yao Uarabuni mara moja.

Ukaja Muungano wetu kati ya nchi mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika – tukawa TANZANIA. Hapo sasa Wazanzibari wakaona mikikimikiki ya mapinduzi itakoma na huko tuendako Muungano utaleta demokrasia ya uchaguzi. 

Baada ya miaka kadhaa ya huo muungano Zanzibar wakaamua kupanua utawala wa demokrasia. Joto lile la Mapinduzi pamoja na mikimikiki yake sasa lilipungua, watu wakaanza kupumua na kutafuta utawala wa kidemokrasia.

Kuanzia utawala wa Mzee Abdul Jumbe Mwinyi 1972 mawazo ya kurekebisha Katiba ya Visiwani yalijitokeza miongoni mwa wasomi na wakaazi wa Zanzibar. Basi Mzee Jumbe (ex – Makererian) na Mzee Nyerere (ex – Makererian) walikubalina kujenga hali ya maelewano kati ya makundi ya Wazanzibari.

Lakini mzee Jumbe, labda kwa msukumo wa wasomi na mabepari wa kule visiwani, alianza kuwa na mawazo ya autonomy kwa kule visiwani. Walitaka wawe na wimbo wao wa Taifa na Bendera na Nembo ya Taifa lao ili mradi pawepo na utambulisho (IDENTITY) wa aina yake kule ya visiwani.

Hilo la kutaka utambulisho lilizusha wazo la kumpata na kumtumia Mwanasheria asiyekuwa Mtanzania. SMZ iliajiri Mwanasheria kutoka nchi ya Ghana (Mr. Swansea) kuja kuandaa mchakato namna ya kupata hiyo Autonomy kutoka Muungano ili Visiwa vile viwe na Uhuru zaidi. 

Zanzibar ikatunga Katiba yake ile ya 1984, kilichofuatia ni andiko maalum la kupeleka The Hague kudai hiyo autonomy. Ilipofikia hatua ile ndipo tukasikia HALI YA HEWA IMECHAFUKA, VISIWANI. Mengi sasa yaliparaganyika. Rais wa Zanzibar Mzee Jumbe alijiuzulu. Baadaye baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM waliondolewa na mambo yakaleta mvurugiko mkubwa kiutawala. Kutokuaminiana sasa kukawa kati ya SMZ na Serikali ya Muungano. 

Baada ya Mzee Jumbe kujiuzulu mwaka 1984 ukaja utawala wa Mzee Mwinyi. Baada ya huyo ukaja utawala wa Sheikh Idrissa Abdul Wakili, ukaja utawala wa Salmin Amour almaarufu “Komandoo”; ukaja utawala wa Karume Junior. Watawala wote hawa ni Marais kutoka Unguja. Wa-pemba wakaanza kuguna. Vipi kwani Pemba hawezi kutokea Rais? Wazo la kutokuaminiana tena wenyewe kwa wenyewe likazuka wakati huu kati ya Unguja na Pemba ambavyo ni visiwa vikubwa viwili kwa pamoja ndiyo tunapata nchi ya Zanzibar.

Muda wote huo makundi ya kule Visiwani bado yakingali kama zamani. Likaja sasa wazo la hasa nani ni Mzanzibari? Hapo harakati zikafanyika kupata tafsiri halisi ya Mzanzibari na sifa zake zikaainishwa. Ilibidi watu wote wajiandikishe wapate vitambulisho maalum vya “Mzanzibari mkazi”. Hili lingesaidia wajijue wako wangapi ili wakati wa uchaguzi kusiwe na wageni kutoka bara kuongeza hesabu. Wakaanza kudai Uzanzibari kama kitambulisho (identity) cha mkazi wa visiwani. 

Mwalimu Julius Nyerere akawa anajiuliza kwa nini litolewe dai namna hii? Basi mwaka 1995 Mwalimu alitoa matamko haya “Huku kuzungumza UZANZIBARI si fahari. Hatima yake tunavunja nchi. Huwezi kukuza UZANZIBARI kwa kujiita. “Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika”. Nje ya Muungano huwezi kusema hivyo. Kuna wao Wapemba sisi Waunguja (Nyufa uk. 10).

Mimi nimechambua kwa kifupi kutoa mwanga kidogo juu ya siasa za visiwani kule bado wana mtazamo wa makundi. Bado hawaaminiani asilani. Ndiyo sababu tangu uchaguzi wa vyama vingi kule Visiwani ufanyike haujapokelewa bila malalamishi. Mara kuna kura za maruhani kule Pemba, mara kuna wizi wa kura ili mradi matokeo ya uchaguzi yasikubalike na pande zote.

Hatimaye baada ya ule uchaguzi wa mwaka 2010 Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharrif Hamad wakafikia muafaka wa kuwa na Serikali ya UMOJA WA KITAIFA. Vyama vyote vikuu vya siasa vishirikiane kujenga nchi na Taifa la Zanzibar. 

Kale kadukuduku ka kwanini Marais wote watoke Unguja tu kalikuwepo bado mioyoni mwa wa Pemba. Basi kuondoa hilo CCM ikateua Mpemba kuwa Rais wa SMZ ndiye Mzee Shein. Ukaja Uchaguzi wa 2010 CCM ikaweka Mpemba na CUF kaweka Mpemba pia. Sisi wengine tukadhani sasa njia nyepesi kwa CCM kule Pemba kupata kura zote. Wapi bwana! Ngangari wakabaki ni upemba tu.

Matokeo haya yanaonyesha mgawanyiko wa kura kati ya Unguja na Pemba. Maana wakati CCM ikishinda viti vingi Unguja ngome ya CUF ni Pemba. 

Tangu enzi za ZNP na AFRO SHIRAZI kulijitokeza sehemu maalum za waarabu na sehemu maalum za watu weusi. Mathalani Unguja inajulikana kiti cha Stone Town ni cha HIZBU wakati kule Pemba kiti cha Wingwi na Mkoani vilikuwa vya ASP. Hali namna hiyo inajitokeza hata leo. Pemba wangali HIZBU wakati Unguja wangali ASP. Kwa “mentality” namna hii makundi hayaishi visiwani. Picha inayojitokeza tangu uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1957 ni hii. Kwamba Chama kinachoshinda Unguja sio Chama kile kile kinachoshinda Pemba. Wakati ASP inashinda viti vya Unguja, ZNP (HIZBU) inashinda viti vya Pemba. Uwiano huu sasa umehamia kwa CCM kuwa na viti vya Unguja na CUF kuwa na viti vya Pemba, mfano katika Uchaguzi wa 1995 CCM viti 26 na CUF 24; uchaguzi wa 2000 CCM 34 na CUF 16, na uchaguzi wa 2005 CCM 30 na CUF 19, mpaka ule uchaguzi wa 2010 CCM 28 na CUF 22. 

Kuhusu uchaguzi wa Rais wa Zanzibar 1995 CCM walipata 50.2% na CUF 49.8%; 2000 CCM 50.1% na CUF 49.1%; 2005 CCM 50.1% na CUF 49.1%; 2005 CCM 53.2% na CUF 46.1%; 2010 CCM 50.1% na CUF 49.1%.

Fikra na mila za huko visiwani siyo rahisi mazonge mazonge ya chaguzi za huko kutatuliwa na mtu asiyekuwa Mzanzibari. Uchaguzi wa mwaka 2000 ulisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na wengine kukimbilia Kenya kama wakimbizi.

Na wala haifai kudhani kuwa matukio ya vurugu baada ya uchaguzi Zanzibar ni matukio yaliyoanza kufuatia uchaguzi wa mwaka 2000 tu. Vurugu zilitokea pia mwaka 1961 baada ya kurudia uchaguzi. Watu wapatao 67 walipoteza maisha kutokanas na marudio ya Uchaguzi wa Januari uliorudiwa Juni 1961. 

Basi ni hali ya kipekee kwa siasa za huko Visiwani. Wanazozana, wanapatana, lakini hawafarakani. Mathalani kuna malumbano makali kati ya Wapemba na Wamakunduchi, lakini hawafarakani. 

Hivi sasa viongozi wakuu wa CUF na CCM huko Visiwani wana asili moja ya upemba. Hapo sioni kwa nini hii “common denominator” yao isirahisishe maelewano. Zile fikra za Hizbu na ASP zisipewe nafasi kwa vijana wa leo maana wao ya nyuma (uhasama kati ya Waarabu wa HIZBU na Waafrika wa ASP) hawayajui na wala wasihusishwe.

Wazanzibari wote wamuweke Mungu mbele kisha uzanzibari wao uwaunganishe. Kwa hawa wawili wachombezee na upemba wao. Hapo pana ukorofi kweli wa tofauti za kusambaratisha umoja wao? Dhana ya Serikali ya umoja inaelekeza kwenye mshikamano. Mimi sintofahamu kwa nini Maalim Seif na Dk. Shein wasifarijiane kwa upemba wao waache mambo ya itikadi ya vyama. 

Nimeambiwa na baadhi ya rafiki zangu huko Visiwani, tofauti hizi za itikadi eti zimeingia mpaka katika ndoa. Mume na mke eti wako radhi kutalikiana kama hawana itikadi ya chama kimoja.

Nasikia wanaambiana, ukienda kupigia kura chama chako basi hapo ni talaka tu! Loh! Kama ni kweli hali imefikia pabaya namna hiyo, basi siasa za Visiwani kamwe watu wa nje hawataweza kusuluhisha. 

Nasema wote Maalim Seifu na Dk. Shein wamepanda ngalawa moja itokayo Nungwi kuelekea Mkoani, asitokee wa kupiga kafia la kuizungusha hiyo ngalawa. Tumuombe Mungu, awajalie viongozi wetu wayaenzi Mapinduzi yale matukufu ya Januari 12, 1964 – Mapinduzi daima. Wasihamaki kwa Uchaguzi uliopita. Watulize mioyo yao watafakari UMOJA WAO na UZANZIBARI wao kwanza.

Wazanzibari waiweke Zanzibar mbele na vyama viwe nyuma yao. Zanzibar kwanza na itikadi na vyama baadaye. Msingi wa Mapinduzi ya 1964 ulikuwa ni kuondoa dhuluma, ubaguzi na kuleta haki na usawa miongoni mwa wazanzibari wote. Kwa kuzingatia misingi hii, Zanzibar itajengwa na Wazanzibari. 

Mungu ibariki Tanzania 

Wabariki viongozi wake watumie hekima na busara zao kudumisha Amani na umoja wa Taifa letu. 

Amina. 

2282 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!