Bomu la watu laja Afrika – 3

Balile

Na Deodatus Balile

Kwa wiki ya tatu sasa nafanya mapitio ya kitabu kiitwacho “Making Africa Work”. Tafsiri isiyo rasmi jina la kitabu hiki linamanisha “Mbinu za Afrika kujikwamua kiuchumi.” Kitabu hiki kimeandikwa na Greg Mills, Olusegun Obasanjo (Rais mstaafu wa Nigeria), Jeffrey Herbst na Dickie Davis. Kimechapishwa na Taasisi ya Brenthurst Foundation ya Johannesburg, Afrika Kusini. Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ameshiriki uzinduzi wa kitabu hiki katika Hoteli ya New Africa, jijini Dar es Salaam. Nilikuwapo.

Katika sehemu ya kwanza ya mapitio ya kitabu hiki, niliandika kwa kina juu ya ongezeko la watu duniani. Nimeeleza kinachotajwa katika kitabu hiki kwamba Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu milioni 58. Kufikia mwaka 2050 Tanzania itakuwa na watu milioni 138.

Afika ina watu bilioni 1.2 kwa sasa. Kufikia mwaka 2050 itakuwa na watu bilioni 2.4 na mwaka 2100 Afrika itakuwa na watu bilioni 5.7. Dunia wakati huo itakuwa na watu bilioni 11, hivyo nusu ya watu duniani watakuwa wanaishi Afrika.

Takwimu hizo tukiziangalia kwa kina kwa mujibu wa UNICEF Tanzania kwa sasa ina watoto milioni 24, na kufikia mwaka 2050 nchi inakadiriwa kuwa itakuwa na watoto milioni 48. Hakika tunahitaji maandalizi makubwa kama nchi. Ingawa uchumi wa Tanzania inakua kwa asilimia 7 kwa mwaka, idadi hii ya watu itaumeza. Tunapaswa kupigana kukuza uchumi kwa asilimia zaidi ya 10 kwa mwaka. Hii itatuwezesha kujenga shule, hospitali, makazi, miundombinu ya usafirishaji na masuala mengine muhimu kwa mahitaji ya binadamu.

Sitanii, hakuna nchi iliyopata kuendelea duniani bila kuwa na viwanda. Kwa idadi hii ya ongezeko la watu Tanzania, hatuna namna ila kuwekeza katika viwanda kwa maana ya kuzalisha ajira, kuzalisha bidhaa tutakazouza nje ya nchi na kupata fedha za kigeni zitakazoongeza amana ya Serikali na hivyo kuipa uwezo wa kuhudumia watu wake. Sasa nadhani hili la idadi ya watu limeeleweka na tunafahamu kwa nini inatupasa kujiandaa.

Katika kufikia adhima hii ya kuendeleza watu wetu na kuepuka aibu kubwa mbele ya safari ya watu wetu kushindwa kupata huduma za msingi ifikapo mwaka 2050 na hivyo kuzalisha bomu la vijana wahuni, wezi, majambazi na wavuta bangi, tunapaswa kujiandaa sasa. Nitataja maeneo tunayopaswa kujielekeza katika uwekezaji, ila kwa ufupi ni pamoja na kilimo cha muhogo, miwa, korosho, kahawa, katani na pamba. Mazao haya yana nafasi kubwa ya kukuza sekta za viwanda nchini na yanatoa ajira nyingi kwa wakati mmoja.

Akina Obasanjo katika kitabu hiki, wanazitaka serikali na sekta binafsi kuandaa makazi bora kwa maana ya miji iliyopangiliwa na kuwa na miundombinu ikiwamo barabara, reli, umeme, maji na viwanja vya ndege kurahisisha usafiri na usafirishaji. Pia, wanagusia demokrasia. Magwiji hawa wanasema imethibitika pasi shaka, kuwa nchi zenye demokrasia zimepata maendeleo kwa kasi kubwa. Hii inatokana na kwamba kila mtu anajisikia yuko huru na anashiriki kazi za maendeleo bila kinyongo wala hujuma.

Sitanii, magwiji hawa wanazungumzia kwa kina kilimo. Wanazisihi Serikali za Afrika kuwezesha watu wake kufanya kilimo. Hii itakuwa na tija kwa maana ya kuwapo chakula cha uhakika, lakini pia watu watapata fedha kwa kuuza mazao wanayozalisha. Wanazitaka serikali kujiepusha na utaratibu wa kupanga bei za mazao, na wanazitaka ziwe na maghala (vihenge) kwa ajili ya kuhifadhia chakula cha kutosha watu wao na hivyo kuepusha dhana kwamba wakulima wakiruhusiwa kuuza mazao yao wanakotaka watauza kila kitu na nchi kubaki bila chakula.

Sera za Serikali zinapaswa kukumbatia mbinu za kisasa za kilimo ikiwamo kutumia mashine badala ya jembe la mkono, kuhamasisha uzalishaji mkubwa na teknolojia itakayoongeza mavuno. Hii itawapa faida wakulima. Nchini Marekani na Uingereza, idadi ya wakulima imeshuka kutoka asilimia 90 miaka ya 1900 hadi asilimia 2 (mbili) mwaka huu. Wengi waliokuwa wakulima wamepata mitaji na wameanzisha viwanda. Hili linawezekana hata hapa Tanzania.

Wanapendekeza kuwapo kwa hati miliki za muda mrefu zitakazoongeza imani ya wawekezaji na benki zinazokopesha. Pia wanapendekeza Serikali kuwekeza katika miundombinu inayoelekea mashambani kwa nia ya kurahisisha usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara. Wiki ijayo, nitapitia sura ya nne ya kitabu hiki, na mapendekezo ya wataalam hawa katika eneo la madini. Yote wanayosema katika kitabu hiki, hakika yanaweza kuliondoa taifa letu katika lindi la umaskini. Usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.