Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limefanikiwa kuwaua wahalifu sita maarufu kama ‘Panya Road’ waliokuwa wakielekea eneo la Goba kufanya uhalifu jana.

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalum, Jumanne Muliro amesema hayo leo 18,2022, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema baada ya taarifa za siri kutoka kwa wasamaria wema,walifanya jitihada za msako kuwakamata wakiwa kwenye gari aina ya Noah iliyokuwa ikitoka Mabibo kuelekea Goba kwa nia ya kwenda kufanya uhalifu.

Kamanda Muliro amesema kuwa waliweka mtego barabarani katika eneo la Makongo na kufanikiwa kuwakamata katika eneo la Makongo Area 4 ya saa nne asubuhi ambapo ndani ya gari hilo kulikuwa na watuhumiwa tisa.

Ameongeza kuwa watuhumiwa hao walikuwa na silaha mbalimbali za jadi na baada ya Polisi kutoa tahadhari ya kuwataka kushuka kwenye gari watuhumiwa walishuka wakiwa na mapanga,visu na mawe.

“Baada ya kugundua kuwa kuna mtego tulitoa tahadhari ya kuwataka kushuka kwenye gari lakini walishuka wakiwa na silaha za jadi kwa lengo la kutuogopesha ili wakimbie.

“Askari waliwatahadharisha na ndipo walipoamua kupiga risasi juu ili wasikimbie lakini bado baadhi yao walikuwa wakifanya jitihada za kutaka kukimbia.

“Katika purukushani hizo watuhumiwa sita walijeruhiwa vibaya kwa risasi na kukimbizwa hospitali lakini walifariki njiani na pia watatu walifanikiwa kutoroka na jitihada za kuwatafuta zinaendelea,” amesema kamanda.

Kamanda Muliro amesema baada ya purukushani hizo walikagua gari hilo na kukuta mapanga tisa na kisu kimoja na dhana za kuvunjia nyumba katika matukio mbalimbali.

Aidha, Kamanda Jumanne Muliro amewataja waliopoteza maisha kuwa, Salum Juma maarufu kwa jina la Babu Salum umri kati ya miaka (20-27), mkazi wa Mbagala, Khalifa Khalifa mkazi wa Buguruni ambaye naye inaonesha aliwahi kukamatwa kwa makosa ya uhalifu wa kutumia mapanga Dar es Salaam.

Pia amebainisha katika upelelezi wa awali wamebaini kuwa, vinara hao walishiriki kwenye tukio la Kawe na eneo la Buguruni kwa kuiba na kuua.

Kamanda amesema, Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza kwa haraka agizo lililotolewa na Mkuu wa Jeshi hilo la kuwashughulikia wahalifu nchini.

“….Jeshi linawapongeza wananchi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa watu wanaopanga ama kutekeleza vitendo vya uhalifu.

Jeshi la Polisi linaendelea kuwatahadharisha wananchi kuacha mara moja kujihusisha kwenye uhalifu na linaendelea na msako mkali wa kuwabaini wote wanaojihusisha na uhalifu.

By Jamhuri