Na Deodatus Balile, Morogoro

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umetoa taarifa muhimu kwa maendeleo ya biashara nchini katika mkutano na Jukwaa la Wahariri Tanzania. 

Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa, ameeleza mfumo wa kusajili biashara kupitia mtandaoni (ORS) ambao umeondoa kero ya watu kulazimika kusafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini kwenda Dar es Salaam kukata leseni.

Brela katika mkutano huo imeeleza kuhusu mfumo wa uendeshaji wa kampuni na kuwasihi Watanzania kufahamu taratibu za kupeana hisa na jinsi ya kumiliki hisa. Miaka ya nyuma, wapo Watanzania ambao wamekuwa wakitoa hisa kwa watoto wao, madereva, watumishi wa ofisi zao, wake au waume zao kwa matumaini kuwa watawashikia kwa muda, ni kosa kubwa, hali inayoleta migogoro.

Ukiacha migogoro ya hisa, kuna eneo ambalo binafsi naona nilijadili kidogo. Mei 11, 2022 wakati Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, ameitaka wizara yake kushauriana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuona jinsi nchi inavyoweza kuunganisha mfumo wa leseni ikawa leseni zote zinatolewa na Brela.

Brela kwa sasa inatoa leseni daraja la A, na daraja la B zinatolewa na maafisa biashara wa halmashauri za wilaya nchini. Kwa leseni za daraja la A, waombaji wanaomba na kupata leseni kupitia mtandaoni, ilhali leseni za daraja la B zinazotolewa na halmashauri, waombaji wanapaswa kujaza fomu na kusubiri kwa muda madiwani wazipitishe kwenye vikao vya madiwani.

Sitanii, leo naomba nijikite kwenye eneo la leseni. Mwaka jana kuna halmashauri kadhaa nchini ziliwekwa katika mfumo wa majaribio kutoa leseni kwa njia ya mtandao. Mpango huu ulikwama. Tulikwenda kuomba leseni, ikawa tunaambiwa mtandao uko chini, tukatakiwa kufungua barua pepe za dharura, tulijaribu kila jambo, lakini hatukufanikiwa.

Hatimaye, halmashauri zote zilitoa maelezo kuwa haziwezi kutumia mfumo huu wa leseni wa Brela kwani zina madeni mengi ya miaka ya nyuma, hivyo kutumia mfumo huu wangepoteza madeni. Binafsi nakubaliana na Waziri Bashungwa kuwa muda umefika leseni zote zitolewe na Brela. Kwa sasa nchi yetu ina utitiri wa leseni na mamlaka za kutoa leseni.

Ni rahisi taasisi zote zinazotoa leseni mbalimbali kuunganishwa na mfumo wa Brela. Kwa kuanzia nasema tuunganishe kwanza halmashauri zote nchini na kutoa leseni katika kituo kimoja. Zipo faida za kutoa leseni kwenye mfumo wa Brela. La kwanza, leseni hizi zitakuwa za kielektroniki. Kutaondoa usumbufu wa watu kusafiri kwenda makao makuu ya wilaya kuomba leseni.

Si hayo tu, kuna hatari kubwa katika mfumo wa sasa wa leseni. Kuna maeneo mbalimbali nchini ambapo watu wanazo leseni wanazodhani ni halali kumbe ni feki. Katika wilaya maafisa biashara wengi wanatengeneza utajiri kwa kuchapisha vitabu vya leseni na kuziuza kwa wafanyabiashara. Wanaziuza kutokana na ukweli kwamba mfumo uliopo sasa wa kupata vitabu vya leseni unatia shaka.

Ilivyo, Brela wanatoa vitabu vya leseni za daraja B kwa kila halmashauri ya wilaya, na baada ya hapo, halmashauri za wilaya zinatoa leseni kwa wafanyabiashara na kurejesha taarifa ya leseni walizotoa Brela. Hawarejeshi pesa, bali taarifa ya idadi ya leseni walizotoa.

Hapa ndipo ulipolala mchezo. Maafisa biashara wanachapisha vitabu vyao, kisha wanavitumia kutoa leseni. Nafahamu baadhi ya halmashauri ambazo mara kadhaa wamekagua na kukutana na leseni feki, ila kila mfanyabiashara wanayemuuliza anatoa ushahidi kuwa amepewa kwenye halmashauri.

Sitanii, namfahamu mkurugenzi mmoja ambaye nusura apigane na afisa biashara wa halmashauri yake baada ya kujiridhisha kuwa mchezo wa leseni feki unaanzia ofisini kwake. Kimsingi kwa kuangalia kiwango cha usumbufu wanaopata wafanyabiashara, nadhani wakati umefika ambapo tunatakiwa kama nchi kukumbatia teknolojia ya elektroniki. Nasema mifumo ya leseni ya daraja la A na B iunganishwe na leseni zote zitolewe na Brela.

By Jamhuri