Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Kamishna Uhifadhi (TANAPA), William Mwakilema ameagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Burigi -Chato kuboresha huduma za utalii pamoja na kuongeza juhudi za kujitangaza ili kufikia uwezo wa kujiendesha na kuchangia pato la Taifa.

Kamishna Mwakilema ameyasema hayo alipotembelea Hifadhi ya Taifa Burigi jana kwa lengo kukagua shughuli za uhifadhi na utalii katika Hifadhi hiyo.

“Boresheni bidhaa za utalii na shughuli mbalimbali za utalii na kuzitangaza zaidi ili kuchangia zaidi pato la Taifa” amesema Mwakilema.

Mwakilema ameisitiza adhma ya Serikali ya kufikia watalii millioni tano na mapato dolla za kimarekani billioni sita ifikapo 2025 na kubainisha lengo hili litatimia kwa hifadhi zote kuongeza jitihada za kujitangaza, kuongeza mazao mapya ya utalii pamoja na kuimarisha miundombinu yote hifadhini.

Kamishna Mwakilema pia ameelekeza hifadhi hiyo kuimarisha ulinzi kwa kuongeza ushirikiano na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama nchini.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato Mkuu wa Hifadhi hiyo Kamishna Msaidizi wa uhifadhi, John Nyamhanga

Amesema Hifadhi ya Taifa Burigi -Chato ni moja kati ya hifadhi mpya zinazoendelea kukua na tayari mikakati mbalimbali imeshawekwa kuhakikisha inaongeza bidhaa za utalii ili kuvutia wageni wengi zaidi kuitembelea.

Pia, Hifadhi imejipanga kuendelea kujitangaza katika nchi jirani kama Uganda, Burundi na Rwanda.

By Jamhuri