Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wataalamu wa afya kutoka nchini Burundi wametembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuona namna ya kushirikiana katika matibabu ya moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI sasa inavutia nchi nyingi kutaka kujifunza kutokana na uwekezaji wa kisasa uliofanywa na Serikali.

Dkt. Kisenge alisema nchini nyingi za Afrika zikitaka kuanzisha Hospitali za moyo zimekuwa zikifanya ziara katika taasisi hiyo kujifunza na kupata uzoefu ili nazo ziweze kufanikiwa.

“Wataalamu hawa kutoka Burundi wamekuja hapa kujionea nini tunafanya lakini pia kuweka mahusiano nasi ili waanze kuwaleta wagonjwa kutoka Burundi kuja kutibiwa JKCI. Tumekuwa tukitembelewa na wataalamu kutoka nchi tofauti kujifunza ikiwemo Somalia, Sierra Leon, Kenya na Burundi”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema dhana ya tiba utalii katika taasisi hiyo imeongezeka kwa kasi kwani kwa kipindi cha miezi mitatu wameweza kuona wagonjwa kutoka nje ya nchi zaidi ya 365.

“Tumekuwa na wigo mkubwa wa kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo hivyo kupelekea kupata idadi kubwa ya wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, lakini pia kutembelewa na wataalamu wa afya kutoka nje ya nchi ili waweze kujifunza hapa kwetu”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema kupitia wagonjwa wanaotoka nje ya nchi uchumi wa nchi na wamtu mmoja mmoja unaongezeka kwani wanapokuwa hapa nchini wanajihusisha na shughuli tofauti zikiwemo za malazi, utalii na zinginezo.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Burundi Constantin Nyamuzangula alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo la matibabu ya magonjwa ya moyo.

Dkt. Constantin alisema kupitia ziara hiyo wamejifunza kuwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inafanya upasuaji wa moyo wa aina karibuni zote, kwani nchini Burundi bado hawajaanza kufanya upasuaji wa moyo wa aina nyingi.

“Tumetembelea maeneo mbalimbali ya taasisi hii, wanaona wagonjwa wengi sana mazingira ya hospitali pia ni mazuri mtu akiwa hapa ni kama yupo eneo linalojihusisha na mambo mengine na si hospitali”, alisema Constantin

Dkt. Constantin alisema kwa sasa Burundi inapeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nchini Ufaransa, Beljium, Kenya na India lakini baada ya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wanaenda kuangalia namna ya kuwaleta wagonjwa kutoka Burundi kuja kutibiwa nchini kwani gharama za matibabu kwa Tanzania zipo chini tofauti na nchi nyingine.

Naye Mkuu wa Hospitali ya Shifaa iliyopo nchini Burundi Dkt. Ndikumana Sudi alisema ujio wao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete umewapa nafasi ya kujifunza mengi kutokana na huduma zinavyotolewa kupitia mifumo ya kisasa kwani kwao yapo mengi bado hawajafikia.

Dkt. Ndikumana ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya sukari alisema wakati wa ziara yao wameweza kutembelea wodi za wagonjwa na kuongea na wagonjwa ambao wameonesha imani kubwa na taasisi hiyo kutokana na huduma wanazozipata.

“Sisi kwetu hatuna mtambo wa cathlab unaotoa huduma za upasuaji wa tundu dogo, lakini pia tumeona hapa wagonjwa wa ICU kila mgonjwa ana muuguzi wake hii inachangia katika kutoa matibabu bora”, alisema Dkt. Ndikumana.

Daktari bingwa wa moyo Constantin Nyamuzangula na Daktari bingwa wa sukari Ndikumana Sudi kutoka nchini Burundi wakiangalia huduma zinazotolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembelea taasisi hiyo leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Lugendo akiwaelezea huduma zinazotolewa katika wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo Daktari bingwa wa moyo Constantin Nyamuzangula na Daktari bingwa wa sukari Ndikumana Sudi kutoka nchini Burundi walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayefanya kazi chumba cha uangalizi maalumu cha watoto (ICU) Jackline Siane akiwaelezea namna wanavyowahudumia watoto Daktari bingwa wa moyo Constantin Nyamuzangula na Daktari bingwa wa sukari Ndikumana Sudi kutoka nchini Burundi walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.

Afisa Uuguzi na mkufunzi wa mafunzo ya huduma za dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joshua Ogutu akiwaelezea mafunzo yanayotolewa na JKCI Daktari bingwa wa moyo Constantin Nyamuzangula na Daktari bingwa wa sukari Ndikumana Sudi kutoka nchini Burundi walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa

By Jamhuri