“Jengo hili litakuwa na ofisi za kudumu za Taasisi ya Mwalimu Nyerere, maktaba ya taasisi itakayotoa fursa kwa Watanzania na watu wengine wote kusoma maandiko na nyaraka mbalimbali alizoandika Mwalimu Nyerere, pamoja na shughuli za uwekezaji za wabia, hususan hoteli ya ngazi ya kimataifa.”

Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Juni 26, mwaka huu inatimiza miaka 23 tangu kuanzishwa kwake.

Taasisi hiyo ilianzishwa rasmi Juni 26, 1996 ikiwa ni kumbukumbu ya kudumu ya Mwalimu Julius Nyerere, misingi aliyoiamini na kuitekeleza, na kazi alizofanya wakati wa uhai wake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Joseph Butiku, amesema kwa kuwa taasisi hiyo inatimiza miaka 23 katika wakati ambao pia taifa litafanya kumbukizi ya miaka 20 baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, shughuli mbili kubwa zitafanywa na taasisi hiyo.

Alizitaja shughuli hizo zitakazofanyika katika kipindi cha kati ya Juni 14 (wiki iliyopita) hadi Oktoba 14, 2019, kupitia taasisi hiyo kuwa ni uzinduzi wa jengo jipya la kitega uchumi la taasisi hiyo na shughuli ya pili ni kuendesha kongamano la kimataifa kuhusu baadhi ya kazi alizosimamia Mwalimu Nyerere nchini, Afrika na duniani.

“Agosti 2019, taasisi inatarajia kuzindua jengo lake jipya la kitega uchumi lililoko katika makutano ya barabara za Morogoro/Mansfield/Zanaki na Sokoine. Jengo hili, The Mwalimu Nyerere Foundation Square Building limejengwa kwa mkopo. Kampuni ya CRJE East Africa Limited, kampuni tanzu ya Serikali ya China ndiyo mjenzi na mkopaji, Shirika la Fedha la Benki ya Dunia na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

“Jengo hili litakuwa na ofisi za kudumu za Taasisi ya Mwalimu Nyerere, maktaba ya taasisi itakayotoa fursa kwa Watanzania na watu wengine wote kusoma maandiko na nyaraka mbalimbali alizoandika Mwalimu Nyerere, pamoja na shughuli za uwekezaji za wabia, hususan hoteli ya ngazi ya kimataifa. Taasisi iko katika maandalizi ya kuzindua Chuo cha Mafunzo ya Uongozi kitakachofahamika kama The Mwalimu Nyerere Foundation Leadership and Management Institute,”  amesema Butiku na kuongeza: “Shughuli ya pili itakuwa kongamano la kimataifa kuhusu baadhi ya kazi alizosimamia Mwalimu Nyerere nchini Tanzania, Afrika na duniani.”

Chimbuko la Nyerere Foundation

Katika kuzungumzia chimbuko la Taasisi ya Mwalimu Nyerere, maarufu kwa jina la Nyerere Foundation, Butiku amewakumbusha Watanzania kwamba, taasisi hiyo ni huru ya kiraia isiyokuwa na uhusiano wowote wa kiitikadi na serikali, wala vyama vya siasa, ikiendesha shughuli zake katika jamii, ndani na nje ya Tanzania katika maeneo matatu makubwa.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kudumisha, kuimarisha, kutetea na kupigania kwanza: amani; pili: umoja na tatu: maendeleo ya tija kwa watu wote, na kwamba maeneo hayo ndiyo malengo makuu ya taasisi hiyo.

“Mwezi Juni kila mwaka umekuwa na umuhimu mkubwa kwa taasisi. Taasisi hii iliandikishwa na kuanzishwa rasmi Juni 26, 1996, muda mfupi baada ya Mwalimu Nyerere kuongoza wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kutia saini zao katika katiba yake (trust deed) Juni 14, 1996. Kwa hiyo ilipofika Juni 14 taasisi hii ilitimiza miaka 23 tangu Mwalimu Nyerere alipokubali ianzishwe na kutumia jina lake,” amesema Butiku.

Butiku ambaye katika mkutano wake huo na waandishi wa habari aliongozana na watendaji kadhaa wa taasisi hiyo, wakiwamo wakuu wa idara za taasisi, amesema wakati wa uhai wake na katika kikao chake cha kwanza cha Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Nyerere akiwa mwenyekiti alishauri taasisi ianzishe mjadala wa kitaifa kuhusu maendeleo.

“Mjadala huu unaendelea hadi hivi leo. Pia akitumia taasisi yake, Mwalimu alisimamia usuluhishi wa mgogoro Burundi, pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya nchi za Kusini ambayo ilichambua matatizo ya umaskini na maendeleo duni yanayozikumbuka nchi nyingi zinazoendelea, uhusiano baina yao na mataifa ya kaskazini, na jinsi ya kuyatatua,” amesema Butiku.

Akifafanua zaidi kuhusu hilo akasema: “Tume ilitoa ripoti ya changamoto za nchi za kusini ambayo inatoa mapendekezo kuhusu jinsi ambavyo nchi za kusini zinavyoweza kutatua matatizo yao kupitia ushirikiano kati yao. Taasisi inatumia taarifa hii kuandaa utekelezaji wa mipango mikakati yake, sambamba na Azimio la Arusha.”

2212 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!