Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imewakosha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam kwa namna inavyotekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015.

Dawasa inatekeleza miradi mikubwa ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwa kutumia fedha zake. Hiyo ni hatua kubwa katika kuwafikishia maji wananchi kupitia kaulimbiu ya ‘Kumtua mama ndoo kichwani’.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) kwa kusimamia na kufanikisha miradi mbalimbali ya maji kwa fedha za ndani na kuacha kutegemea wafadhili.

Mama Kate Kamba alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam ilipotembelea miradi ya maji inayotekelezwa na kuendeshwa na Dawasa pamoja na kukagua maendeleo yake.

“Nawapongeza Dawasa kwa kutumia vyanzo vya ndani kwa kutenga asilimia 35 ya mapato kufanikisha miradi ya ndani bila kutegemea wafadhili, hili ni jambo la kujivunia sana.

“Nchi kwa sasa inakwenda mahali pazuri, tumetembelea baadhi ya miradi ya maji tumeona Dawasa ilivyofanikiwa kusimamia na kuendesha miradi ya maji, kwa sasa ni tofauti na miaka mitatu, sasa hivi maji ni mengi na maendeleo yanaonekana Dar es Salaam,” amesema Kamba.

Mwenyekiti huyo wa CCM amesema ifike mahali wataalamu wa ndani wa Dawasa watumike kuangalia namna ya kuvuna maji ya mvua kwani mvua zinaponyesha maji mengi hupotea.

“Tuangalie tunapokwenda, maji mengi ya mvua yanapotea, tuna wahandisi wengi… mje na mawazo ya kuokoa maji ya mvua, angalieni namna ya kutumia hata maji ya bahari,” amesema Kamba.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Cyprian Luhemeja, amesema ili kukabiliana na changamoto ya ukosekanaji wa maji katika baadhi ya maeneo mamlaka hiyo imeamua kutumia asimilia 35 ya mapato ya makusanyo yake ili kuendesha miradi katika maeneo mbalimbali.

Mhandisi Luhemeja aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji katika kipindi cha miaka mitatu cha mamlaka hiyo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Luhemeja amesema ili kufanikisha suala hilo walilazimika kutenga Sh bilioni 4 kila mwezi zinazotokana na mapato ya ndani.

“Hii imeshapitishwa na lazima suala hilo lifanyike kila mwezi, na tumefungua akaunti maalumu benki ambayo haiguswi na kila wakati huangaliwa kama kuna kiasi kisichopunguzwa,” amesema Luhemeja.

Amesema kupitia fedha hizo miradi 16 katika maeneo mbalimbali inatekelezwa huku sita kati yake ikiwa imekamilika, miwili inajengwa na mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za manunuzi ya mkandarasi.

“Tutaendelea kuhakikisha fedha hizi zinasaidia katika kuendesha miradi tunayotaka kuitekeleza badala ya kusubiri fedha kutoka kwa wahisani na serikali,” amesema Luhemeja.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, alipongeza uamuzi uliochukuliwa na Bodi ya Dawasa huku akibainisha kuwa suala la kubuni jinsi ya kutekeleza miradi kwa fedha za makusanyo linapaswa kuigwa na watu wengine.

“Unapotembeza bakuli kuomba msaada hauna uhakika, lakini unapobana kidogo kidogo cha kwako unakuwa na uhakika wa kufanya unachokusudia,” amesema Kamba.

Dawasa inatekeleza miradi 41 kwa fedha za ndani ambapo imetenga asilimia 35 ya mapato yao ya kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali.

“Katika kipindi cha miezi sita tumetumia shilingi bilioni 15 kwa ajili ya miradi 41 iliyopo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na mingine ikiwa ni mipya itakayotatua changamoto ya maji kwenye maeneo yaliyokosa mtandao kwa muda mrefu,” amesema Mhandisi Luhemeja.

Lengo kuu la Dawasa ni kuwekeza kwenye mtandao kwa kutumia fedha za ndani na kila mwezi wamekuwa wanatumia Sh bilion 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Gezaulole, Chalinze Mboga, Kisarawe, Kibamba, Kiwalani Phase 3 na miradi mingine.

Luhemeja amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam upatikanaji wake wa maji ni asilimia 85, ambapo kwa siku yanazalishwa maji lita za ujazo milioni 502 kutoka kwenye mtambo wa Ruvu Juu, Ruvu Chini, Mto Kizinga na visima vilivyojengwa na jamii au watu binafsi.

849 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!