Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU 

Wiki iliyopita kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen, ametangaza kikosi chake ambacho kilitarajiwa kukusanyika na kuingia kambini Jumapili ya juzi kwa ajili ya kujiandaa na michezo yake mbalimbali.

Ukikisikia au kukitazama kikosi hicho kilichoitwa, kwa hakika kinavutia sana machoni, hasa masikioni. 

Kinavutia zaidi unapoona kikiwa na mchanganyiko wa wachezaji wanaocheza ndani na nje ya nchi yetu, vijana kadhaa wakiitwa kwa mara ya kwanza wakitokea Ulaya wanakosakata soka la kulipwa. Hongera nyingi zimwendee Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Kim Poulsen.

Lakini kiuhalisia kikosi hiki kilichotajwa wiki iliyopita ni kama vile mwili wa ‘baunsa’. Kwa kawaida na inafahamika kwa wengi kwamba mwili wa ‘baunsa’ huwa unajazia kifuani hadi kwenye kiuno, lakini aghalabu miguuni huwa hakuna supu, nyama au musuli wa kutosha. Timu yetu ya taifa, Taifa Stars, iliyoitwa na Kim Poulsen ina sura kama hiyo.

Mashabiki wengi wanaofuatilia soka la ndani watakubaliana nami kwamba akina Kelvin Yondani, Agrey Morris na Erasto Nyoni ni miamba mitatu iliyotikisa soka la Tanzania kwa zaidi ya miaka 15. 

Hawa walikuwa ni sehemu ya vikosi vingi sana vya timu ya taifa vilivyokuwa vikiitwa kwa nyakati tofauti na makocha tofauti, pia jamaa hawa wamecheza mechi nyingi sana za Taifa Stars.

Katika masikitiko yangu ni kwamba safari hii Yondani na Erasto hawajaitwa. Na inasemekana kwamba wachezaji nyota hawa hawajaitwa kutokana na mizengwe. 

Hawana quality (ubora) ya kuvaa jezi ya Taifa Stars na kuwa askari wakakamavu katika uwanja wa vita. Hawana tena ubora waliokuwa nao. Kwamba hatimaye nyakati zao zimepita. Huu ni ukweli mchungu. 

Kwa upande wake, Morris ameshatangaza kustahafu kuchezea timu ya taifa. Tungeweza kumuomba arejee, lakini naye ni kama akina Yondani. Nyakati zimempita sambamba na ubora aliokuwa nao. Muda unaongea na tayari umeongea. 

Baada ya miaka mingi na muda mrefu kupita, hatimaye safari hii Taifa Stars imeingia kambini ikiwa na mlinzi mmoja tu wa kati. Nieleweke vema katika suala hili. Kwamba Taifa Stars imeingia kambini ikiwa na mlinzi mmoja tu wa kati. 

Haya sasa, twende pamoja na tutaelewana tu. Wale wachezaji wengine akina Hajji Mnoga, Dickson Job na Lusajo Mwaikenda, huwa wanacheza nafasi ya ulinzi wa kati, na muda mwingine huwa wanacheza sehemu tofauti tofauti uwanjani. 

Ndiyo. Kuna nyakati nyingine wachezaji hawa huwa wanacheza nafasi ya ulinzi wa pembeni, kiungo mkabaji. 

Kukosekana kwa Erasto Nyoni na wenzake hakukuja kwa bahati mbaya. Ukweli ni kwamba tayari nyakati zimewaacha nyuma. Muda wao wa soka la ushindani umepita au tayari umeshapita.

Walikuja na kuingia kikosini (Taifa Stars) kwa muda na nyakati tofauti, lakini wameondoka wote kwa pamoja na kwa bahati mbaya wameondoka bila ya kutuachia mtu madhubuti wa kuziba nafasi zao; ulinzi wa kati.

Walipoondoka kina Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hamis Yussuph ‘Waziri wa Ulinzi’, na Victor Costa ‘Nyumba’ hakukuwa na hofu kubwa kwa kuwa walikuwapo akina Yondani waliolipokea vema jahazi la Taifa Stars na kuendelea kufanya vizuri. Vipi kina Job wako tayari kuupokea mzigo huu?

Ligi yetu ina namba kubwa ya walinzi wengi wa kati. Lakini ni ukweli kwamba ligi hii haina walinzi bora. Ni wachezaji wachache wanaoweza kuitwa na kuichezea Taifa Stars na kuvaa jezi ya taifa letu. Wengi wako kawaida sana tu. 

Kando ya Abdi Banda na pacha wake wa pale Mtibwa Sugar, Ibrahim Ame, kuna wale akina Abdulrazack Maliki wa Namungo FC na Samson Madereke wa Mbeya City.

Hawa wanaweza kutupa kitu siku za baadaye iwapo watakuja kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars. 

By Jamhuri