Uteuzi wa Steve Nyerere Shirikisho la Muziki uwashtue wasanii

DAR ES SALAAM

NA CHRISTOPHER MSEKENA

Miongoni mwa mambo yanayoirudisha nyuma sekta ya sanaa nchini ni utamaduni wa wasanii kupuuza mambo muhimu yaliyowekwa kwa ajili ya ustawi wao.

Wiki jana tasnia ya burudani ilikuwa gumzo baada ya Shirikisho la Muziki Tanzania kumteua mchekeshaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ kuwa msemaji wa chombo hicho muhimu kwa wasanii.

Uteuzi huo umekuwa gumzo zaidi pale majina makubwa katika muziki kuinuka na kulipinga shirikisho huku wasanii wengine wakikubaliana na uteuzi huo.

Steve Nyerere ameweza kuwagawa wasanii katika makundi mawili kutokana na sababu nyingi, ila kubwa ni ile ya kutokuwa mwanamuziki, hivyo wanahoji ataweza vipi kuwasemea wasanii wa muziki?

Wasanii nyota waliojitokeza hadharani kupinga uteuzi wa Shirikisho la Muziki ni Diamond Platnumz aliyeshangazwa na mwigizaji huyo kupewa nafasi ya kuwasemea wasanii.

Diamond Platnumz ameweka wazi mtazamo wake kuwa shirikisho limeikosea heshima tasnia ya muziki ambayo imetoa ajira kwa mamilioni ya vijana kwa sababu ya uteuzi wa Steve Nyerere.

Hivyo kitendo cha shirikisho hilo kufanya uteuzi huo kunaidhalilisha tasnia kwa sababu walipaswa kumpa nafasi hiyo mwanamuziki mwenzao na si mwigizaji/mchekeshaji.

Diamond alikwenda mbali zaidi kwa kumchana mmoja wa viongozi wa shirikisho hilo, Farid Kubanda a.k.a Fid Q, kwa kile alichodai kuwa rapa huyo amejivunjia heshima kwa kushiriki kumteua Steve Nyerere huku akijua haujui muziki.

Hali kadharika rapa Nay wa Mitego aliwapa makavu viongozi wa shirikisho hilo kuwa wanauchezea muziki kwa kuweka masihara kwenye mambo makini yanayohusu muziki.

Nay wa Mitego alikwenda mbali zaidi kwa kudai halifahamu kabisa shirikisho hilo zaidi ya kuwa mwanachama wa Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya, na hiyo yote ikiwa jinsi gani hakubaliani na Steve Nyerere kuwa msemaji wa wanamuziki.

Hao ni baadhi tu ya wasanii wakubwa ambao wameonyesha wazi kutofurahishwa na uteuzi huo lakini pia kuna kundi la wasanii linakubaliana na shirikisho kwa kufikia uamuzi huo.

Katika mvutano wote huo nimeweza kujifunza mambo kadhaa yaliyomo kwenye tasnia ya muziki, hasa wale wanaofanya Bongo Fleva na yamekuwa yakiikwamisha tasnia nzima.

Kwanza, nimegundua wasanii wengi si washiriki katika vyama vyao vya muziki. Kama nilivyosema hapo mwanzo kuwa wasanii wengi hasa maarufu wanapenda kupuuza kushiriki kwenye mambo yaliyowekwa ili kusimamia ustawi wao.

Katika hili la Steve Nyerere nimeona jinsi gani wasanii hawajui hata kama kuna shirikisho la muziki linalosimamia aina zote za muziki. Ndani ya shirikisho kuna muziki wa Bongo Fleva, taarabu, dansi, singeli na nyinginezo kibao.

Huu ndio umoja wenye nguvu zaidi kwa sababu vyama vya muziki vyote vinakutana kwenye shirikisho lakini ajabu wasanii hawajui kama lipo ambalo ni chombo muhimu kwa ajili ya ustawi wao, hilo ni tatizo kubwa.

Mara kadhaa nimekuwa nikishuhudia mialiko ya shirikisho kwenda kwa wanamuziki kuhusu vikao muhimu lakini ubaya ni kwamba wasanii hao hawashiriki na hawatumi hata wawakilishi.

Ndiyo maana unapofanyika uamuzi mkubwa kama huo wa kumteua Steve Nyerere kushika nafasi hiyo ambayo haikuwepo hapo kabla, wasanii hao hao wanalalamika wakati walikuwa na nafasi ya kukataa au kushauri kabla.

Vikao vingi vya shirikisho na wasanii, wanamuziki chipukizi ndio wanajitokeza kwa wingi kuliko wale maarufu ndiyo maana unapotolewa uamuzi mastaa lazima walalamike kwa sababu huwa wanapuuza vikao hivyo.

Pili, nimegundua miongoni mwa wasanii wenyewe kuna makundi mengi. Wasanii hawapendani, hawashirikiani, hivyo kuweka mpasuko unaofanya wasiweze kukaa pamoja.

Ndiyo maana tasnia inahitaji kulipa shirikisho nafasi ya kufanya kazi bila kuingiliwa ili kuondoa hivyo viambaza vinavyoikwamisha tasnia ya muziki.

Ni mapema kusema kwamba Steve Nyerere ataweza kazi ya kuwasemea wanamuziki au hataweza, lakini ni vema kumpa nafasi afanye kazi na asipoweza kuna namna ya kumtumbua na si kuanza kumkataa wakati kazi bado hajaifanya.