UJUMBE WA KWARESMA – (2)                                                            ‘Tunawasihi kwa jina lake Yesu  Kristo, mpatanishwe na Mungu’

Hii ni sehemu ya pili ya Ujumbe wa Kwaresma kwa mwaka 2022 kama ulivyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC). Tuendelee…

Agano Jipya

9. Kwa njia ya dhambi binadamu anatengeneza uadui na  Mungu. Anatengwa na Mungu na anakuwa chini ya ghadhabu  yake, wala hawezi kuwa na ushirika naye (taz. Rum 1:18; 8:7-8; Efe 2:3; Kol 1:21). 

Mungu kwa utakatifu wake ni mwenye upendo kwa mambo mema na anachukia maovu. Tunapotafakari ‘Tunawasihi mpatanishwe na Mungu’  (2Kor 5:20) aya hii inafungua na kuimarisha Ukristo na fundisho la upatanisho. 

Utimilifu wa uwepo wa Mungu katika Kristo ni hali ya tabia inayowajumuisha wote na upatanisho. Andiko hili la Mtume Paulo ni moja ya ushauri mzito alioutoa kwa Wakristo wa Korintho. Kuanzisha uadui na Mwenyezi Mungu ni jambo lenye hasara kubwa sana kwa binadamu.  

10. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kanuni ya msingi ya upatanisho haijabadilika tangu Agano la Kale.  Mshahara wa dhambi bado ni kifo. Tofauti kati ya upatanisho katika Agano la Kale na upatanisho katika Agano Jipya upo juu ya kile kinachotolewa katika dhabihu. 

Sadaka za Agano la Kale zilikuwa na maana kubwa kwa mwenye dhambi aliyetubu. Lakini damu ya wanyama haikuweza kuondoa dhambi moja kwa moja (taz. Ebr 10:4). 

Damu ya Kristo tu, yaani kifo chake msalabani, iliweza kufanya hivyo. Kilele cha mipango ya Mungu ya wokovu kilipatikana katika Kristo, maana yake jambo la pekee linalotoa upatanisho na Mungu ni kifo cha Kristo. 

11. Barua kwa Waebrania inatuonyesha wazi: “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” (Ebr 9:22). 

Kifo cha Yesu msalabani kinalipa adhabu ya dhambi mara moja. Kifo chake kinafunika dhambi zote za watu wote ambao wamewahi kuishi. 

Kwa damu ya Yesu iliyomwagika binadamu  alipatanishwa na Mungu. Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. 

“Kwa  maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama wa ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo maovu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? “Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.” (Ebr 9: 12-15). 

12. Kadiri ya Biblia, upatanisho ni kuondolewa kwa dhambi ili kurejesha uhusiano kati ya watu na Mungu. Kwa kuchukua adhabu kwa dhambi zetu juu yake mwenyewe, Yesu amefungua mlango wa watu wote kujipatanisha na Mungu na tena kurejesha furaha ya uhusiano na Yeye.  

Wenye dhambi hupokea manufaa ya upatanisho huo wanapomwitikia Mungu kwa imani na toba (taz. Rum 5:1; 2Kor 5:20). Amani huingia mahali pa uadui (taz. Efe 2:3; 14-17). Na amani hiyo ni zaidi kuliko kuondolewa uadui tu, ni hali ya utulivu wa kiroho iliyotokana na kurejeshwa kwa uhusiano mwema na Mungu. 

13. Baada ya kupokea kazi ya neema ya upatanisho wa Mungu, wakati huu wa Kwaresima, waamini wanapaswa kutangaza neema hiyo kwa watu wengine, ili hata wao waweze kupatanishwa na Mungu (taz. 2Kor 5:18). Zaidi ya hayo wanapaswa kuwa watu waliopatana na watu wengine.  

Ikiwa ni katika jumuiya ya Wakristo au nje yake, Wakristo wanapaswa kujaribu kuishi kwa amani na watu wengine (taz. Mt 5:23-26; Rum 12:18-21; 2Kor 6:11-13), nao wahimize tabia hiyo hata kwa watu wengine (taz. Mt 5:9). 

Pia wanapaswa kufanya bidii kuelekea kupatanisha watu na ulimwengu wa viumbe vingine ambamo wanaishi. 

Upatanisho wa namna hii ni sehemu ya makusudi ambayo Kristo alikufa kwa ajili hiyo (taz. Rum 8:19-23; Kol 1:16-20). Wakati huu wa Kwaresma, tunaalikwa kujipatanisha na Mungu kwa kuwa yeye ndiye anayetoa msamaha kwa makosa yetu. 

Aidha, tunaalikwa  kuchukua hatua za kumwendea Mungu tuliyemkosea na hata wenzetu tuliowakosea. Tuimarishwe na mfano mzuri wa Injili wa upatanisho, ule wa baba anayempokea mwana wake mpotevu anayerudi na anayetubu makosa yake (taz. Lk 15: 11-32). Tukubali kupokea huruma ya Mungu kwa kujipatanisha naye na jirani. 

14. Kwa kweli ni neema ya Mungu inayotupatia moyo  mpya kutupatanisha naye na sisi kwa sisi. Ni Kristo aliyerudisha ubinadamu katika upendo wa Baba. Upatanisho  chanzo chake ni katika upendo huo; unaotokana na uamuzi  wa Baba wa kufanya upya uhusiano wake na binadamu,  uhusiano uliovunjwa na dhambi ya binadamu. 

Katika Yesu Kristo, katika maisha yake na katika huduma yake, lakini hasa katika kifo na ufufuko wake, Mtume Paulo alimwona Mungu Baba akiupatanisha ulimwengu (vitu vyote mbinguni na duniani) naye, bila kuhesabia dhambi ya binadamu (taz. 2Kor 5:19; Rum 5:10; Kol 1:21-22). 

Paulo alimwona Mungu Baba akiwapatanisha Wayahudi na watu wa mataifa kwake, akiumba mtu mmoja mpya kwa njia ya msalaba (taz. Efe  2:15; 3:6). 

15. Kwa namna hiyo, tendo la upatanisho hujenga ushirika katika ngazi mbili: Ushirika/muungano kati ya Mungu na binadamu; na ushirika kati ya watu – kwa kuwa tendo la upatansiho pia hutufanya sisi (kama binadamu tuliopatanishwa) kuwa mabalozi wa upatanisho. 

Upatanisho unarudisha pia uhusiano kati ya watu kwa njia ya maridhiano ya tofauti zao na kwa kuviondoa vizuizi vya uhusiano wao kwa kuonja kwao upendo wa Mungu. 

Mtaguso wa Pili wa Vatikano na Katekisimu ya Kanisa Katoliki juu ya upatanisho 

16. Mtaguso wa Pili wa Vatikano unahimiza na kuhusisha upatanisho na Sakramenti ya Kitubio. Taifa la Mungu linaalikwa kuitumia vema Sakramenti ya upatanisho katika kujipatanisha na Mungu na kisha binadamu wenzake.  

“Wanaoijongea sakramenti ya kitubio hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la makosa yaliyotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na kianisa, ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala huhangaikia wongofu wao,” (LG 11). 

Dhambi haiathiri tu uhusiano wa mtu na Mungu lakini pia uhusiano wa mtu na Mwili wa Kristo, Kanisa. 

17. Kwa sababu hii, Mtaguso wa Pili wa Vatikano unaona kwamba, sakramenti ya upatanisho si tu kwa ajili ya msamaha wa dhambi (kati ya mwenye kutubu na Mungu); bali pia inatakiwa kusherehekea na kutekeleza upatanisho, ambao ni ukweli wa kijumuiya, muundo ambao hutupatia uwezo wa kuwa Mwili wa Kristo kwa ufanisi zaidi.  

Hata Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua zaidi kwamba: “Awali ya yote, dhambi ni chukizo kwa Mungu, kuvunjika kwa muungano naye. Papo hapo dhambi yaharibu muungano na kanisa. Kwa sababu hiyo uongofu huleta papo hapo msamaha wa Mungu na upatanisho na kanisa, ambao hudhihirishwa na kutekelezwa kiliturujia kwa njia ya sakramenti ya Kitubio na Upatanisho,”(KKK 1440). 

18. Mtaguso wa Pili wa Vatikano unalifafanua kanisa kama ‘Sakramenti ya wokovu – ishara na chombo, ambacho  kinafanya ushirika na Mungu na umoja kati ya watu wote,’ na kwa kuonyesha kama kazi ya kanisa ni ile ya kupata ‘umoja kamili katika Kristo’ mababa wa Mtaguso walitambua kwamba kanisa lazima lijitahidi zaidi ya yote kuwaleta watu wote kwenye upatanisho kamili. (LG 34). 

Mtu anayetubu na anayesamehewa hupatanishwa na yeye mwenyewe katika nafsi yake ya ndani; anapatanishwa na ndugu zake ambao kwa njia fulani amewakwaza na kuwajeruhi. Anapatanishwa  na kanisa.

Anapatanishwa na viumbe vyote; “Nguvu yote ya Sakramenti ya Kitubio inajumuisha kuturejeshea neema ya Mungu na kuungana nasi pamoja naye katika urafiki wa karibu,” (KKK 1468); “Kwa wale wanaopokea sakramenti kwa moyo wa unyenyekevu na tabia ya uchaji, upatanisho kawaida hufuatwa na amani na utulivu wa dhamiri na faraja ya kiroho,” (KKK 1551). 

Itaendelea…