CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na viti mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya sekondari ya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Msaada huo ulikabidhiwa jana shuleni hapo na Mkurugenzi wa Taaluma wa CBE, Dk. Shima Banele, katika hafla fupi iliyowashirikisha wanafunzi zaidi ya 110 wa shule hiyo wenye mahitaji  maalum.

Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk. Shima Banele ambaye ni Mkugenzi wa Taaaluma wa chuo hicho akimsukuma mwanafunzi kwenye wheelchair walipokwenda kutoa msaada wa viti mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya sekondari Jangwani jijini Dar esSalaam jana

Akizungumza maara baada ya kukabidhi msaada huo, Dk. Banele alisema  chuo hicho kimejenga utamaduni wa kusaidia shule hiyo kila mwaka kwani inapokea wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma elimu jumuishi.

Dk. Banele alisema chuo hicho kitaendelea kusaidia shule hiyo ili wanafunzi wenye mahitanji maalum waweze kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao siku za baadaye.

Alisema kila mwaka chuo hicho kimekuwa na utamaduni wa kuchukua sehemu ya wanachopata na kurejesha kwenye makundi mbalimbali ndani ya jamii kama sehemu ya kutambua mchango wake kwa chuo.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari kwani wanafunzi wengi walikuwa wanashindwa kwenda shule kutokana na kukosa ada.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam Paulina Aweda (kulia) akionyesha tuzo ambayo alipewa jana na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutambua mchango wa shule hiyo kutunza na kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakati walipowatembelea jana shuleni hapo na kuwapa zawadi mbalimbali vikiwemo viti mwendo.

Alipongeza pia hatua ya serikali kuweka elimu jumuishi ambapo wanafunzi wenye mahitaji maalum wamekuwa wakichanganywa na wale ambao hawana changamoto yoyote.

Aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuachana na fikra za kujiona wanyonge kwani wakijiamini wanaweza kufaulu vyema kwenye masomo yao na kufanya vizuri kwenye elimu ya vyuo vikuu.

“Mnaweza kuwa na changamoto ya maumbile lakini ubongo wenu unafanyakazi vizuri kwa hiyo msifikirie kwamba hamuwezi, mnaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii kama mtajibidisha na mkafaulu vizuri,” alisema

“Mtakapomaliza sekondari mkafaulu vizuri na kwenda vyuo vikuu mkimaliza hangaikeni kutafuta ajira kwasababu mnauwezo wa kufanyakazi kama wengine. Kila mtakapoona nafasi za ajira pelekeni wasifu wenu,” alisema

Aidha, aliwataka kuishi kwa upendo na kupeana moyo kwenye masomo yao ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao na kukua kitaaluma badala ya kukandamizana kwa uchoyo na chuki.

“Mimi leo hapa namwakilisha Mkuu wa chuo cha CBE lakini kwa nafasi yangu pale ni Mkurugenzi wa taaluma sasa kama mimi nimeweza kufika nilipo kwa sasa kwanini kesho usiwe wewe.  Kwa hiyo unatakiwa kuanza kufikiria kesho yako leo hii na ninaamini mtafanikiwa sana mkijituma,” alisema

Makamu Mkuu wa shule hiyo, Paulina Aweda, alisema shule hiyo inawanafunzi 110 wenye mahitaji maalum na wanasoma masomo yote kama walivyo wanafunzi ambao hawana changamoto yoyote.

Aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanasoma bila vikwazo vyovyote na kwamba wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho ya kitaifa.

Alisema wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wamekuwa wakipatiwa chakula, malazi na mahitaji mengine yote wanapokuwa shuleni hapo hali ambayo imewawezesha kufanya vizuri kitaaluma.

“Tunabahati ya kuwa na waalimu wa kutosha waliosomea elimu maalum ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa hiyo serikali imewafikiria kwa kiwango kikubwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” alisema

Please follow and like us:
Pin Share