Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeanza kutoa mafunzo kwa wahudumu wa kwenye mabasi ya abiria ili kuifanya kazi hiyo kuheshimika kama zilivyo fani zingine.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga wakati wa uzinduzi wa amesema katika kuunga mkono juhudi za serikali CBE imeamua kutoa mchango wake katika kukuza weledi na ufanisi wa wahudumu wa usafiri wa umma.

Amesema lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinakuwa na ubora wa hali ya juu na kwamba CBE ni miongoni mwa taasisi ambazo zimepewa kibali cha kutoa mafunzo hayo.

Amesema tayari chuo kimeshaandaa mitaala, mwongozo wa mafunzo, pamoja na kuandaa wawezeshaji na vitendea kazi vyote muhimu kwa mafunzo hayo.

“Ni matarajiio yetu kuwa mara tu baada ya uzinduzi huu chuo kitaanza rasmi udahili wa washiriki wa mafunzo na yatafanyika katika vituo vilivyoko katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya,” amesema.

Amesema CBE inatambua juhudi zilizofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), katika kuboresha usafiri wa barabara nchini.

Amesema kuanzishwa kwa LATRA kupitia Sheria ya Udhibiti wa Usafiri ya mwaka 2019 ilikuwa hatua muhimu katika kusimamia na kuboresha sekta hiyo  muhimu.

“Hata hivyo bado tunashuhudia sekta hii ikiendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uvunjifu wa sheria na  kanuni za usalama barabarani, huduma kwa wateja isiyoridhisha hali hii inahitaji jitihada zaidi kutoka kwa wadau wote,” amesema.

Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi, Michaek  Deleli, alisema Jeshi hilo linaona mafunzo hayo ni fursa kubwa kwasababu yataondoa changamoto nyingi za barabarani kwenye usafiri wa umma.

“Kuna mambo yanafanyika ya kiuhalifu kwenye usafiri wa umma na yanatokana na wahudumu kutokuwa na elimu sahihi, mfano tumeshuhudia kusafirishwa kwa wahamiaji haramu vitendo vinafanywa na wahudumu wasio na mafunzo wala kujua sheria za nchi,” amesema.

Alisema hata dawa za kulevya zinasafirishwa kupitia magari hasa mabasi lakini yanapokamatwa wahudumu wanashindwa kuwatambua wamiliki hali ambayo imekuwa ikisababisha changaoto.

 “Kwa mfano tunapokamata mzigo haramu kwenye basi unakuta mhudumu wa basi hajui ni wa nani na ukiwauliza hata abiria wanaukataa lakini wakipata  mafunzo haya wataweza kuweka mizigo kwa namna ambayo kila mwenye mzigo atatambulika kwa urahisi,” amesema.

Mweka Hazina wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mbazi Mjema aliipongeza serikali kwa uamuzi wa kuanzisha mafunzo hayo kwani yatasaidia chama hicho kutimiza majukumu yake na utendaji wa kazi utaboreshwa.

 “Tunawafanyakazi wengi wa darasa la saba kwa hiyo vyeti watakavyopata ni mali yao wakihama kampuni moja kwenda nyingine cheti kinabaki ni mali yao binafsi kwa hiyo tupunguzieni ada ya mafunzo ili tuweze kuwapeleka mafunzo wahudumu wengi,” amesema.

By Jamhuri