Wanachama wa Chama Cha  Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wamewakataa viongozi watatu wa chama hicho mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Mwakasubi, JAMHURI inaweza kuripoti.
Viongozi waliokataliwa na wanachama hao ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Igunga, Abdallah Kazwika, Katibu Msaidizi Wilaya hiyo, Flora Machichu, na Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) wa Wilaya hiyo, Deus Thomas.


  Wanachama hao waliwakataa viongozi hao kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi za CCM wilayani hapa, ambako kilio kikubwa cha wanachama hao ni kushindwa kwa viongozi hao kusimamia kazi za chama, hivyo kushauri waondolewe.
Jumanne Rashid, mmoja wa wanachama hao, anasema wanashangazwa na viongozi wao kwa kushindwa kuitisha mikutano ya wanachama kwa ajili ya kukijenga chama chao na badala yake wamekuwa wakifanya kazi kwa maslahi yao binafsi, hali ambayo imesababisha baadhi ya vitongoji kuchukuliwa na upinzani.
  Hata hivyo, wanachama hao kwa ujumla walibainisha kwamba hivi karibuni katibu wa wilaya alichangisha Sh. 10,000 kwa kila tawi la CCM kwa madai kuwa zinakwenda kufanya shughuli za chama.


Licha ya michango hiyo, vile vile katibu huyo aliwachangisha Sh. 150,000 kwa baadhi ya wenyeviti walioshindwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita, na kushindwa katika nafasi za vitongoji na vijiji kwa kuwaahidi kuwa angewatafutia wakili wa kusimamia kesi zao walizofungua katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga.
Wanachama hao walidai kuwa ili kukinusuru chama katika uchaguzi ujao, viongozi hao wanatakiwa kuhakikisha wanahamishwa wilayani Igunga.


 “Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa, leo tunakuomba hawa viongozi uondoke nao, sisi hatuwataki katika wilaya yetu kwani hapa wapo kwa maslahi yao binafsi na siyo kwa maslahi ya chama chetu,” alisikika mmoja wa wanachama hao, huku akishangiliwa kwa makofi.
 Hata hivyo, baada ya mwenyekiti kusikiliza malalamiko ya wanachama kwa zaidi ya saa nne, ndipo viongozi hao walipotakiwa kujibu tuhuma hizo kwa kila mmoja kujieleza na ndipo baada ya kupewa nafasi hiyo, viongozi hao walionekana kuanza kujikanyaga katika kujibu tuhuma wanazolalamikiwa na wanachama wao.
  Kutokana na majibu yao, mwenyekiti kwa upande wake pia alionesha kutoridhishwa na majibu yao na ndipo alipowaomba wanachama wampe muda, ili aweze kuzipatia ufumbuzi tuhuma hizo na kuahidi kurudi mjini Igunga kutoa majibu kwa wanachama hao.


Hata hivyo, wanachama hao licha ya kuridhika na maombi ya mwenyekiti wa mkoa, lakini walishauri pia kwamba endapo viongozi hao wataendelea kufanya kazi katika ofisi ya chama ya wilaya, itawalazimu kwenda kuonana na Katibu Mkuu wa CCM (Taifa), Abdulrahman Kinana, ili aweze kuwaondoa.

 
2369 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!