Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kupitia maabara yake ya utafiti wa madini, imefanikiwa kuongeza thamani ya madini ya nikeli (Ni) kutoka katika mbale za Milima ya Mahanza-Haneti mkoani Dodoma.
  Akizungumza na MEM Bulletin, Mhandisi Priscus Kaspana, mmoja wa wanajopo la watafiti kutoka GST, anasema kuwa utafiti huo ulianza Machi 2015, na tayari sampuli nne zimefanyiwa utafiti wa uongezaji thamani kupitia maabara ya GST, huku  sampuli moja ikionesha  kuwa na madini ya nikeli yenye oksaidi kwa asilimia 3.34 (NiO).
  “Baada ya kufanyiwa uchunguzi, GST, kupitia wataalamu wake wa maabara, wameweza kuongeza thamani na kufikia kiwango cha asilimia 2.6280 yenye nikeli halisi bila oksaidi (2.6280 Ni),” anasema Mhandisi Kaspana.
  Kadhalika, anasema kuwa katika maendeleo ya utafiti huo, sampuli nyingine yenye madini ya nikeli na oksaidi (NiO) kwa kiwango cha asilimia 6.66 kutokana na utafiti huo, GST, kupitia wataalamu wake ndani ya maabara, wameweza kuongeza thamani kufikia kiwango cha asilimia 5.24035 yenye nikeli halisi (Ni).
  “Utafiti wetu ulianza mwezi Machi mwaka huu wa 2015, tulichukua sampuli kutoka katika milima ya Haneti, sampuli moja ilituonesha kuwa na kiwango cha nikeli yenye oksaidi kwa asilimia 3.34 ilichunguzwa na kuongezewa thamani kufikia asilimia 2.6280 ikiwa nikeli halisi bila oksaidi, na nyingine tuliongezea thamani kutoka asilimia 6.66 NiO na kufikia asilimia 5.2403 nikeli isiyo na oksaidi,” anasema.
  Naye Meneja wa Mawe, Madini na Uchakataji kutoka GST, Philipo Momburi, anasema kuwa kuwapo kwa mafanikio ya utafiti huo kunaongeza tija kutokana na ongezeko la mahitaji makubwa ya madini hayo ya kiteknolojia duniani hususani katika nchi za viwanda.
  Momburi anaeleza kuwa madini hayo nchini Tanzania yanapatikana sehemu mbalimbali ambazo ni eneo la Kabanga Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera (Kabanga Nickel), eneo la Kapalagulu, Zanzuri, Kaskazini Ukinga, Ngasamo, Kaskazini Mara, Itiso, Milima ya Haneti mkoani Dodoma, Milima ya Uluguru na Milima ya Mbalangeti.
  Vilevile, anasema sambamba na maeneo hayo, tayari eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Itiso na Haneti yameanza kufanyiwa utafiti na unaendelea, ambapo katika utafiti huo, eneo la Itiso na Haneti yameonesha matumaini makubwa kutokana na wawekezaji kuwasilisha sampuli kwa wingi katika maabara ya GST kwa ajili ya upimaji wa sampuli zao.
  Momburi ametoa wito kwa Serikali na wadau kuweka nguvu zaidi katika madini ya nikeli ili kuweza  kufanya mchakato wa utafiti nchi nzima.
  Aidha, amewataka   wazawa kutumia fursa hiyo ya madini ya nikeli katika utafiti na upimaji ili kuweza kuwekeza kwa lengo la kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuongeza ajira pamoja na Pato la Taifa (GDP).
  Matumizi makubwa ya madini ya nikeli ni kutengeneza betri za simu, kutengenezea pesa za fedha (silver-coins). Nikeli hutumika pia katika glasi kuipa rangi ya kijani; hutumika pia kama kichochezi cha kuhifadhi mafuta ya mimea. Nikeli hutumika katika mitambo ya kielektroniki pamoja na kulinda vifaa mbalimbali vya chuma visipate kutu ikiwa ni pamoja na  kutumika katika vifaa mbalimbali vya umeme kama vile nyaya.

 
2798 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!