Changamoto zilizopita zilete suluhu

DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga

Miaka takriban 70 ya vyama vya siasa na uhuru Afrika; Tanzania ikiwa na uzoefu wa takriban miaka 30 ya siasa za vyama vingi, lakini bado haijashuhudia upinzani ukiinusa Ikulu ya Tanzania Bara wala ya Zanzibar.

Pamoja na malalamiko yanayoibuka kila baada ya uchaguzi, Tanzania ya vyama vingi vya siasa imeendelea kuwa chini ya chama kimoja; Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chama hiki hujihakikishia ushindi katika kila nafasi inayowaniwa, hali ambayo imezorotesha matumaini ya wengi kuiondoa CCM madarakani licha ya ushiriki wa vyama zaidi ya 10 katika kila uchaguzi, vikichuana kushika dola.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa matumaini ya kisiasa nchini yanaendelea kushuka kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulioiacha nchi ikiwa chini ya CCM katika nafasi zote.

Mwaka mmoja nyuma, CCM ilitwaa mitaa, vijiji na vitongoji vyote nchini. Uchaguzi huo wa mwaka 2019 na 2020 umelalamikiwa kuwa michakato yake haikuridhiwa na vyama vingine.

Kinachoacha midomo wazi kwa Watanzania wengi hasa wanaopenda kuona heshima katika juhudi za ujenzi wa taifa, demokrasia na misingi ya utawala bora wa kisheria, ni pale viongozi walio juu kutoyaishi wanayoyadai kuyaishi.

Hisitoria inafichua kuwa tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya vyama vingi, 1995, mpinzani aliyebeba matumaini ya wengi waliotamani mageuzi, Augustine Mrema (NCCR-Mageuzi), alikuja kutoa kauli tata na kugombana na chama chake.

Baadaye akaendelea kula maisha katika nafasi mbalimbali nyingine za uteuzi.

Mpinzani mwingine aliyetikisa miaka ya 1995 – 2010, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), alijifutia umaarufu wake baada ya kutangaza kujivua uenyekiti wa taifa wa chama hicho katikati ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Uchaguzo huo ulikuwa na upinzani wa nguvu zaidi nchini na kutoa matumaini ya kuiondoa Ikulu CCM.

Uamuzi wa Lipumba ukazorotesha umoja wa vyama vya upinzani na kuua heshima ya CUF Zanzibar.

Wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanakitazama pia kitendo cha ACT-Wazalendo na Chadema kuingia katika matendo yanayokinzana na matamko yao kama sehemu ya dhoruba la upinzani Tanzania.

Baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana, Chadema na ACT kwa pamoja vilitoa matamko mazito kulaani mchakato wa uchaguzi, ukidaiwa kugubikwa na hujuma na udanganyifu.

Vikatoa msimamo wa kutotambua matokeo na fursa zote ambazo zingetokana na uchaguzi huo.

Shida ikaanza baada ya Mwenyekiti wa ACT Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad, kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.

Maalim aliyekuwa mpinzani mkuu katika mbio za urais Zanzibar, alisema alifikia uamuzi huo baada ya michakato halali ndani ya ACT kuridhia uamuzi huo.

Chadema nako hakukuwa kimya, kwani siku kadhaa baada ya kuweka misimamo yake, makamanda wanawake wa chama hicho wakiwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya chama hicho, walishuhudiwa wakila kiapo mbele ya Spika wa Bunge kuchukua nafasi za ubunge wa Viti Maalumu vilivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa chama chao.

Kina mama 19 wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, walikula kiapo Dodoma siku chache kabla ya Chadema kuwaita kwa dharura na kuwavua uanachama wakidaiwa kukiuka misimamo na taratibu za chama.

Wamekata rufaa ngazi ya juu ya chama wakidai watabaki kuwa Chadema.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, aliamini kuwa wanasiasa hawawezi kuleta mageuzi ikiwa hawatakuwa huru kifikra na kusimamia kwa ari yale wanayoyaamini kwa mustakabali wa taifa.

Mtikila alipendekeza mambo kadhaa kwa wapinzani wa kisiasa nchini, akiwaasa wanasiasa hasa vijana, kuwa ili upinzani uzae matunda na kulisaidia taifa, mambo kadhaa ya kimifumo lazima yashughulikiwe na kufanyiwa mabadiliko.

Mambo hayo ni pamoja na mabadiliko ya Katiba iendane na muktadha wa siasa ya vyama vingi na kuweka mifumo rafiki ya jamii kushiriki shughuli za kisiasa bila bughudha.

Misingi ya madai ya Mtikila inaweza kutumika hata leo kutatua changamoto zinazokabili maendeleo ya kijamii, ikiwamo namna ya kuchagiza siasa safi na utawala bora kwa maendeleo ya jamii, mamlaka na mtu mmoja mmoja kwa nafasi yake, kuyatazama yafuatayo kwa lengo la kuleta mabadiliko.

Madai ya Katiba mpya

Katiba ya sasa iliundwa wakati wa chama dola, chama tawala ndicho kina mamlaka ya uchaguzi na namna ya uendeshaji wa siasa za nchi kupitia wateule wa kiongozi wake mkuu, ambaye pia ni Rais.

Kutarajia kumshinda mgombea wa chama tawala na kutangazwa katika mazingira ambayo ni sawa na watu wawili wanaogombea ndizi; mmoja ameshikilia mkungu na kisu, wakati mwenzake anaomba kibali agombanie, ni unafiki wa kiwango cha shahada ya uzamivu.

Lazima vyama vidai Katiba mpya na chama chochote kitakachopuuza ajenda hii kinastahili kupuuzwa na kila anayetamani ustawi wa demokrasia.

Tume mpya, huru ya uchaguzi

Jambo muhimu la pili, vyama vijikite kulaani na kupinga Tume ya Uchaguzi ya sasa kwani upatikanaji na muundo wake unatokana na mfumo wa chama kimoja kupitia mamlaka zake.

Hii inadhoofisha afya ya uhalali na uhuru wa kusimamia haki ya upinzani katika uchaguzi.

Chama cha siasa kitakachopuuza matakwa ya tume huru ya uchaguzi kitazamwe kwa jicho makini na wananchi wanaotamani uchaguzi huru na wa haki.

Ushirikiano wa vyama vya upinzani

Upendo huleta mapatano; mapatano huleta umoja na umoja huleta ushindi.

Vyama vya upinzani haviwezi kukiondoa chama tawala Ikulu ikiwa vitapambana vyenyewe kwa vyenyewe. 

Hii itafanya vyama visivyo na nguvu vijishikize kwa chama tawala ili kuwahujumu wenzao wanaofanya watawala wakose usingizi. Ni kudhoofisha nguvu ya upinzani na kuhubiri unafiki majukwaani.

Upendo, umoja na ushirikiano wa kweli wenye masilahi sawa kwa vyama vyote vya upinzani ni fimbo yenye nguvu zaidi kwa vyama.

Kwa Tanzania ya leo, chama chochote cha siasa kitakachopuuza matakwa haya, kipuuzwe na wote wenye nia njema.

Vyama kujenga taasisi, misingi kuliko watu

Upinzani wa Tanzania, tangu awali umeshindwa kuzaa matunda kutokana na kujenga misingi na ushawishi wake kwa kutumia ‘nguvu ya mtu/watu’.

CUF imebebwa na jina la ‘Lipumba’ na makada wachache wenye umaarufu, ACT ni ya ‘Zitto’, ‘Maalim’ na wengine wachache sana, pia katika vyama vingine.

Hali hii inafanya vyama kuishia kunadi na kupata wafuasi kwa kumfuata mtu au watu fulani na si kushawishiwa na falsafa, itikadi na madai ya chama katika utetezi na ujenzi wa jamii na taifa.  

Ndiyo maana kwa siasa za Tanzania, kujiunga au kujiondoa mtu mmoja katika chama kuna nafasi kubwa kukuza au kukiua chama hicho.

Hizi ni siasa zisizo na masilahi kwa taifa, bali ni mchezo wa watu kusaka umaarufu na nafasi za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Vyama vinapaswa kusimama katika itikadi, madai na msimamo maalumu na misingi na madai hayo yajengwe katika ajenda ya taifa kama nguzo ya sera zake na yajulikane kwa wananchi. 

Hii itaondoa nguvu ya mtu bali chama kama taasisi kitavuta watu na kujengeka.

Chama kisichotii matakwa haya, hakina nia ya kweli.

Watanzania kuacha unafiki

Upinzani wa Tanzania umekuwa na wafuasi wengi wanafiki ambao wapo kimasilahi. 

Ukisimama katika vyama vya siasa Tanzania si chini ya saba watafagilia upinzani lakini uchaguzi ukifika upinzani huambulia kura za aibu, huku idadi kubwa ya wafuasi wakidai uchaguzi kugubikwa na hila na ukiwauliza husema hawakupiga kura.