CHAUMMA: Tunawaomba wadau,wanachama kukichangia chama ili kufanikisha mikutano yake

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimewaomba wadau na wanachama wa chama hicho kukichangia chama ili kufanikisha mikutano yake ya hadhara ambayo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2023.

Tamko hilo limetolewa leo Machi 11, 2023 jijini Dar es Salaam na mwenyekiti taifa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe Spunda mara baada kikao cha Kamati kuu ya chama hicho.

Rungwe amesema kwa sasa chama hakina pesa za kutosha za kuendesha mikutano yao nchi nzima hivyo wanatarajia kufanya mikutano yao ya awali kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya shughuli ikiwemo maeneo ya masoko na stedi za mabasi.

“Tunawaomba wadau,mashabiki na wanachama kukichangia chama kupitia akaunti zetu za CHAUMMA kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha kufanikisha kufanya kampeni zetu na kutoa sera za chama na kuainisha mapungufu ya Serikali inayotutawala ambayo inaongozwa na CCM”amesema Hashim Rungwe.

Mbali na hayo kupitia kikao hicho kimewapongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Alli Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku wakitumia nafasi hiyo kumtaka Rais Samia kukubali mialiko kutoka vyama vingine vya upinzani.

“Tunampongeza Rais Samia kwa kuhudhuria mkutano wa baraza la Wanawake wa Chama cha Chadema (BAWACHA) kwani ni kitendo cha kihistoria ambacho hakijawahi kufanywa hapa nchini na ni kitendo cha ujasiri na cha kidemokrasia na ingependeza kama Rais Samia angevitembelea na vyama vingine”alisema Hashim Rungwe

Kwa upande wake Makamo Mwenyekiti Zanzibar Mohammed Masoud Rashid amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kujiunga na CHAUMMA na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi huku akisisitiza kuwa chama hicho kinatoa fursa za kutosha kwa wanawake.

Kikao hicho cha CHAUMMA ni cha kwanza kufanyika tangu kuondolewa kwa katazo la mikutano ya hadhara huku kikiwa na lengo la kujadili hali ya Kisiasa nchini,Suala la Katiba mpya, Kujadili miaka miwili ya utawala wa Rais Samia,Mikutano ya hadhara na mipango mikakati ya chama cha ukombozi wa Umma (CHAUMMA).