Na Allan Vicent,JamhuriMedia,Tabora

Chama cha ACT-Wazalendo kimeshauri Serikali kutunga sheria ya kilimo na kuweka utaratibu wa kodi kama ilivyo katika sekta ya madini ili kuleta tija na ufanisi ikiwemo kuhimiza kilimo cha umwagiliaji.

Ushauri huo umetolewa na kiongozi wa chama hicho Zuberi Zitto Kabwe alipokuwa akiongea na mamia ya wanachama na wapenzi wa chama hicho juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha shule ya msingi Town School mjini Tabora.

Amesema umefika wakati sasa Serikali ikakifanya kilimo kuwa kichocheo kingine kikubwa cha uchumi wa nchi kwa kuweka mikakati na kusimamia kwa dhati utekelezaji mikakati hiyo badala ya kutoa kauli za uhamasishaji tu.

Amesisitiza kuwa kama Serikali inataka kilimo kiwe na tija kubwa kwa wakulima na kuchangia pato la taifa ni haina budi kuachana na kauli mbiu zisizo na tija za kilimo kwanza, kilimo ni uti wa mgongo, uchumi wa kijani, bali itungwe sheria itakayosimamia sekta hiyo kama ilivyo kwenye madini.

Amesema kuwa Serikali inawalaghai wananchi na wakulima kwamba bajeti ya kilimo imeongezeka toka bilioni 202 mwaka 2016-2020 hadi kufikia bilioni 600 mwaka 2021-2023/23 wakati imerejea katika kiwango hicho cha mwaka 2014-2015 bilioni 663.

Zitto amesema kilimo kikisimamiwa ipasavyo kitaleta tija kubwa na kuinua maisha ya wakulima ikiwemo kulifanya taifa kuondokana na umasikini uliokithili na kuongeza kuwa nguvu kubwa ingeelekezwa kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji ili kutotegemea msimu wa mvua tu au jembe la mkono.

‘Watu milioni 14 nchini hawana uhakika wa kupata mlo wa uhakika, wengi hawapati milo mitatu,wanaishi maisha ya kubahatisha na wana umaskini uliokithiri wakati ardhi ipo ya kutosha,wataalamu wapo na serikali ipo, tatizo nini,’ amesema.

Kiongozi huyo amesema miaka 5 iliyopita Serikali ilipata faida shilingi mil.848 kupitia zao la tumbaku iliyazalishwa mkoani Tabora pekee, lakini Mkoa huo bado ni miongoni mwa Mikoa 5 yenye umasikini, hapa kuna tatizo.

Amemtaka Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kufuatilia kampuni zilizoingia mkataba na vyama vya msingi kununua zao hilo na kuhakikisha wanawalipa wakulima fedha zao na ikishindikana kuwapata serikali iwalipe wakulima haki zao.

Awali Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa Haji Duni amesikitishwa na bei za vyakula kuwa juu sana ambapo hata ukiuza kilo 4 za korosho huwezi kununua hata kilo 1 ya mchele.

Duni ameitaka Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuwaondolea kero wananchi kwa kuwa kila mtu anastahili kupata haki sawa na wengine na sio watu wachache wanufaike wakati wengine wanalia.

Aidha ameomba Serikali kuangalia upya suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi kwani halmashauri nyingi hazitoi ipasavyo asilimia 10 ya mikopo kwa vijana,wanawake na walemavu kama ilivyoagizwa.

Naye Makamau Mwenyekiti wa ACT Bara Doroth Semu amesema huduma za afya nchini zinatolewa kwa gharama kubwa, wataalamu ni wachache, madawa hayatoshelezi na vitendea kazi havikidhi mahitaji.

By Jamhuri