Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameshauri serikali kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya usambazaji wa nishati ya gesi asilia majumbani ili kupunguza matumizi ya kuni kwa wakazi wa Lindi na Mtwara.

Chikota akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/24, amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mkoa wa Mtwara tayari nyumba 420 zimeunganishwa nishati hiyo na kwa Mkoa wa Lindi nyumba 209.

“Rais nampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya nishati, lakini naomba fedha ziongezwe kasi iongezeke ili wananchi wa Lindi na Mtwara inufaike na gesi asilia na tupunguze matumizi ya kuni,”amesema.

Aidha, Chikota ameishauri Serikali kuhakikisha wanaishirikisha jamii katika utekelezaji wa mradi wa LNG hatua ambayo itasaidia kuondoa migongano.

“Suala la kushirikisha jamii naomba liendelee, kuna mambo mengi ya kufanya kwa vijana, wanawake, wazaee makundi ya kijamii lazima yajulishwe kuhusu hatua zinazochukuliwa kwenye mradi huu.”

“Matarajio ya wananchi wa maeneo ya mradi husika hawataishi kama wanavyoishi sasa kwa kuwa na maboresho kwenye uwanja wa ndege wa Lindi, barabara za Lindi na Mtwara zinakuwa bora sambamba na huduma za afya, elimu na maji yanafikia mwisho,”alisema.

Mbunge huyo amesema mikakati ya serikali itaiwezesha kuondoa changamoto ya ukatikataji wa umeme kwa kukamilisha mradi wa uzalishaji wa megawati 20 na ule wa kuzalisha megwati 300 unaanza kutekelezwa.

By Jamhuri