Marekani inatarajia kuidhinisha viwango vipya vya ushuru ya bidhaa kutoka China hadi kufikia
dola za Marekani bilioni 60, huku China nayo ikiahidi kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya
bidhaa kutoka Marekani.
Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa, ameliambia Shirika la
Habari la Uingereza (Reuters) kwamba japokuwa nchi yake haijatoa orodha ya bidhaa
ambayo ushuru wake utapanda, lakini ni wazi kuwa jambo hilo liko hatua za mwisho.
Amesema ikiwa China inataka kuizuia Marekani kuchukua hatua inazopanga kuzichukua ya
ongezeko la viwango vya ushuru ya bidhaa zinazoingia Marekani kutoka nchini humo,
inapaswa kufanya kazi ya ziada.
Kwa upande wake, China imesema kuwa iko tayari kukabiliana kwa vitendo na jaribio lolote
kutoka Marekani litakalolenga kuhujumu biashara yoyote inayotoka nchini humo kwenda katika
taifa lolote.
Kutokana na tishio hilo la mgogoro huo wa kibiashara, nchi hiyo tayari imechapisha orodha ya
bidhaa kutoka Marekani ambazo huenda zikaguswa katika mpango wake mpya wa viwango
vya juu vya ushuru.
Katika orodha hiyo bidhaa zilizotajwa ni pamoja na nyama ya nguruwe, matunda, mvinyo
pamoja na bidhaa nyingine zinazoagizwa na wafanyabiashara wa Kichina kutoka Marekani na
kuendelea kuibua maswali mengi.
China imefikia hatua hiyo ya kulipiza kisasi kutokana na mpango wa sheria mpya za kibiashara
uliotiwa saini na Rais Donald Trump hivi karibuni, unaolenga kuziwekea bidhaa za China
viwango vya juu vya kodi.
Balozi wa China nchini Marekani, Cui Tiankai, amesema mgogoro huo hautamsaidia mtu yeyote
na badala yake utaleta madhara makubwa kwa wananchi wa kawaida hasa wafanyabiashara
wa nchi mbili hizo.
Amesema hatua hii inayotarajiwa kuchukuliwa na nchi hizi, haiwezi kuwa na tija wala faida
yoyote zaidi ya kulenga kuwaumiza wananchi wa kawaida wanaonufaika na bidhaa zitokazo
pande zote.
Wakati hali ikiwa hivyo tayari bei za bidhaa za kilimo nchini China zimeanza kupanda, kufuatia
vitisho hivyo vya kibiashara kutoka pande zote mbili.
Tayari Wizara ya uchumi na biashara nchini humo, imeshaonya kuwa huenda ikapitisha
viwango vya juu vya ushuru katika bidhaa za nyama ya nguruwe kutoka Marekani pamoja na
matunda, karanga, mvinyo na mabaki ya mabati.
Kwa hivi sasa masoko yanasubiri kuona ikiwa mgogoro huo wa kibiashara wa kulipiziana kisasi
kati ya China na Marekani, utatanuka na kuzihusisha bidhaa kubwa kama uuzaji wa ndege
kutoka Marekani na bidhaa nyingine.

Please follow and like us:
Pin Share