Na Padre Dk. Faustin Kamugisha

 

Neno la kutia moyo ni siri ya mafanikio. “Neno la kutia moyo kutoka kwa mwalimu linabadilisha maisha ya mwanafunzi. Neno la kutia moyo kutoka kwa mwenza, linaokoa ndoa.” alisema John Maxwell (Kiongozi wa kidini wa Marekani.” Wanafunzi wanahitaji kutiwa moyo ili wafanikiwe.

 

Nathaniel Hawthorne alipopoteza kazi serikalini alirudi nyumbani akiwa na huzuni mkubwa amekata tamaa. Mke wake alipomtazama badala ya kumlalamikia alimpa kalamu na kumwekea wino mezani na kumwashia taa na kumwambia kuwa anaweza kutumia muda huu kuandika kitabu.

 

Jamaa huyo akaandika kitabu kizuri kinachoitwa The Scarlet Letter. Mafanikio ya bwana huyo yalitokana na neno la kutia moyo toka kwa mke wake. Neno la kutia moyo wakati umeshindwa ni bora zaidi ya sifa wakati umefanikiwa.

 

Kuna mtu aliyekuwa akivua samaki katika kisima cha samaki kwa muda wa saa moja. Alikaribia kukata tamaa. Mtoto wa umri wa miaka mitano akamuuliza: umepata samaki wangapi? Mzee huyo akamjibu mtoto huyo: Sijapata samaki hata mmoja. Mtoto akamjibu: Mambo yako si mabaya. Nafahamu mtu aliyevua samaki kwenye kisima hiki kwa muda wa wiki mbili bila kupata chochote kama umevua kwa muda wa saa moja bila kupata chochote si vibaya. Maneno hayo yalimtia moyo huyo mzee akaendelea kuvua mpaka akapata samaki.

 

Jifariji. Jitie moyo, kama mwandishi William Allen White (1868-1944) alivyosema: “Siogopi kesho, kwa vile nimeiona jana na naipenda leo.” Kuna mwanasheria wakili Lord Erskine haikuwa kazi rahisi kwake kuwapa matumizi ya kutosha watoto wake na mke wake. Siku moja alikuwa anatetea kesi iliyovuta nyoyo za watu.

 

Alitoa utetezi mzuri sana. Alizungumza kwa lugha fasaha na kwa akili. Rafiki yake akamuuliza. Uliwezaje kuzungumza vizuri sana namna hiyo. Wakili alijibu: “Niliposimama kuzungumza nilifikiria mtoto wangu akinivuta na kusema dadi zungumza vizuri; unatutengenezea mkate wetu sasa.” Alijitia moyo. Jitie moyo.

 

Unaweza kujitia moyo. Kuna mwanafunzi ambaye alikuwa hapendwi na wenzake. Aliitwa Siima. Hata walimtania kuwa hata kivuli chake hakimpendi hakiko tayari kumfuata. Siku moja alikuwa anaadhimisha Siku yake ya Kuzaliwa. Alijua kuwa hakuna atakayemwandikia kadi ya pongezi. Alifanya kitu fulani.

 

Wenzake walipokuja kumtembelea na kumkejeli walikuta kadi kumi na mbili. Walishangaa. Walipozisoma zilikuwa zote zinatoka kwa mtu mmoja. Kutoka kwa Siima kwenda kwa Siima. Kutiwa moyo na kujipa moyo ni ufunguo wa mlango wa kutoka kwenye jaribu. Kutia moyo ni chakula cha moyo na kila moyo ni moyo wenye njaa.

 

“Neno la ovyo linaweza kuanzisha ugomvi; neno la kikatili liweza kuvunja maisha. Neno kali linaweza kuleta chuki; neno la kinyama linaweza kugonga na kuua. Neno lenye adabu linaweza kusafisha njia; Neno lenye furaha linaweza kutia mwanga katika siku. Neno ambalo linasemwa wakati muafaka linaweza kupunguza msongo wa mawazo; neno la upendo linaweza kuponya na kubariki,” alisema Grenville Kleiser.

 

Kuna Mkenya mmoja aliwashangaza watu kwenye mashindano ya mbio. Alikuwa akiongeza spidi ghafla ghfala. Aliposhinda mwandishi wa habari alimuuliza: kwa nini ulikuwa unaongeza spidi ghafla ghafla? Alijibu: “Nilikuwa nasikia sauti ya mtoto nyumbani inasema: Dad uongeza spidi sina karo.” Unaweza katika maisha kujitia moyo.

By Jamhuri