Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Katibu Mku wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka makatibu wa chama hicho kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa kuhakikisha wanasimamia vizuri mali za chama ili kukifanya chama hicho kuwa na maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akipita mbele ya Vijana wa Chipukizi alipowasili Somangira kwenye hafla ya kuwela jiwe la msingi wa ujenzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Kigamboni

Chongolo ametoa agizo hilo leo Oktoba 22,2022, wakati wa uwekaji wa majiwe ya msingi katika ujenzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Kigamboni pamoja na nyumba ya kuishi Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam inayojengwa wilayani humo.

Amesema kwamba maafisa masuhuli wa chama pamoja na makatibu wanawajibu wakuhakikisha mali za chama zinakua salama hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kulingana na majukumu yake kwenye nafasi aliyo nayo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akisalimiana na Wazee wa mkoa wa Dar Es Salaam wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa nyumba ya Katibu wa CCM mkoa Dar es Salaam

Pia amesema chama kitawachukulia hatua za kisheria wale wote ambao watahusika katika kuhujumu mali za chama kwani chama hicho kina malengo makubwa ya kuwa na miradi mikubwa ambayo itasaidia kukifanya kiwe imara kiuchumi na sio kutegemea wanachama wake kukichangia.

Katibu huyo wa CCM Taifa amesema kuwa kila kiongozi wa chama hususani makatibu ambao ndio watendaji wakuu watapimwa kwa vigezo ambavyo vinaendana na uwajibikaji wao nakwamba ambaye ataonekana kwenda kinyume na misingi ya chama atawajibishwa.

“Dhamana yakuwa katibu sio dhamana bali kuna uwajibikaji nyuma yake,makatibu wote kuanzia ngazi ya tawi,kata,Ward,Wilaya,na Mkoa mimi ndio kiongozi wenu hivyo nawasihi mlinde mali za chama,na moja ya kigezo ambacho kitatumika kuwapima kwenye utendaji wenu ni utekelezaji wa yale yaliyoelekezwa kwenye sehemu ya nafasi yenu ya kazi”amesema.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akiongoza Viongozi wengine wa CCM mkoa wa Dar Es Salaam wakati kukata utepe wakati wa hafla ya kuwela jiwe la msingi wa nyumba ya Katibu wa CCM mkoa wa Dar Es Salaam

Katika hatua nyingine Chongolo amesema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanachama ambao wanatumia rushwa kwa ajili ya kupata uongozi hivyo CCM haitafumbiwa macho nakwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo ya Chongolo imekuja kutokana na hivi karibu uchaguzi wa viongozi ngazi ya wilaya ndani ya chama CCM uligubikwa na vitendo vya rushwa hadi kufikia uamuzi wa baadhi ya uchaguzi katika wilaya zipatazo 21 kufutwa na kurudiwa upya.

“Bado tuna changamoto ya rushwa kwenye chaguzi zetu ndani ya chama,tumemaliza uchaguzi ngazi ya wilaya macho yetu kwa sasa ni uchaguzi wa viongozi ngazi ya mkoa,macho yetu yapo wazi hatutasita kumchukulia hatua mgombea yeyote atakayebainika kutumia rushwa ili apate uongozi”amesema Chongolo.

Amesema kuwa CCM kina watu wasomi,wazuri,viongozi wenye mapenzi ya dhati na chama lakini tatizo ni baadhi yao kutengeneza miundombinu ya haramu ikiwemo rushwa ili kuwadhibiti wasipate dhamana yakuwa viongozi.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Mama Kate Kamba alisema kuwa mkoa wa Dar es salaam upo salama kutokana na ushirikiano wa viongozi wa chama uliopo nakwamba viongozi hao watashirikiana ili kutekeleza vyenma ilani ya chama cha mapinduzi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akifurahia jambo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Kate Kamba wakati wa hafla ya kuwela jiwe la msingi wa nyumba ya Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam.

Naye Katibu Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Dar es Salaam Adam Ngalawa, amesema kuwa ujenzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Kigamboni unagharimu kiasi cha shilingi milioni 28.1 lakini mpaka sasa kiasi kilichotumika ni shilingi milioni 19.7 hivyo kiasi kinachohitajika ili kukamilisha ujenzi huo ni shilingi milioni 9.5 hata hivyo ofisi ya Katibu Mkuu CCM Taifa tayari imechangia shilingi milioni 5 hadi sasa.

Amesema kuwa ujenzi wa nyumba hiyo tayari umefikia hatua ya umaliziaji na kwamba ujenzi umeanza Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Hata hivyo baadhi ya viongozi na wadau mbalimbali wameahidi kuendelea kuchangia ujenzi huo ili kuweza kufanikisha kukamilisha haraka miradi hiyo.

Please follow and like us:
Pin Share