Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mfanyabiashara na mbunge wa zamani wa Jimbo la Igunga mkoani, Tabora Rostam Aziz,amesema kuwa elimu na ujuzi itasaidia kujenga mitaji wa umma wa ndani ili kuwezesha wananchi wa Rais wa Tanzania na Rais Zanzibar na wananchi kufaidika na juhudi zinazofanywa na marais hao katika kuchochea mitaji kutoka nje.

Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano wa kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ulioandaliwa na Maalim Seif Foundation uliofanyika mjini Unguja Rostam ambapo alikuwa akizungumzia mada ya ‘elimu kama msingi wa kukuza uchumi na kuzalisha utajiri wa Taifa.’

Amesema kuwa mitaji kutoka nje ni kichochea cha ukuaji uchumi kwani mitaji hii inaziba la uwezo mdogo wa kuweka akiba tuliyo nayo hivi sasa.

“Uwiano wa uwekaji akiba wa pato wa taifa hapa Tanzania ni wa kiwango cha chini sana yaani ni chini ya asilimia 15 wakati wa uchumi wentu ili tupige hatua tunahitaji angalau kuwa na uwiano wa asilimia 30,” amesema.

Rostam amesema kuwa tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt.Hussein Ally Mwinyi kumekuwa na juhudi kubwa zinazofanywa na marais hao katika kuchochea maendeleo.

Amesema kuwa elimu na ujuzi zitasaidia kujenga mtaji wa umma wa ndani ili kuwezesha wananchi wa Tanzania na Zanzibar kufaidika kwa pamoja katika juhudi zinazofanywa na marais hao.

Amesema kuwa tangu kuingia madarakani kwa viongozi hao Rais Samia na rais Mwinyi wamekuwa mstawi wa mbele kushawisihi mitaji kuingia nchini ambapo katika kipindi cha mwaka mmkoja tangu Machi 2021 hadi Machi 2022 mtaji kutoka nje uliongia nchini uliongeza kwa asilimia 300 kutoka bilioni 1.3 na kufikia bilioni 4.14 za kimarekani.

“Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo yake na Rais William Ruto wa Kenya hivi karibuni, tusipoimarisha uwezo wa watu wetu kushiriki katika uchumi, tutajikuta tunagawana umasikini badala ya kugawana utajiri,” amesema

Amesema kuwa kwa kulitambua hilo, ndiyo maana Rais Samia amejitoa na kujipambanua kuwa mkombozi halisi wa wanyonge na masikini wananchi hii, kwa tafsiri sahihi ya neno hili.

“Mtetezi au mkombozi wa wanyonge si anayepiga piga kelele kusema bali ni yule anayewapa vituo vya afya, kuwajengea shule, kuwajengea masoko, kuwafungulia fursa za biashara na ujasiriamali na kuifungua Tanzania kimataifa ili kuongeza fursa kwa Watanzania.

“Unaiona dhamira yake hasa ya kuwafanya Watanzania wawe wachezaji, na siyo watazamaji tu wa maendeleo ya wengine. Anataka kuona Watanzania kuwa washiriki na siyo waimba mapambio,” amesema Rostam.

Katika kumuenzi Maalim Seif amesema kuwa ni muhimu sana kuwekeza nguvu kubwa katika ubora wa elimu ili kuwaandaa Wazanzibari kwa uchumi ambao yeye Maalim Seif akiamini unapaswa kufikiwa ambao ni wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Kituo cha Biashara na Huduma katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.

Amesema kuwa kwa kuwa Dira ya Maalim Seif na Wazanzibari wengi ni Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika, ni vyema kutazama namna nchi hiyo ilivyoweka nguvu kwenye elimu katika maendeleo yake. Waziri Tharman Shanmugaratnam wa Singapore amenukuliwa katika Kitabu cha The Asian Aspiration akisema “Elimu ndio mkakati wetu muhimu zaidi kiuchumi na kijamii.

Rostam amesema kuwa Maalim Seif, katika uongozi na dira yake, alisisitiza sana umuhimu wa kujenga uwezo wa kielimu kwa Wazanzibari ili kuweza kukabili changamoto za maisha yao, kuleta maendeleo yao na kutenegeneza utajiri katika nchi yao.

“Alikuwa na ndoto ya kuifikisha Zanzibar mahala pakubwa kiuchumi na katika maendeleo ya jamii kwenye eneo letu la ukanda wa Afrika Mashariki na katika Dunia. Kutengeneza ndoto kwa unaowaongoza, na kuwapa hamasa na imani ya kuweza kuifikia ndoto hiyo, ni wajibu mkubwa wa kiuongozi lakini sio viongozi wote wana uwezo huo” amesema.

Amesema kuwa Maalim Seif alitaka kujenga Zanzibar yenye watu wenye elimu na maarifa ya kutosha kuendesha uchumi ambao unatoa huduma kwa eneo lote la Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Bahari ya Hindi.
“Kuiishi dira yake, tunapaswa kujielekeza huko. Hiyo ndio namna bora kabisa ya kumuenzi Mzee wetu huyu.

“Watoto wetu wapate elimu, vijana wetu wapate ajira, mama zetu waweze kuishi maisha bora bila ya kuhangaika na kuteseka na wajasiriamali wetu waweze kutajirika na kutengeneza mitaji ya kuwekeza zaidi,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share