Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Zanzibar
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuleta maridhiano na mageuzi ya uendeshaji wa siasa nchini.
Kinana ameyasema hayo jana wakati akiufunga mkutano wa pili wa kumuenzi Hayati Maalim Seif Sharif Hamad wenye maudhui ya elimu, ukuzaji vipaji, ubunifu na uwezeshaji, uliofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, kisiwani Unguja.
”Hii sio kazi rahisi kwani ziko changamoto zinazotukabili ikiwa ni pamoja na kutofautiana katika utekelezaji wake, kubishana kuhusu vipaumbele vyake na kuwa na mawazo tofauti kwa namna ya kasi ya utekelezaji wake,” amesema.
Kinana aliwataka wanasiasa nchini kuendeleza utamaduni wa kuzungumza, kushauriana na kila mmoja kuheshimu mawazo ya mwenzake licha ya tofauti za kimtazamo na kimkakati.
Amesema Rais Samia ana lengo la kusimamia haki, kukuza na kuimarisha uhuru, kupanua wigo wa kuendesha shughuli za kisiasa na kuleta mageuzi katika uendeshaji wa serikali kwa madhumuni ya kuharakisha maendeleo ya nchi na watu wake.
Pia, Kinana amesema wanasiasa wote kwa pamoja wanapaswa kukubaliana kuhusu mambo muhimu yanayofanywa na Rais Samia kutokana na umuhimu wake kwa nchi na mustakabali wa taifa.
Amesema katika kudhihirisha utayari wake katika kuleta mageuzi ya kweli ya kisiasa nchini, mwaka jana Rais Samia alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kumbukumbu ya Maalim Seif ambapo Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi na Rais Mstaafu Amani Karume walikuwa wageni mashuhuri katika mkutano huo.
Amesema viongozi hao watatu ni viongozi wakuu ndani ya chama hatua ambayo siyo ya kiitifaki bali ni tafsiri ya dhamira ya kweli ya kujenga mazingira mapya ya kisiasa na kijamii nchini.
Akimzungumzia Maalim Seif, Kinana amesema ni kiongozi aliyekuwa na sifa nyingi nzuri zinazomfanya kuwa mtu mwenye maono, msimamo, subira, mpenda haki, mwanamapinduzi na mwenye ushawishi.
Amesema Maalim alipenda kuona vijana wanapata elimu bora iliyolingana na mahitaji ya wakati na yenye kuwajenga vijana kudadisi, kujituma, kujitegemea na kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Aidha,ameamini kwa dhati kuwa elimu ndiyo mkombozi wa kweli kwa mwanadamu ndio maana elimu yake ya msingi na ya juu aliipata kwa kujituma bila kukata tamaa.
Kwa mujibu wa Kinana, ndiyo maana viongozi wa wakati huo waliona na kuthamini kiu ya Maalim Seif jambo lililofanya apewe nafasi ya kuongoza Wizara ya Elimu akiwa na umri mdogo.
“Jukumu hilo lilikuwa zito kwa kuwa fursa za elimu zilikuwa ndogo na hafifu, kwa ujasiri mkubwa na kwa hatua za kuthubutu alijitwisha dhamana ya kufanya kazi aliyopewa kwa ustadi, hasama na ari kubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa, kutokana na juhudi zake vijana wengi wa Zanzibar walipata nafasi za elimu ndani na nje ya nchi, ambapo Maalim aliamini katika elimu, nafasi ya elimu na fursa zinazotolewa na elimu katika maisha ya binadamu na uhai wa taifa.
Ameeleza kuwa, kwa kutambua hayo yote,Tanzania iko katika mchakato wa kutazama upya sera na mfumo wa elimu kwa lengo la kuboresha elimu ili elimu wanayopatiwa watoto ilenge kujenga, kujitegemea na kuendana na mabadiliko na mahitaji ya dunia ya sasa.
Amesema mada zilizojadiliwa katika mkutano huo zimejadili umuhimu wa elimu, sera na namna inavyotakiwa kuikomboa jamii na kuharakisha maendeleo yao hususan katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya teknolojia.