Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam

Benki ya CRDB imesaini makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kwa lengo la kuimarisha uwezo wa taasisi za umma Zanzibar kutumia mali na fursa walizonazo kwa tija, kuvutia mitaji na kuchangia ukuaji wa uchumi baina ya pande mbili

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuweka msingi wa ushirikiano katika kutoa ushauri wa kifedha, kutafuta njia mbadala za upatikanaji wa mitaji, kuboresha ufanisi wa taasisi na kuunganisha taasisi za umma na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo Oktoba 1,2026 wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema ushirikiano huo unaendana na mtazamo wa Tanzania wa kujenga uchumi unaoshindana, endelevu na unaozalisha fursa zaidi kwa wananchi w

Dk. Nsekela amesema taasisi za umma hazipaswi kuangaliwa kama wahitaji wa fedha pekee, bali kama wamiliki wa mali, fursa na miradi inayoweza kutumika kuzalisha thamani na kuchochea maendeleo.

“CRDB imekuwa ikifanya kazi na taasisi za serikali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika miradi mbalimbali ya kimkakati, hivyo makubaliano hayo yanaongeza wigo wa ushirikiano huo wa mlengo wa muda mrefu ni kuona taasisi za umma Zanzibar zikiwa imara kifedha, zikitumia mali zao kwa tija, zikivutia mitaji na kuchangia ongezeko la ajira na mapato ya serikali”amesema Nsekela

Dkt Nsekela amesema CRDB ina uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika kufadhili miradi mbalimbali ya biashara, kilimo, viwanda, miundombinu, nishati na sekta nyingine za kiuchumi, ikiwemo uchumi wa buluu., benki hiyo pia imekuwa ikishirikiana na taasisi za serikali katika kutafuta mitaji ya kuwezesha miradi ya kimkakati na kuimarisha mnyororo wa thamani.

Akitolea mfano mpango wa CRDB wa ufadhili wa miradi inayozingatia mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ambao alisema uliwezesha kupatikana kwa zaidi ya Sh bilioni 171 kwa ajili ya miradi hiyo.

Aidha, alisema CRDB kupitia programu mbalimbali imeweza kukusanya zaidi ya Sh bilioni 325 kwa ajili ya kusaidia uwekezaji na kuwawezesha wakandarasi wazawa.

Dk. Nsekela alisema uzoefu huo utawezesha CRDB kuwa daraja kati ya taasisi za umma Zanzibar, taasisi za fedha, wawekezaji na wadau wengine ili kuhakikisha fursa zilizopo zinageuzwa kuwa miradi yenye manufaa kwa wananchi.

Alisema baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, hatua inayofuata ni kufanya tathmini ya pamoja ya taasisi za umma Zanzibar ili kubaini mahitaji yao ya kifedha, fursa walizonazo na maeneo ambayo yanaweza kuhitaji ushauri wa kitaalamu.

“Safari imeanza. Baada ya kuweka saini leo, kazi inaanza mara moja. Tunahitaji kutengeneza vipaumbele ili tuanze kuona matokeo,” alisema.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Ibrahim Muhammad Sanya, ameshukuru CRDB kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendeleza mpango huo.

Amebainisha kuwa mchakato wa kufikia makubaliano hayo ulianza muda uliopita na umefikia hatua hiyo baada ya pande zote kuona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma Zanzibar na sekta ya fedha.

Waheed amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar inasimamia taasisi mbalimbali za umma, zikiwemo taasisi zinazojihusisha na biashara, elimu, afya na huduma nyingine, hivyo ushirikiano huo utasaidia kutafuta njia bora za kuziimarisha.

“Ni mchakato ulioanza kipindi cha nyuma kidogo, lakini tunashukuru kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu leo tunafikia hatua hii. Tunataka kuona taasisi zetu zikifanya vizuri zaidi,” amesema Waheed

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na CRDB katika kutekeleza makubaliano hayo na kuhakikisha yanazaa matokeo yanayotarajiwa.