Na Mwandishi wa OTR, Arusha
Arusha. Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina, ametoa vipaumbele vitano vya kuleta mageuzi katika Mashirika ya Umma Tanzania, akisema umiliki wa Serikali unapaswa kupimwa kwa thamani ya kiuchumi na kijamii inayozalishwa kupitia mali za umma.
Dk Adesina amesema Tanzania inapaswa kuangalia namna mashirika ya umma yanavyozalisha ajira, uwekezaji, mauzo ya nje, mapato ya Serikali, huduma bora na ubunifu, badala ya kupima tu ukubwa wa mali na uwekezaji unaomilikiwa na Serikali.
“Umiliki siyo mwisho wa safari. Lengo ni kuzalisha thamani,” amesema.
Dk Adesina alitoa kauli hiyo Jumanne, Septemba 27, 2026, alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026) unaofanyika jijini Arusha, ambapo viongozi wa taasisi hizo wanajadili mchango wao katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania na utekelezaji wa Dira 2050.
Amesema kufikia azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kutahitaji mashirika ya umma kuongeza tija, kuimarisha utawala na kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuvutia mitaji binafsi na kuzalisha thamani ya kiuchumi inayoweza kupimika.
Dr Adesina aliongeza kuwa utawala bora unapaswa kuanzia katika kuweka wazi uwajibikaji kati ya Serikali kama mbia, Bodi za Wakurugenzi na menejimenti.
“Mbia anaweka matarajio. Bodi inasimamia. Mkurugenzi Mtendaji anaongoza. Menejimenti inatekeleza. Na Bodi inamuwajibisha Mkurugenzi Mtendaji kwa matokeo,” alisema.
Alizitaka Bodi kutoa mwelekeo wa kimkakati, kusimamia vihatarishi na kuhoji menejimenti kwa njia yenye kujenga, huku viongozi wa menejimenti wakiwa na mamlaka ya kutosha kutekeleza mikakati iliyokubaliwa.
Dk Adesina pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kukuza viongozi, mipango ya kurithishana uongozi na mifumo ya taasisi, akisema mashirika ya umma hayapaswi kutegemea viongozi binafsi kupita kiasi.
Alisema taasisi imara zinahitaji mifumo, uwezo wa menejimenti na utamaduni wa taasisi unaoweza kuendeleza utendaji hata pale uongozi unapobadilika.
Alieleza pia umuhimu wa kuongeza tija ya mitaji na mali za umma, akisema kila shilingi inayowekezwa na Serikali inapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia fursa za kiuchumi inazozalisha, zikiwemo ongezeko la tija, ajira, mauzo ya nje, mapato, uwezo na uwekezaji binafsi.
“Kila shilingi inayowekezwa na Serikali ni fursa,” alisema.
Katika suala hilo, Dk Adesina aliutaja Mfuko wa Uwekezaji wa Umma kuwa unaweza kuwa nyenzo muhimu katika hatua inayofuata ya mageuzi ya mashirika ya umma, akisema unapaswa kuelekeza mitaji katika taasisi zenye uwezo wa kukua, zikiwa na mipango ya wazi ya maboresho na malengo yanayoweza kupimika.
“Mtaji unapaswa kuambatana na mageuzi. Uwekezaji unapaswa kuambatana na uwajibikaji,” alisema.
Alisema mfuko huo nao unapaswa kupimwa kwa thamani inayozalisha, mitaji binafsi inayovutia, maboresho ya tija, ajira endelevu na faida inayopatikana.
Dk Adesina pia aliitaka Tanzania kupanua ushiriki katika mashirika ya umma imara kupitia wawekezaji wa kimkakati, ubia na, pale inapofaa, kuorodheshwa katika soko la hisa.
Hata hivyo, alisema kuorodheshwa katika soko la hisa kunapaswa kuja baada ya kampuni kuwa na utawala imara, kuwa na menejimenti yenye uwezo, taarifa za fedha zinazoaminika, mifumo imara ya udhibiti na mfumo wa biashara unaoweza kushindana.
“Kampuni imara inapaswa kutangulia kabla ya kuingia kwenye soko la hisa,” alisema.
Alisema kuorodheshwa katika soko la hisa kunaweza pia kuwapa watanzania, mifuko ya pensheni na wawekezaji wa kitaasisi fursa ya kushiriki katika ukuaji wa mali za Taifa zinazozalisha.
Mtazamo wa Dk Adesina umeungwa mkono na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliyesema faida na gawio pekee haviwezi kuwa kipimo pekee cha mchango wa taasisi zote za umma.
Alisema baadhi ya taasisi zimeanzishwa mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma muhimu, kusimamia viwango, kulinda usalama wa umma na maslahi ya wananchi, pamoja na kujenga uwezo wa Taifa.
Alisema tathmini ya utendaji inapaswa pia kuzingatia maboresho ya huduma, kupungua kwa gharama kwa wananchi na Serikali, kuongezeka kwa ufanisi na kiwango ambacho taasisi zinashughulikia changamoto ambazo hapo awali zilihitaji Tanzania kutafuta huduma nje ya nchi.
“Kwa taasisi za kibiashara, tunaangalia tija, uimara wa kifedha, faida na mchango kwa Serikali,” alisema.
“Kwa taasisi zenye majukumu ya huduma kwa umma, tunaangalia pia maisha yaliyookolewa, wananchi waliofikiwa, ubora na upatikanaji wa huduma, muda na gharama zilizopunguzwa,”
Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026), unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ulifunguliwa jijini Arusha Septemba 28, 2026, na unatarajiwa kufungwa Septemba 30, ukiwa na kaulimbiu “Mashirika ya Umma yenye Ufanisi wa juu kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050.”







