Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Nzega

Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela daktari wa hospitali ya Mji Mdogo wa Nzega Daudi Hashim Msokwa (29) kwa kosa la kumwomba rushwa mgonjwa aliyekuwa akitibiwa hospitalini hapo.

Awali Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani hapa Mazengo Joseph akishirikiana na mwenzake Shabani Mntambo waliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Aprili 16 mwaka huu katika hospitali hiyo.

Alisema kuwa mtuhumiwa ambaye ni Mtumishi wa Serikali aliomba rushwa ya kiasi cha sh. 150,000 kwa Christina Aloyce (39) mkazi wa Mjini Nzega ambaye alikuwa amemleta ndugu yake Gaudensia Eugene (25) katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu na kufanyiwa oparesheni.

Mazengo alisema mtuhumiwa aliomba kiasi hicho kutoka kwa ndugu wa mgonjwa huyo ili amruhusu kuondoka hospitalini hapo baada ya kumfanyia oparesheni.

Alibainisha kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1)(a),(2),(3)(a) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Baada ya kusomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya hiyo Saturin Condrad Mushi, mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo huku akiahidi kuwa hatarudia tena kuomba rushwa.

Baada ya kukiri kosa hilo, Mwendesha Mashtaka Mazengo Joseph aliiambia Mahakama kuwa upande wa Jamhuri hawaoni sababu ya kupeleka mashahidi mahakamani kwa kuwa mshitakiwa amekiri mwenyewe.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Saturin Condrad Mushi alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri mwenyewe shitaka lake mbele ya mahakama, hivyo mahakama inamtia hatiani.

Albainisha kuwa, kwa kuwa vitendo vya rushwa vimekuwa vikiharibu utendaji wa serikali, mahakama inamhukumu kutumikia kifungo cha miaka 2 jela au kulipa faini ya sh. 500,000 (laki tano) ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo, mshitakiwa alilipa faini na kuachiwa huru.

Please follow and like us:
Pin Share