Na Mwandishi Maalumu, Kampala

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amewaasa vijana wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa chachu ya utengamano katika Jumuiya hiyo kwa hatua zilizobakia za Umoja wa Kifedha na Shirikisho la Kisiasa.

Ameyasema hayo katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.

Mkutano huo uliojadili umuhimu na nafasi ya viongozi waliopo madarakani kuandaa viongozi wanaochipukia ulihudhuriwa na zaidi ya marais na viongozi wa sasa na waliowahi kuwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya nchini Uganda zaidi ya 1,000.

Makamu wa Rais wa Uganda, Bi. Jessica Allupo na Waziri Mkuu Mstaafu wa nchi hiyo Ruhakana Rugunda pia walishiriki katika mkutano huo uliofanyikia katika Chuo Kikuu maarufu cha Makerere, Kampala nchini Uganda.

Pamoja na mambo mengine, washiriki wa mkutano huo, ambao wengi ni vijana, walijadili kwa kina na uwazi fursa, changamoto na matamanio yao kama vijana ambai tayari wameonesha uwezo wa kuongoza na namna serikali na jamii ya Uganda inavyoweza kuwatumia katika nafasi mbalimbali za kiongozi serikalini, kwenye mashirika mbalimbali na kwenye jamii kwa ujumla.

Aidha, suala la kufanya siasa za vyama ndani ya vyuo vikuu lilijadiliwa kwa kirefu ambapo washiriki walitofautiana maoni ambapo wapo walioona kuwa ushiriki kwenye siasa za vyama kwa wanafunzi waliopo vyuoni ni jambo la msingi katika kutetea maslahi ya wanafunzi na kuwaandaa wanafunzi kuwa viongozi na wanasiasa wazuri wa siku za usoni, huku wengine wakieleza mtizamo wao kuwa mwanafunzi makini anaweza kuwa kiongozi katika nafasi mbalimbali kwenye jamii bioa ya kufungamana na vyana vya siasa.

Waliounga mkono hoja hii walieleza kuwa, siasa vya vyama zinaweza kufungamanisha na kufunga mawazo mazuri ya kimaendeleo aliyonayo mwanafunzi kwa ajenda za kiasiasa za chama cha siasa ambacho ni mwanachama na kumfanya kutoona maeneo mengine kwenye jamii ambayo anaweza kuonesha uwezo wake wa kiuongozi.

Kwa upande wake Rais Mstaafu Kikwete aliwapa uzoefu wake katika siasa za vyuo vikuu alipokuwa Rais Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1973 na namna alivyojifunza kipindi hiko umuhimu wa viongozi vijana kuwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati.

Akawaasa viongozi hao kujifunza kujenga hoja za nguvu ya kufanya mabadiliko katika mambo wanayoyataka na kujiepusha na kishawishi cha kulazimisha jambo ambalo wakati wake bado haujafika au kwa kukiuka taratibu ambazo zimewekwa kwa makubaliano ya pamoja.

Akaongeza kuwa kijana yoyote, si lazima awe kiongozi, ana uwezo wa kutumia vyema kipaji chake, uwezo wake wa kufikiri na nguvu alizonazo kupaza sauti itakayoleta mabadiliko katika jamii na taifa lake kwa ujumla.

Aidha, kwa nafasi yake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Kikwete alieleza kuvutiwa kwake na ubunifu wa mkutano huo kwa kuwakutanisha viongozi wa sasa na wa zamani wa vyuo vikuu pamoja na viongozi wa serikali kwani unatoa fursa ya kujadili na kulinganisha hatua zilizofikiwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ambayo serikali za wanafunzi zimekuwa zikiyafuatilia kwa nyakati tofauti.

Vilevile, alishauri kuwa itakua jambo la busara kwa mkutano huo sasa kuandaliwa katika ngazi ya vyuo vyote kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuwa jukwaa jingine la vijana kijadili masuala ya jumuiya na kuwa chachu ya kuharakisha jitihada za utenganamano wa kikanda katika nchi za EAC.

Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Jopo la Wazee la Jumuiya ya Maendelo Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Mstaafu Dkt. Kikwete alitumia fursa ya kuwa Uganda kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na usalama katika ukanda wa maziwa makuu na kusini mwa afrika.

Makamu wa Rais wa Uganda, Bi. Jessica Allupo  akifuatilia hotuba ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akifurahia jambo kabla ya kuhutubia katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi jana Jumatatu.
Wahudhuriaji katika katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.
Please follow and like us:
Pin Share