*Barabara ya Segerea, Tabata hadi mzunguko wa Kigogo nayo imo

Dar es Salaam

Na Joe Nakajumo

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DAR RAPID TRANSIT – DART) ni taasisi ya serikali chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) yenye jukumu la kupunguza adha katika usafiri wa umma Dar es Salaam.

Januari 21, mwaka huu, DART iliandaa warsha ya siku moja kwa wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tanzania Editors’ Forum) kujadiliana kuhusu majukumu ya Wakala.

Mwandishi wa makala hii, Joe Nakajumo, aliyeshiriki kwenye warsha anaeleza hatua za utekelezaji zinavyoendelea. 

Idadi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam inaongezeka kila mwaka na kwa kutambua hilo, serikali mwaka 2002 iliamua kutafuta ufumbuzi wa tatizo la usafiri katika jiji.

Kwa takwimu za Sensa ya Taifa iliyofanyika 2012, Dar es Salaam ilikuwa na wakazi milioni 4.365. Sensa ya Taifa nchini hufanyika kila baada ya miaka 10, hivyo Agosti mwaka huu itafanyika tena.

Kuna kila dalili inayoashiria kwamba idadi ya wakazi wa Dar es Salaam itaongezeka na kufikia milioni sita itakapofanyika sensa.

Ili kutekeleza azima yake ya kulipatia ufumbuzi tatizo na kuleta mageuzi ya usafiri wa umma Dar es Salaam, serikali mwaka 2007 iliwapa kazi wataalamu wa Bus Rapid Transport (BRT) kutoka Marekani ya Kusini (Latin America) kufanya utafiti.

Wataalamu baadhi kutoka Brazil walikuja na ushauri kwamba uanzishwe mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) utakaotekelezwa kwa awamu sita kwa kujenga miundombinu ya barabara.

Serikali ilianza utekelezaji wa ushauri wa wataalamu kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa awamu ya kwanza.

Taasisi maalumu ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndiyo yenye jukumu la kusimamia mradi wa mabasi yaendayo haraka.

DART ilianza ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza Agosti 2010 ukiwa wa kilomita 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni. Awamu hiyo ni pamoja na kutoka Magomeni – Barabara ya Kawawa hadi Morocco. Pia kutoka Kituo Kikuu cha Zimamoto (Fire), Barabara ya Msimbazi hadi Gerezani, Kariakoo.

Usafiri wa haraka waanza

Mradi wa Awamu ya Kwanza ulikabidhiwa kwa serikali Februari 2016 na kuanza kazi Mei 16, mwaka huo.

Gharama za ujenzi wa Awamu ya Kwanza zilikuwa ni Sh bilioni 385. Mradi ulianza na mabasi 140 na idadi ya abiria imeongezeka kutoka 76,000 huduma ilipoanza miaka sita iliyopita hadi kufikia  200,000 kwa siku hivi sasa.

Watendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Dk. Edwin Mhede, akifungua warsha, amesema wanufaika wakubwa wa mradi wa mabasi yaendayo haraka ni wananchi wa kawaida.

Mafanikio yanaonekana

Dk. Mhede anasema kwa kiasi fulani huduma za mabasi yaendayo haraka zimewapunguzia adha ya usafiri wa kwenda na kurudi kwenye shughuli zao za kila siku.

Moja ya mafanikio katika Awamu hii ya kwanza ni kwa wananchi kutumia muda mfupi wanapotumia mabasi yaendayo haraka, kwa mfano anayesafiri kutoka Kimara hadi Kivukoni anatumia wastani wa dakika 45 badala ya saa mbili hadi tatu.

DART katika warsha ilieleza kwamba utekelezaji wa Awamu ya Pili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ya urefu wa kilomita 20.3 kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi katikati ya jiji na kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani hadi Magomeni kwa kupitia Chang’ombe, Keko na kuingia Barabara ya Kawawa hadi Magomeni unaendelea kwa gharama ya dola za Marekani milioni 141.7 ambazo ni sawa na Sh bilioni 327.3 kwa kiwango cha thamani ya dola ya Marekani Januari 24, 2022 siku makala hii ilipoandikwa.

Kazi ya miundombinu imepangwa kukamilika mwaka 2023 ambapo huduma za mabasi yaendayo haraka zitaanza.

Mkataba Awamu ya Tatu

Kwa mujibu wa maelezo ya watendaji kwenye warsha, Awamu ya Tatu ni ujenzi wa miundombinu ya kilomita 23.6 kutoka katikati ya jiji kwenda Gongo la Mboto kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 148.2 ambazo ni sawa na Sh bilioni 342.3. Mkataba wa ujenzi wa awamu hii utasainiwa wakati wowote mwezi huu.

Awamu ya nne ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka wenye kilomita 26 itaanzia Maktaba Kuu ya Taifa, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda Tegeta hadi Dawasa, eneo la Boko.

Awamu hii pia itajumuisha barabara kutoka Mwenge hadi Daraja la Kijazi, Ubungo.

Kiasi cha gharama kwa awamu hii ni dola za Marekani milioni 98 ambazo ni sawa na Sh bilioni 226.3.

DART imesema fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili, ya Tatu na ya Nne zimeshatolewa na Benki ya Dunia (WB).

Awamu ya Tano itaanzia Ubungo katika Barabara ya Mandela hadi Daraja la Nyerere kwenda Kigamboni.

Imeelezwa kwamba usanifu kwa utekelezaji wa Awamu ya Tano wa kilomita 27.6 umekamilika na mfadhili ni Serikali ya Ufaransa ambayo itatoa Euro milioni 178 ambazo ni sawa na Sh bilioni 465.

DART

 Katika warsha hiyo inasema Awamu ya Sita inahusisha Barabara ya Mwai Kibaki inayopitia vituo vya Kisiwani Mikocheni, Chama, Kwa Mwalimu Nyerere, Kwa Warioba, Kawe hadi Lugalo ambako itaungana na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Hata hivyo, bado upembuzi yakinifu haujafanyika na fedha za ujenzi hazijapatikana. 

Tabata na Kigogo kunufaika

Katika mtandao huo wa Mabasi Yaendayo Haraka kutakuwa na barabara mpya kutoka Tabata Segerea hadi mzunguko wa Kigogo katika Barabara ya Kawawa.

DART imesema awamu zote sita zinatakiwa ziwe zimekamilika ifikapo mwaka wa fedha wa 2025/26.

Huduma hadi Kibaha na Vikindu

DART imesema katika mipango ya baadaye kutakuwa na upanuzi wa barabara kutoka Kimara kwenda Kibaha kwa kuweka njia na vituo maalumu.

Kadhalika utafanyika upanuzi kutoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Vikindu katika Barabara ya Kilwa.

Kwa awamu zote sita zitakapokamilika kutakuwa na kilomita 154.6.

Kwa sasa kuna jumla ya mabasi 210 yanayotoa huduma zinazoendeshwa na UDART kwa ubia wa taasisi mbili; serikali ikimiliki asilimia 49 na binafsi asilimia 51.

Wamiliki daladala wakaribishwa

DART imo katika mchakato wa kumpata mtoa huduma wa ziada, mmiliki wa mabasi 65 katika mtandao wake wa barabara ili kuimarisha huduma kwa wananchi.

Aidha, imewataka wamiliki wa daladala kuungana na kuunda taasisi moja ili kutoa huduma katika barabara za mabasi yaendayo haraka kwa kuwa fursa hiyo ipo kwa wawekezaji binafsi. 

Katika Bara la Afrika kuna nchi tatu; Tanzania, Afrika Kusini na Nigeria zinazotoa huduma za mabasi yaendayo haraka.

DART yang’ara kimataifa

Januari 9, 2018, DART ikiwa na miaka miwili tangu ilipoanza kutoa huduma za mabasi yaendayo haraka, ilipokea Tuzo ya usafiri endelevu jijini Washington, Marekani, kuitambua Dar es Salaam kama jiji la kwanza barani Afrika katika kipindi cha miaka 13 iliyopita kwa kufanya mageuzi makubwa katika usafiri wa umma kwa kutumia mfumo wa BRT (Bus Rapid Transport) kwa kujenga miundombinu kwa vigezo vya kimataifa.

Kufuatia utendaji bora na wenye ufanisi, wakala wa DART umekuwa ukipokea wajumbe kutoka nchi mbalimbali wanaokuja kujifunza namna mradi wa mabasi yaendayo haraka unavyoendeshwa na kufanya kazi kwa ufanisi.

Nchi ambazo zimekwisha kutuma maofisa wake kuja Tanzania kujifunza ni pamoja na Kenya, Rwanda, Senegal na maseneta wa Ufaransa.

Mwandishi wa makala hii, JOE NAKAJUMO, ni mhariri na mwanahabari mwandamizi ambaye kwa sasa ni mjumbe wa TEF. Anapatikana kwa simu namba 0784 291 434.

By Jamhuri