Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Kuna mstari mwembamba umepita katika kutenganisha jina la Edna Lema na majina ya makocha wengine wa soka la wanawake nchini. Kimuonekano ni mstari mdogo.

Ni mstari mdogo wenye changamoto. Ukiutazama juu juu unaweza kuuona ni kama mstari wa kawaida na kila mmoja wetu anaweza kuuvuka kwa urahisi akaenda zake.

Edna ni kocha anayeujua mpira kwa kuuzungumzia, kuucheza na kuufundisha. Tuna namba ndogo ya watu wa hivi katika soka letu. Kufundisha, kuucheza na kuuelezea.

Hatuwezi kuuzungumzia mpira wa wanawake nchini bila kutaja jina la huyu dada wa Kichaga. Ameanza kuutumikia mpira katika ngazi zote. Kuucheza, kuusomea. Sasa ni kocha. Hongera nyingi kwake.

Historia ina tabia ya kuwakumbuka mashujaa. Edna ni shujaa wa mpira wa wanawake Tanzania.  Alikuwapo kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’. Miaka 20 iliyopita.

Edna alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya wanawake kilichotwaa Kombe la CECAFA kwa mara ya kwanza akiwa kocha msaidizi. Iwe mafanikio, iwe changamoto za mpira wa wanawake huwezi kukwepa jina la Edna kwa namna yoyote ile.

Edna ndiye kocha mwenye leseni kubwa kwa Tanzania Bara kwa upande wa kina mama. Ana leseni B. Hii ni leseni ambayo hata wanaume wengi wanaitafuta. Edna anayo leseni hii miaka sita sasa. Iko kabatini inakula vumbi tu.

Licha ya kuwa na leseni hiyo, lakini amewahi kwenda Ujerumani ‘kupigwa msasa’. Miongoni mwa makocha aliokuwa nao darasani huko Ujerumani ni kocha wa sasa wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann. 

Imeanza kuniudhi. Naona inatokea sana siku hizi. Edna anadharauliwa. Kibaya zaidi wanaofanya hivi hawajui hata A, B, C za mpira. Wanapayuka tu.

Lakini naelewa kwa nini iko hivi. Edna hajaweka ‘gate’ mbele yake. Anazungumza na kucheka na kila mtu. Anayemjua na asiyemjua. Hii ni nzuri, lakini pia ni mbaya. Si kila anayependa kucheka na wewe anakupenda. Tunacheka na watu wengi kinafiki.

Edna huwezi kumbadili. Anapenda kukaa na kila mtu. Amewasogeza watu katika maisha yake. Mwanafalsafa mmoja wa Kigiriki aliwahi kusema usimuamini kila mtu, lakini usimsikilize kila mtu.

Mwanafalsafa yule aliyeagana na uso wa dunia hivi sasa aliwalenga watu aina ya Edna. Tumechagua kumchukulia poa kwa kuwa Edna ni rafiki yetu sana. Edna hajatuwekea uzio ndiyo maana tunambeza.

Tunambeza na kumpuuza, lakini kwa maana ya kufundisha, Edna ni kocha kweli. Amewazidi makocha wengi wa kike nchini. Amewazidi vitu vingi. Amewazidi uzoefu, elimu ya mpira. Huyu ndiye kocha wetu bora kwa wanawake. 

Hakuna namna ambayo tunaweza kuukana ukweli huu. Tumkubali japo kwa unafiki.

Changamoto zake kama binadamu haziwezi kuondoa uwezo alionao katika soka. Katika suala la kufundisha soka Edna ni mwalimu mahiri.

Baada ya kuacha mpira na kuhamia katika kuusomea na baadaye kuufundisha hakuwahi kufundisha timu za klabu. Alikuwa kocha msaidizi wa timu zote za taifa. 

Lakini kwa sasa Edna anaifundisha Yanga. Si kazi rahisi kwa mwanamke kuishi kwenye presha ya timu kubwa. Mpaka sasa Simba juu ya umwamba wao hawajawahi kumuamini kocha mwanamke kumpa timu yao ya wanawake.

Unadhani Simba hawatamani kuwa na kocha mwanamke wa ndani? Wanatamani sana, lakini sokoni hakuna kocha mwenye daraja la Edna. 

Ndiyo maana wameamua kuwapa timu yao makocha wa kiume, lakini haina maana kuwa hakuna makocha wa kike nchini. Wengi wao ndio wako shuleni hivi sasa.

Edna hajalala na kuamka akawa kocha wa viwango vile. Ametengenezwa na kujitengeneza. Amepitia aliyopitia na bado ana nafasi ya kuendelea kufanya vizuri kuanzia ndani hadi nje.

Edna ana mengi ya kufanya Yanga na timu zetu za taifa. Ni suala la muda tu kutuonyesha hicho kilichomo ndani yake. Mwalimu mzuri ni yule anayechukua changamoto na kuanza kuyatafuta mafanikio na kusonga mbele. Ni suala la muda tu.

By Jamhuri