Dar es Salaam

Na Mwalimu Samson Sombi

Mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa Afrika bado unaendelea kupita katika milima na mabonde tangu kurejeshwa miaka ya 1990.

Demokrasia ni uhuru wenye mipaka na sheria wa serikali iliyowekwa madarakani na wananchi kwa ajili ya masilahi yao mapana.

Katika nchi ya kidemokrasia, wananchi hushiriki katika kupanga, kuamua, kusimamia na kutekeleza mipango yote ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa taifa lao.

Baada ya nchi zote za Afrika kupata uhuru na kuanza kujitawala, yale matumaini makubwa ya wananchi kufurahia uhuru na utawala wa viongozi wa Kiafrika yakakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uchu wa madaraka kwa baadhi ya watawala na vyama vyao vya siasa.

Lengo na madhumuni ya mfumo wa vyama vingi nikupanua, kudumisha na kulinda demokrasia ambayo ni msingi katika uongozi unaozingatia haki na usawa wa binadamu.

Uchaguzi wa ngazi mbalimbali huendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya nchi husika.

Tume ya uchaguzi ndiyo chombo chenye mamlaka ya kupanga, kuendesha na kusimamia shughuli zote za uchaguzi kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho; kutangaza matokeo.

Kwa miaka mingi sasa kumekuwa na malalamiko ya wananchi juu ya utendaji kazi wa tume za uchaguzi katika baadhi ya nchi, zikidaiwa kutotenda haki.

Tume nyingi zimeonekana kupendelea vyama tawala katika kutangaza matokeo.

Baadhi ya viongozi wa vyama tawala hutumia vyombo vya dola na wajumbe wa tume katika harakati za kuhakikisha ushindi na kuendelea kubaki madarakani hata bila ridhaa ya wananchi ambao ndio wapiga kura.

Hata hivyo, kadiri miaka inavyosonga mbele, mfumo wa vyama vingi umeanza kuzaa matunda kwa baadhi ya nchi kuviondoa

Madarakani vyama tawala kwa kupitia njia ya demokrasia ya sanduku la kura.

Kwa sasa ni vyama vichache sana vilivyopigania uhuru ambavyo bado vinaendelea kutawala.

Pamoja na vyama hivyo vikongwe kuendelea kushika dola, vinakumbana na changamoto nyingi kutokana na mwamko wa kisiasa Afrika.

Pamoja na mwamko huo bado viongozi wa upinzani na vyama vyao wanapaswa kuwa na  siasa za uvumilivu na kishawishi kikubwa cha kisiasa kwa wapiga kura.

Baada ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuendelea kuzaa matunda katika nchi nyingi za Afrika Magharibi, Zambia imekuwa kinara wa kubadilishana uongozi kupitia uchaguzi.

Mwaka 2021 ulikuwa wa kicheko kwa wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zambia baada ya mgombea wao kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliofanyikaAgosti 12.

Uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali kati ya Rais Edgar Lungu aliyekuwa madarakani wa  PF dhidi ya Haikande Hichilema wa UPND.

Katika majimbo 155 kati ya 156 ambayo matokeo yalitangazwa Agosti 16 mwaka jana, Hichilema alipata jumla ya kura 2,810,757 wakati Rais Lungu akipata kura 1,814,201.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), Jaji Esau Chulu, alimtangaza Haikande Hichilema kupitia televisheni ya taifa kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Zambia.

Ushindi wa Hichilema ulihitimisha miaka sita ya utawala wa Lungu aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza Januari 25, 2015 katika uchaguzi mdogo ili kukamilisha muhula wa Rais Michael Sata aliyefariki dunia Oktoba 28, 2014.

Agosti 2016, Zambia ilifanya uchaguzi mwingine wa kikatiba na Lungu akachaguliwa tena kuwa Rais kwa muhula wake wa kwanza, kwa ushindi mwembamba dhidi ya Hichilema.

Hii si mara ya kwanza Zambia kufanya mageuzi ya kisiasa kwani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1991, Baba wa Taifa hilo, Kenneth Kaunda, na Chama chake cha UNIP aliondolewa madarakani na Chama cha MMD kilichoongozwa na Fredrick Chiluba.

Baada ya Chiluba aliyekuwa Makamu wa Rais, Levy Mwanawasa, aligombea na kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2001.

Alitumikia wadhifa huo hadi alipofariki dunia Agosti 2008 na kiti chake kurithiwa na Rupiah Banda.

Katika uchaguzi wa Septemba 20, 2011, Michael Sata alichaguliwa kuwa Rais wa tano wa Zambia. 

Hata hivyo alifariki dunia Oktoba 28, 2014 na Guy Scott akawa Kaimu Rais mpaka Lungu wa PF aliposhinda uchaguzi mdogo wa Januari 2015.

Ijumaa ya Agosti 24 mwaka jana, Rais Hichilema aliapishwa kushika wadhifa huo huku akiahidi kufanya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili nchi hiyo ipige hatua katika maendeleo. 

Rais Hichilema aliyewania urais kwa mara ya sita, ameahidi kasi katika kukuza uchumi, kutengeneza ajira na kutofanya siasa za ukandamizaji wa haki.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika viwanja vya Lusaka, Hichilema alisema ushindi alioupata si wake bali ni wa wananchi wote wa Zambia, hasa vijana waliojitokeza kwa wingi kupiga kura.

Alisema wameonyesha dunia uthabiti wa demokrasia yao na  wamethibitisha kwamba madaraka yanatoka kwa wananchi na sasa wameamua kufanya mabadiliko.

“Njia mbele yetu haiwezikuwa bila changamoto lakini kwa dira na mipango tuliyonayo tutafanikiwa na kutimiza matarajio yetu kutoka kwetu,” alisema Hichilema huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria katika uwanja huo.

Rais Hichilema aliwahakikishia kwamba serikali yake itakwenda kutengeneza fursa za ajira kwa ajili ya vijana wasio na ajira na kurudisha mazingira bora ya wananchi wote kwenye familia zao kama ilivyokuwa zamani.

Kiongozi huyo wa nchi alisisitiza kwamba wanakwenda kuweka vizuri mazingira ya uwekezaji nchini humo na kwamba wamejipanga vizuri kuwatumikia na kujenga uchumi wao upya kwa sababu sasa wamekuwa taifa jipya.

“Hatutayachukulia majukumu haya kwa wepesi, tutawatumikia kwa ukamilifu kama watumishiwenu na si kama watawala, hiyo ni ahadiyetu kwenu,” alisema Rais Hichilema.

Tutakuza uchumi wetu ili tusiwaache wenzetu kwenye umaskini kuliko wakati mwingine wowote. Tutalinda haki, uhuru na demokrasia. Tutadumisha utawala wa sheria na kuirudisha nchi yetu katika haliyake,” alisema.

Rais Hichilema ameahidi kufanya siasa za haki bila kuwaonea wapinzani kama alivyofanyiwa yeye wakati wa utawala wa Edgar Lungu.

Aidha, amewataka wafuasi wake wasilipe kisasi kwa waliyotendewa bali washirikiane kuinua uchumi wa Zambia.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na marais mbalimbali akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. Rais mstaafu wa nchi hiyo, Edgar Lungu, alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria tukio la kuapishwa kwa Rais Hichilema na kuahidi kumuunga mkono katika uongozi wake.

Kitendo cha Rais mstaafu Lungu kuhudhuria hafla hiyo kimeonyesha kukua na kukomaa kwa demokrasia nchini humo.

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, aliwahi kusema kuwa siasa si uadui na kwamba wapinzani wa kisiasa si maadui katika ujenzi wa taifa.

Demokrasia ya vyama vingi vya siasa ni kwa ajili ya masilahi na ustawi wa wananchi na si tamaa na uchu wa madaraka kama inavyofikiriwa na wanasiasa wengi.

0755-985966

By Jamhuri