*Wapinzani sasa waweka masharti

*Mwakilishi UN amtembelea Sambi

NA MWANDISHI WETU

Utawala wa Rais Azali Assoumani wa Muungano wa Visiwa vya Comoro unazidi kubanwa kutokana na hatua yake ya kumweka kizuizini Rais mstaafu wa nchi hiyo, Ahmed Mohamed Sambi.

Sambi amezuiwa kizuizini kwa takriban miaka minne sasa akiwa amezuiwa katakata kuonana na mkewe na watoto wake kwa muda wote huo.

Wiki iliyopita, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) katika Visiwa vya Comoro, Francois Batalinganya, alipata kibali cha kumuona Rais Sambi kizuizini alikowekwa.

Taarifa zinasema baadaye kiongozi huyo alionana na Rais Azali, dhamira kuu ikiwa kumsihi amwachie huru kiongozi huyo anayeheshimika mno ndani na nje ya Comoro.

Lakini ombi jingine lilikuwa kumuomba Rais Azali amruhusu ‘mfungwa huyo wa kisiasa’ aweze kwenda nje ya Comoro kupatiwa matibabu.

Watu waliokuwa karibu wakati Batalinganya anakwenda kumjulia hali Sambi, wanasema gari lake lilizuiwa kuingia, hivyo akalazimika kuliacha nje.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kuomba kumuona Sambi. Mara ya kwanza licha ya kukubaliwa, baadaye alizuiwa kumuona.

Kwa miaka mitatu sasa, Rais Sambi anaomba akatibiwe, na ombi lake lilishakubaliwa na mamlaka za Comoro kabla ya Rais Azali kuagiza ruhusa hiyo ifutwe licha ya kwamba alishapata hadi tiketi ya Shirika la Ndege la Kenya. Sambi alikuwa afike Dar es Salaam kutibiwa baada ya Rais wa wakati huo, Dk. John Magufuli, kukubali kugharimia matibabu yake.

Rais Azali ameendelea kuwa na msimamo mkali dhidi ya Sambi kwani Agosti 23, mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan alimtuma Rais mstaafu Jakaya Kikwete ampelekee salamu zilizohusu hatima ya Rais Sambi, lakini duru za habari kutoka pande zote zinaonyesha kuwa kiongozi huyo hadi mwezi uliopita alikuwa hajaonyesha dalili za kukubali maombi ya Rais Samia.

Hayo yakiendelea, vyama vya siasa nchini Comoro vimepinga mpango wowote wa kuwa na mkutano wa upatanishi na Rais Azali, kwa shinikizo kwamba hilo litawezekana tu endapo atakuwa amemwachia huru Sambi.

Joto la kisiasa linazidi kupanda huku Rais Azali mara kadhaa hata akiwa maeneo ya ibada amekuwa akizongwa na wakati mwingine kuzomewa kama ishara ya hasira za wazi za baadhi ya wana Comoro wanaopinga Sambi kuteswa kizuizini.

Wananchi wanaompinga Rais Azali wanasema yuko madarakani kinyume cha Katiba ya Comoro, na kwamba mwisho wa utawala wake ulikuwa mwaka jana, lakini amepuuza katiba na kuendelea kushikilia madaraka.

Wakosoaji walioketi Desemba 4, mwaka jana walisema endapo Rais Azali anataka maridhiano ya kitaifa kama anavyoonyesha sasa, pamoja na kumwachia Sambi, sharti awaachie wafungwa wengine wa kisiasa wanaoteswa magerezani kwa uonevu.

Wanamtaka Rais Azali awaache wakimbizi wa kisiasa walioko nje warejee Comoro bila masharti yoyote, na mwisho akewe mazingira mazuri ya amani yenye kurejesha haki na uhuru wa watu.

Wanamtaka Rais Azali arejee kwenye utaratibu wa kuiheshimu katiba ya nchi kwa kuzingatia Makubaliano ya Fomboni yaliyoasisi utaratibu wa kuwa na rais wa Comoro kwa mzunguko wa visiwa.

Anatakiwa pia aache kuingilia taratibu za kumpata rais wa Comoro kwa kuwapa nafasi wananchi ya kuamua nani wanataka awe kiongozi wao.

Jumuiya ya kimataifa, wadau wa maendeleo na marafiki wa Comoro wanatajwa kama wadau wakuu wa kuipata Comoro yenye ustawi, usawa na haki.

By Jamhuri