Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo – Busisi) lenye urefu wa Kilomita 3.0 na barabara unganishi Kilomita 1.66 linatarajiwa kuanza kutumika Tarehe 30 Disemba 2024 likiunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita zenye urefu wa Kilomita 90.
Daraja hilo linajengwa Urefu wa kilometa 3.0 Upana meta 28.45; unaojumuisha njia mbili (2) za Magari (Carriageways) zenye upana wa meta 7.0 kila upande, njia ya maegesho ya dharura meta 2.5 kila upande, njia za watembea kwa miguu (Walkways) meta 2.5 kila upande, eneo la kati linalotenganisha uelekeo tofauti wa barabara (Median) meta 2.45, kingo za magari (GuardRails Kerbs) meta 0.5 kila upande, na kingo za watembea kwa miguu (HandRails Kerbs) meta 0.5 kila upande.
Akizungumza mara baada ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa daraja hilo Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania – TANROADS Mkoa wa Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose amesema kuwa daraja hilo linajengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation ikishirikiana na China Railway 15 Bureau Group Corporation (CCECC – CR15G JV) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 592.6 bila 18% VAT.
Amesema kuwa kwa ujumla Mradi huo umeshatoa jumla ya ajira 29,211 tangu kuanza kwake tarehe 25 Februari 2020 ambapo asilimia 93.33 sawa na ajira 27,262 ni Wazawa na ajira 1949 sawa na asilimia 6.67 ni Wageni.
Amebainisha kuwa Utekelezaji wa Mradi huo umefikia asilimia 88.61 dhidi ya 91.70% ya Mpango kazi Na. 5 ulioidhinishwa huku Vifaa na mitambo ya ujenzi vilivyofika eneo la kazi hadi sasa vimefikia asilimia 99.
Mhandisi Ambrose amezitaja faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa daraja hilo kuwa ni pamoja na kupunguza muda wa kusafiri na uwepo wa uhakika wa usafiri masaa 24, kuondoa msongamano wa magari uliokuwa unatokea kwenye feri, Litakuwa kiungo muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na Mikoa inayouzunguka pamoja na Nchi Jirani na pia Daraja hilo litakuwa kivutio muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na ni nembo kwa nchi ya Tanzania.
Mhandisi Ambrose ameeleza kuwa Usanifu wa daraja hilo umetumia teknolojia ya madaraja marefu (Long Span Bridges), inayoitwa “Extra Dosed Bridge” ambapo kutakuwa na Nguzo Kuu (Pylons) tatu (3) zenye kimo cha mita 40 na umbali mita 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Amesema Daraja litakuwa na nguzo nyingine 64, ambapo 2 kati ya hizo zitakuwa umbali wa mita 100 kutoka nguzo moja hadi nguzo kuu wakati zilizobaki zitakuwa umbali wa mita 40 kutoka nguzo moja hadi nyingine na Jumla ya nguzo katika daraja lote zitakuwa ni 67.
Kila Nguzo ya Daraja ina nguzo za msingi (pile foundations) zilizochimbiwa ardhini kwa urefu wa kati ya mita 11.5 na mita 66, vilevile kutakuwa na Barabara unganishi yenye njia mbili zenye upana wa mita 7 kila upande kwa ajili ya magari na mabega ya mita 2.5 kila upande wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1.66 (Upande wa Kigongo kilometa 1.16 na upande wa Busisi mita 500).