Na Mwamvua Mwinyi JamhuriMedia ,Pwani

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti,Kanal Joseph Kolombo ameagiza kufuatiliwa na kukamatwa , wazazi waliomtelekeza mtoto wao mwenye ulemavu wa viungo ,Theresia Moses tangu akiwa na miezi sita ,huku wao wakiendelea kula bata.

Ameeleza, taarifa zilizotolewa na mtoto huyo,wazazi wake wapo Wilaya ya Temeke, hivyo atawasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mobhare Matinyi ili wazazi hao watafutwe.

Akifunga mafunzo ya miezi mitatu ya operesheni miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa ,kikosi cha 832 KJ ,Ruvu JKT , Mlandizi mkoani Pwani, Kolombo alieleza ,kitendo hicho ni cha ukatili .

“Haiwezekani mzazi ukamnyanyapaa mtoto wako uliemzaa,huo ni ukatili mkubwa, unaacha mtoto wako anataabika ,analelewa na majirani na bibi, halafu nyie mnaendelea kula bata , haiwezekani “

“Nitaongea na DC Temeke, wazazi hawa wafuatiliwe ,eti mama kisa kazaa mlemavu katelekeza kichanga cha miezi sita na kwenda kuolewa na mwanaume mwingine”alifafanua Kolombo.

Aidha alitoa rai kwa vijana waliomaliza mafunzo hayo kuzingatia kiapo ,wawe watiifu,waaminifu na wasijiingize katika matumizi mabaya ya mtandao na uvunjifu wa amani.

“Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi kwa vijana kupata mafunzo haya kwa upana wake, kujifunza kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara,uzalishaji na kijana kuwa mlinzi katika jeshi la akiba.”anasisitiza Kolombo.

Akimwakilisha Mkuu wa Majeshi, Brigedia Jenerali Geofrey Nyoni ,Tawi la Udhibiti na ukaguzi wa fedha JWTZ aliwataka vijana hao kuwa wazalendo na nchi yao.

Nyoni aliwaambia, dhana ya uzalendo,mshikamano,umoja na nidhamu ikawe silaha wakiwa ndani ya jamii.

Nae Kamanda Kikosi Cha Ruvu JKT, Kanal Peter Mnyani alieleza, mafunzo hayo waliyopatiwa vijana hao ni kwa mujibu wa sheria.

Amesema, mafunzo hayo yalianza Juni 19 mwaka huu ,yamedumu kwa miezi mitatu,ambapo wamefundishwa kuwa wazalendo kwenye nchi yao,watii,wawe na umoja, kujifunza mambo ya uzalishaji,kujiajili na kulinda nchi yao na kuwa na maadili mema.

Mnyani alieleza, katika mafunzo hayo walishiriki vijana wenye makundi maalum akiwemo Theresia Moses.

“Theresia tulimpokea na wenzake lakini yeye historia yake ni tofauti,baada ya kuzaliwa kufika miezi sita mama yake alimnyanyapaa ,alimtelekeza na kumuacha kwenda kuolewa kwingine,”

“Lakini baba yake alimuacha kwa bibi yake ambae nae ana maisha yake mengine,huwa akimuona wakati akienda kumsalimia mama yake yaani bibi wa Theresia, majirani walimsaidia na kusoma hadi kufikia sekondari Jangwani,sasa kapata mafunzo ya JKT na bado anahitaji msaada”alibainisha Mnyani.

Mnyani alitoa milioni moja mtoto huyo,na baadhi ya wananchi waliofika katika shughuli hiyo ya kufunga mafunzo walichangia na kupata zaidi ya milioni tatu.

Katika kumchangia Theresia pia kundi la operesheni Kambarage waliahidi kumpatia milioni moja na kuwa walezi wa Theresia kuanzia sasa.

Akishukuru Theresia amempongeza Rais Samia kwa kuendeleza mpango huo wa mafunzo ya JKT kwa vijana na makundi maalum ambao nao wanauhitaji huo.

Anamshukuru Kanal Mnyani kwa kumbeba ,na vijana wengine katika kikosi ,ambapo ameongeza kwamba hajawahi kumuona mama yake mzazi ,akipatikana hana tatizo ameshamsamehe .

Theresia aliiomba jamii ,wazazi waache tabia ya kunyanyapaa watoto wao wenye ulemavu kwani ni matakwa ya Mungu ,na watoto hao Wana haki ya malezi Kama wengine wasio na ulemavu.

By Jamhuri