Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Mobhare Matinyi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa wilaya hiyo huku akitumia nafasi hiyo kueleza fedha ambazo Rais amewapatia mwaka jana Sh bilioni 152 na kati hizo Sh bilioni 43.7 zilitumika kujenga barabara.
Matinyi ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mbagala Zakhiem na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kufanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Mkuu wa Mkoa tunaomba utufikishie salamu zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, fedha ambazo amtupatia katika mwaka wa fedha ulioisha Juni mwaka huu zimetuwezesha kufanya mambo makubwa ya maendeleo. Rais alitupatia Shilingi bilioni 152 na kati ya hizo fedha tumezitumia kujenga barabara.
“Mkuu wetu wa Mkoa leo umejionea mwenyewe katika kila mtaa tuliokuwa tunakatiza ni lami kama sio lami ni zege. Lakini mbali ya ujenzi wa miundombinu ya barabara Shilingi bilioni 61.6 zilitumika katika miradi ya umeme katika wilaya yetu tunayo wilaya kubwa hasa kwa idadi ya watu, eneo linaweza lisiwe kubwa baada ya kumega eneo la kuwasaidia ndugu zetu wa Kigamboni
“…Wilaya ya Temeke inakaribia watu milioni 1.4 sasa huduma za jamii zinahitaji fedha nyingi na ndio maana Rais wetu amekuwa akitupatia fedha hizo. Upande wa maji kwa mwaka wa fedha uliopita zimetumika Shilingi bilioni 15.5 na kwasababu tuna watoto wengi Rais alitupatia Shilingi bilioni 7.6 zilizotusaidia kwenye upande wa elimu ya msingi tu ambapo shule sita madarasa 147, matundu ya vyoo, madawati na vifaa mbalimbali tumefafanikisha kupitia fedha hizo,”amesema Matinyi.
Aidha amesema katika Shule za Sekondari, wilaya hiyo kiwango cha ufaulu kitoka shule za msingi kwenda sekondari kiko juu ya asilimia 95, hivyo wana mahitaji makubwa ya shule za sekondari lakini Rais Samia aliwapatia Sh bilioni 10.
Pia ameeleza kwenye upande wa afya Rais aliwapatia Sh bilioni 6.1 na hizo hazijumuishi ambazo alivyoona Mkuu wa mkoa wakitembelea hospitali.
“Hii inaonesha Rais anavyowajali wananchi wa Temeke, tunakuomba fikisha shukrani zetu kwa Rais na tunamhakikisha kila senti inayokuja Temeke itatumika kama alivyokusudia.”