Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile ametoa pongezi kwa Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama pamoja na Mbunge viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Jacklin Ngonyani Msongozi kwa juhudi zao na ushupavu wa kuwatumikia wananchi.

Pongezi hizo amezitoa jana kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya soko kuu manispaa ya Songea ambapo mkuu huyo wa Wilaya alikuwa Mgeni rasmi.

Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile akizungumza kwenye uzinduzi wa siku ya Wanawake Duniani katika viwanja vya soko kuu Manispaa ya Songea.

Alisema kuwa kazi nzuri wanazofanya Jenista na Msongozi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwenye maeneo yao, na namna wanavyowajali wananchi katika mikakati mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ni ya kuthaminiwa.

“Niseme tu ukweli huyu Mbunge Msongozi akitoka safari lazima apite ofisi za mkuu wa Mkoa alafu atapita ofisini kwangu atasalimia na kuhoji tunachangamoto gani, lakini huyu Mbunge wananchi wakimtumia ujumbe tupo mtaa wa makambi nyumba zinataka kubomoka ananitumia na mimi mkuu wa Wilaya hata kama yupo Dodoma vivyo hivyo kwa Mbunge Jenista Mhagama akitumiwa tu ujumbe wa maafa hawezi kubaki na ujumbe huo peke yake lazima anitumie “alisema Kapenjama

Alisema kuwa huo ni uwajibikaji mzuri wa wabunge kwa kuwa wanachukuwa hatua za kutatua kero za wananchi na kwamba inadhihirisha jinsi wanavyojihusisha na masuala ya maendeleo ya wananchi wanaowatumikia.

Alieleza zaidi kuwa wabunge wenye utendaji kama huu mara nyingi huleta mabadiliko chanya katika maeneo yao kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wananchi pia ni mfano mzuri kwa wabunge wengine nchini.

“Wabunge shupavu kama Jenista Mhagama na Msongozi wanastahili pongezi kwa juhudi zao za kusikiliza na kutatua matatizo ya wananchi japo kuwa wakati mwingine kazi ya Mbunge inakuwa ngumu lakini wanapojitahidi kutatua changamoto za wananchi na kuleta maendeleo katika majimbo yao wanastahili kuthaminiwa na kupongezwa” alisema mkuu huyo wa Wilaya Kapenjama.

Mbunge viti maalum Mkoa wa Ruvuma Jacklin Ngonyani Msongozi akihutubia Wanawake wa Mkoa wa Ruvuma.

Hata hivyo alisema kuwa kila mwaka kuna kuwa na kauli mbiu na kauli mbiu ya mwaka huu inasema “wanawake na wasichana mwaka huu wa 2025 tuimarishe haki,usawa na uwezeshaji” hivyo wewe kama mwanadamu haki na usawa vinajulikana ikiwemo haki ya kuishi na kusikilizwa.

Prisca Kaponda akisoma risala kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kimkoa wa Ruvuma alisema kuwa siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka kote ulimwenguni ambapo katika kusherekea wanawake wanaungana pamoja kufanya tathimini ya utekelezaji wa azimio la ulingo wa Beijing kwa kutafakari namna mafanikio yaliyopatikana kwa wanawake na wasichana katika nyanja zote za maendeleo.