Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.
Waziri wa Katiba na Sheria Dk . Damas Ndumbaro amesisitiza umuhimu wa kutambua, kukumbuka, na kuheshimu mchango wa mwanamke katika maendeleo ya dunia ya leo.
Alisema kuwa kwa sababu wanawake wanachangia katika kukuza pato la Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, siasa, uchumi, na jamii kwa ujumla.

Alisema kuwa kutoka na mchango huo Wanawake wanapaswa kuthaminiwa na kuenziwa ili kuendeleza usawa na maendeleo endelevu katika jamii.
Dk. Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini ameyasema hayo leo kwa njia ya simu kufuatia Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika mkoani Arusha na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
” Tunapaswa kutambua ,kukumbuka na kuheshimu mchango wa mwanamke katika maendeleo ya Dunia ya leo,bila mwanamke hakuna maisha Bob Marley aliwahi kuimba ” No woman no Cry” akimaanisha bila mwanamke hakuna mtoto atakayezaliwa.” Alisema Dk. Ndumbaro.
Hata hivyo wakati tunaposherekea siku ya Wanawake sekta zinazohusu masuala ya kisheria zinapaswa kuhakikisha zinapambana na Sheria kandamizi zinazodidimiza mkakati wa Maendeleo ya Wanawake.

