Na Mwandishi Wetu

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeandaa Mkutano Mkuu Maalum wa wanachama wake wote, ambao umepangwa kufanyika Aprili 3 – 5, 2025, katika Manispaa ya Songea, mkoani
Ruvuma.

Mgeni rasmi katika mkutano huo wenye kauli ya ‘Uchaguzi Huru na wa Haki’ anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais wa CCM kwa mwaka 2025, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 07, 2025 na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imeeleza kuwa, Mkutano huo ni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa viongozi kwa kuzingatia Ibara ya 7.8 ya Katiba ya TEF, ambapo muda wa uongozi wa sasa unafikia tamati mwaka huu, baada kuwapo madarakani kwa miaka minne tangu Mei 2021.

“Tunatarajia kwamba Balozi Nchimbi, atafungua Mkutano huu, Aprili 4, 2025 na uchaguzi wa Viongozi wa TEF utafanyika Aprili 5, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Imebainisha kuwa na nafasi ambazo viongozi wake watapigiwa kura kwa mujibu wa Katiba ni tisa (9) ambao ni Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti na wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji (KUT) ya TEF.

“Fomu za kuomba nafasi za uongozi zitaanza kutolewa rasmi Jumatatu Machi 10, 2025 kwenye Ofisi za TEF. Siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu itakuwa ni Jumatatu ya Machi 24, 2025, saa 10:00 jioni.

“Mgombea atarejesha fomu pamoja na picha ndogo (passport size) ambayo itatumika kwenye karatasi ya kura ikiwa atateuliwa kuwania nafasi anayoomba.
Muda wa kuchukua na kurejesha fomu ni kuanzia saa 03:00 asubuhi – 10:00
jioni kwa siku za kazi. Hii inamaanisha kwamba fomu hazitatolewa wala
kupokelewa Jumamosi, Jumapili wala siku za Sikukuu,” imeeleza taarifa hiyo.

Imefafanua kuwa, ada ya fomu za uongozi ni Sh.150,000 kwa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na Sh. 100,000 kwa nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.

“Utoaji na urejeshaji wa fomu za kuomba uongozi utasimamiwa na Sekretatieti ya Jukwaa la Wahariri (TEF) chini ya Ofisa ya Mtendaji Mkuu. Kamati ya Uchaguzi itaongozwa na Frank Sanga (Mwenyekiti) na wajumbe wengine wawili ambao ni Angela Mang’enya na Rashid Kejo.

“Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TEF, Kamati hii ndiyo yenye wajibu wa kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ikiwa ni pamoja na vigezo na sifa za wagombea. Tunashauri wanachama wote na hasa wale wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi, wasome Kanuni za Uchaguzi na kuzielewa,” imeeleza taarifa hiyo.