Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
UTAFITI uliofanywa hivi karibuni umeonesha kuwa endapo gesi asilia itatumika kwa kiasi kikubwa kwenye usafiri na usafirishaji gharama za maisha zitapungua.
Hayo yameelezwa kwenye ripoti ya Utafiti huo uliofanywa na Dkt. Achilana Mtingele akishirikiana na Wilfred Mwakalosi, walipowasilisha mada kuhusu Utafiti huo katika Kongamano la 11 na maonesho ya Petroli nchi Wanachama Afrika Mashariki (EAPCE’25).
Akizungumza mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu utafiti huo, Mwakalosi ambaye ni Afisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) amesema kuwa utafiti huo wameufanya kuanzia Septemba 2024 hadi Januari 2025, ambapo ulilenga kuchunguza kutakuwa na faida gani za kiuchumi na kijamii iwapo nchi itaamua kutumia kwa kiwango kikubwa gesi asilia kwenye usafiri na usafirishaji.
“Ni Utafiti ambao upo katika kundi la namna ambavyo Nchi za Afrika Mashariki zinaweza zikachanganya vyanzo vya nishati ili kuleta unafuu. Tulikuwa tunataka kuangalia hivyo kwasababu kama mnavyofahamu sekta ya usafiri ndio kila kitu, usafiri gharama yake ikiwa kubwa hata mbolea kufika Songea itakuwa gharama kubwa, hata mafuta yenyewe kuyasafirisha gharama yake itakuwa kubwa.
“Bei za bidhaa mbalimbali jinsi zinavyokuwa kubwa zinakwenda kuathiri kwenye mfumuko wa bei. Kwahiyo tulikuwa tunaangalia je kama gesi asilia ambayo inapatikana nchini, itatumika kwenye usafiri na usafirishaji itaweza ikawa na manufaa gani kwa kuzingatia gharama yake iko chini sana,” amesema.
Utafiti unaonesha kuwa mwaka 2022, Tanzania ilitumia Dola za Kimarekani milioni 2,447.4 ambazo ni sawa na asilimia 20.8 ya fedha zote zilizotumika kuagiza bidhaa, mwaka 2023 zilitumika Dola 3,139 na mwaka jana zilitumika Dola 2,802.2 sawa na asilimia 20.3.
Amebainisha kuwa matokeo ya utafiti yameonesha kuwa endapo gesi asilia itatumika hasa kwenye usafiri wa umma mfano malori, mabasi, daladala ni dhahiri kuwa gharama za usafirishaji zitakuwa chini.
“Kama mtakumbuka wakati lita moja ya petroli au dizeli ni kati ya 2700, 2800 kilo Moja ya gesi asilia ni 1550. Hii maana yake, faida ya kwanza zile fedha za kigeni ambazo tunazitumia katika kuagiza mafuta tutakuwa tumeziokoa na zitafanya kazi nyingine.
“Lakini inamaana pia mfumuko wa bei ambao unasababishwa mara kwa mara na gharama za usafiri na wenyewe utakuwa umedhibitiwa kwa kiasi fulani. Haya yote yanaonesha pia Watanzania wanaweza wakawa na hali bora zaidi na gharama za maisha zitapungua kwasababu gharama za usafiri zitakuwa zimepungua,” amesema.
Aidha ametoa wito kwa Serikali kutengeneza Sera ambazo zitatoa kipaumbele matumizi ya gesi Asilia nchini.
Amefafanua kuwa, sera hiyo pia ielekeze vyombo vya usafirishaji vianze kutumia nishati ambayo itakuwa nafuu zaidi ambayo ni CNG.
“Na Kwa kuanzia hata serikali yenyewe ambayo ina magari mengi ikiamua kuonesha nia ya dhati kwa kubadilisha au ikaingiza magari mapya ambayo ikaamua yatumie gesi asilia maana yake tutakuwa tumeokoa fedha nyingi za kideni ambazo zinatumika kuagiza mafuta nje ya nchi.
“Kutokana na hayo inamaana sasa itawezekana kutoa unafuu katika Uwekezaji katika vituo vya CNG. Pia kupitia sera hizo hizo tutaona itawezekana hata kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutambua magari yanayoingia nchini na yanatumia CNG,” amesema na kuongeza kuwa:
“Sasa hivi ukienda katika ukokotoaji wa kodi kwa TRA anatambua magari yanayoendeshwa hapa kwa petroli au dizeli…kwahiyo ukija na gari yako ya CNG huwezi kupata unafuu wowote kwasababu bado katika mifumo yetu hiyo haitambuliki,” amesema.
Amebainisha kuwa, hadi sasa kuna vituo sita vya CNG ambavyo vipo kati ya Mtwara, Dar es Salaam na Lindi.
“Hivi vituo havitoshi, kwahiyo kama tukijitahidi kutoa gesi Mtwara ikaja Dar es Salaam, pia tunaweza kutoa gesi Dar es Salaam kuelekea maeneo mengine,” amesema.
