Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA), imekamata kilogramu 4.623 za aina mpya ya dawa za kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV), iliyokamatwa Dar es Salaam ikisafirishwa na raia wa Comoro Ahmed Bakari Abdou mwenye umri wa miaka 32.

Akitolea ufafanuzi wa operesheni hiyo leo Aprili 4, 2024, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wamekamata kilogramu 54,504.553 za dawa za kulevya za mashambani na viwandani.

Dawa hizo ni bangi kilo 54,489.65, mirungi kilogramu 10.3, heroin gramu 90.93, na cocaine gramu 1.98, ambapo mamlaka imeteketeza mashamba 262 ya bangi katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya na Tabora kwa mwezi Februari na Machi mwaka huu.Watuhumiwa 72 wamekamatwa na baadhi yao wamefikishwa mahakamani.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema MDPV ni aina mpya ya dawa ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu ambayo inaweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji kwa kuwa imeongezwa nguvu ya kilevi.

“Dawa hii ya kulevya huuzwa kwa mtandao na kusafirishwa kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi na hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama vile, Ivory Wave, plant fertilizer, Vanila Sky, na Energy,” amesema Kamishina Jenerali Lyimo.

Amesema wamebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga, na Mabatini mkoani Tabora ambapo wahusika wamekata miti katika misitu hiyo kulima dawa hizo.

“Kwa ushirikiano tulioupata kutoka Wakala wa Misitu (TFS) tumefanikiwa kuteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusika,” ameongeza.

Amesema mamlaka hiyo imekusudia kufanya operesheni katika mikoa yote kuhakikisha dawa za kulevya zinazozalishwa nchini ikiwemo bangi na mirungi mashamba yake yanateketezwa.

Aidha amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za wahusika wanaolima dawa hizo katika mikoa yote nchini ambayo inapelekea kuharibu uoto wa asili na misitu.

By Jamhuri